Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 25 Mei 2015 21:41

Mazazi ya Imam Hassan (as) tarehe 3 Sha'aban

Mazazi ya Imam Hassan (as) tarehe 3 Sha'aban

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuzaliwa Imam Hussein (as), mjuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw), karibuni.

Tarehe Tatu mwezi Sha'ban mwaka wa nne Hijiria, mji wa Madina ulishuhudia mazazi ya mtoto kutoka familia ya Utume. Hii ni familia ambayo baada ya kushuka aya ya Tat'hir ambayo ni ya 33 ya Surat Ahzab, kwa mara kadhaa Mtukufu Mtume alikuwa akiwasalimia na kuwaita watu wake kuwa ni 'Ahlu Baytin-Nubuwwat' yaani Watu wa Nyumba ya Utume. Katika siku ya furaha ya tarehe Tatu mwezi Sha'ban, Mtukufu Mtume alikuwa amesimama kando ya chumba cha Bibi, Fatwimat Zahraa (as) akisubiri kuchomoza nuru ambayo si nyingine ila ni kuzaliwa Imam Hussein (as). Na wakati mtoto huyo alipozaliwa, Mjumbe wa Allah Muhammad (saw) alipaza sauti kwa kusema: 'Ewe Asma! Niletee mwanangu.'  Bi Asma, akasema: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Bado sijamsafisha'. Mtume akauliza katika hali ya mshangao: 'Kwani wewe ndiye unayemsafisha'! Hapo Bi. Asma akawa amediriki malengo ya Mtukufu Mtume kusema vile na kisha akamleta Imam Hussein kwa Mjumbe wa Allah. Mtume alimkumbatia na kumbusu na kisha akaanza kuzungumza taratibu na mtoto mchanga huyo ambaye ndio kwanza alikuwa amezaliwa (tazama kitabu cha Biharul-Anwar juzu ya 23). Wapenzi wasikilizaji  sanjari na kutoa mkono wa kheri na baraka kwa kuzaliwa Imam Hussein, nakukaribisheni kujumuika nami katika dakika hizi chache za kipindi hiki ambacho kutazungumzia kwa ufupi nafasi na fadhila za mtukufu huyo, karibuni.

********************************************

Kwa hakika Imam Hussein alikuwa kipenzi cha Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Ni Imam Hussein ndiye alikuwa akiingiza furaha na utulivu katika moyo wa Mtume kila pale mtukufu huyo alipokuwa akimkumbatia mjukuu wake huyo. Mtoto huyo Hussein (as) aliweza pia kupata kumbukumbu nzuri kutoka kwa babu yake huyo Mtume Muhammad (saw). Wakati mwingine mtoto huyo alikuwa akipanda mabegani kwa Mtume na wakati mwingine Mtume (swa) alikuwa akimbeba mikononi mwake na kwenda naye huku na huko. Watu wote walikuwa wakishuhudia namna Mjumbe huyo wa Allah alivyokuwa akibusu paji la uso wa Imam Hussein (as). Mbali na hapo Mtukufu Mtume alikuwa akizungumza na mtoto huyo kwa lugha ya kitoto na kwa mapenzi ya hali ya juu. Mapenzi hayo yalifikia kiasi cha kuwashangaza masahaba. Hata hivyo Nabii wa Allah alikuwa akiweka wazi sababu ya yeye kufanya hivyo kwa kusema: “Upole na mapenzi yaliyofichika moyoni mwangu, ni zaidi ya kile mnachokishuhudia nyinyi dhahiri.” (Tazama Biharul-Anwaar juzu ya 43). Kwa maneno hayo Mtume aliweka wazi uhakika huu kwamba, mapenzi yake kwa mtoto huyo, hayakuwa mapenzi ya kawaida, kama vile ambavyo pia hayakuwa ya kifamilia tu. Bali yalikuwa mapenzi yaliyotokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kama mnavyojua, Mtume wa Mwenyezi Mungu hakuwa mtu wa kawaida kama watu wengine. Kwa mujibu wa Qur’an Tukufu, Nabii Muhammad hakufanya jambo wala kutamka kitu kwa matamanio yake binafsi. Qur’an inasema: “Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa hayo ila ni ufunuo uliofunuliwa.” Surat Najm aya ya 3-4. Ni katika mtazamo huo ndipo Mwenyezi Mungu akasema: “Hakika nyinyi mnayo ruzawa (kiigizo) njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.” Surat Ahzab aya ya 21.

Aidha mapenzi hayo ya hali ya juu ya Mtume Muhammad kwa Imam Hussein (as), ni suala ambalo limebainishwa katika vitabu tofauti vya Ahlu Sunnah wal Jamaa. Katika moja ya riwaya  kumepokelewa kuwa, kundi moja la watu lilikuwa linaenda na Mtume katika dhifa, wakiwa wanatembea njiani, Nabii Muhammad (saw) akamuona Hussein (as). Mtume akataka kumkumbatia. Hata hivyo Hussein akawa anacheza na babu yake huyo kwa kukimbia upande huu na ule. Mtume akatabasamu kwa mandhari ile na hivyo naye akawa anamfuata mtoto huyo kwa kukimbizana naye, hadi pale alipomshika na kumkumbatia na kisha akambusu. Mtume akawageukia hadhira na kusema: “Enyi watu! Tambueni kwamba Hussein anatokana na mimi na mimi ninatokana na Hussein. Yeyote atakayempenda Hussein basi Mwenyezi Mungu naye atampenda.” Mwisho wa riwaya. (Tazama kitabu cha Musnad Imam Ahmad, juzu ya nne, Sunan Ibn Majah juzu ya kwanza na kitabu cha Manaqib Shahr Ashub, juzu ya tatu).

Katika upande wa pili, Imam Hussein alikuwa ni mwenye shakhsia ya hali ya juu kwa pande tofauti. Katika ukamilifu na ubora na hata katika ibada, alikuwa mtu aliyepiga hatua kubwa miongoni mwa watu. Mjukuu huyo wa Mtume alikuwa akizingatia sana ibada, kiasi kwamba, tangu alipokuwa mtoto mdogo na hata alipokuwa akikabiliana na ujahili wa Bani Umayyah, katika mahala na wakati wote daima alikuwa akimsabihi, akimshukuru na kumtakasa Mwenyezi Mungu, sanjari na kujishughulisha pia na kusoma Qur’an Tukufu. Akizungumzia ibada yake, mwanaye Imam Sajjad Ali bin Hussein (as) anasema: “Baba yangu Hussein bin Ali alikuwa akipitisha usiku kwa kurukuu na kusujudu sanjari na kunong’ona na Mwenyezi Mungu na kila siku alikuwa akifanya ibada.” Mwisho wa kunukuu.

*****************************************************

Mbali na ibada, Imam Hussein pia alikuwa msimamizi wa matukufu ya dini na mlinzi wa suna za Mtume Muhammad (swa). Mtukufu huyo katika kufikia malengo ya Kiislamu hakukuwa na shinikizo au kikwazo chochote ambacho kingerudisha nyuma azma yake hiyo. Aidha moja ya sifa maalumu za mtukufu huyo ni kupigania uhuru, kupambana na dhulma na ukandamizaji. Si tu kwamba Imam Hussein alikuwa mshindi katika kukabiliana na dhulma, bali pia alikuwa mwasisi wa mwenendo wa uhuru na ubinaadamu, ambaye wapigania uhuru wote, wanamapambano dhidi ya dhulma na wapigania uadilifu, wanapaswa kufanya harakati zao kwa kuiga mfano wa Imam Hussein (as). Hivyo ndivyo mtukufu huyo alivyoamiliana na siasa mbovu na za uongo, zilizoambatana na dhulma na ukandamizaji za Bani Umayya ambapo alipotakiwa kuchagua moja ya njia mbili ambazo ni ima akubali kuishi chini ya udhalili na dhulma, au njia ya ushujaa na ambayo ilisafisha historia kwa kuuawa kwake shahidi, Imam alisema kama ninavyonukuu: “Kamwe suala hilo halitatokea! Na Hussein hawezi kukubali kuwa chini ya udhalili.” Ni katika hali hiyo ndipo mtukufu huyo akasimama imara katika kukabiliana na dhulma ya mtawala Yazidi mwana wa Muawiya.

Kuheshimu shakhsia za watu ni sifa nyingine iliyotuama katika maisha ya Imam Hussein ambapo si tu kwamba alikuwa akichukia kuwafanyia dharau watu wahitaji, bali pia alikuwa akihisi aibu juu ya suala hilo. Imepokewa riwaya kwamba, mtukufu huyo alimuona mtu mmoja wa makamu ambaye alikuwa hajui kutawadha. Imam alihitaji kumuelekeza namna bora ya kutawadha lakini hata hivyo akahisi aibu. Hivyo akamtaka ndugu yake Imam Hassan (as) washindane kutawadha kwa njia sahihi na wakati huo wapate kumfundisha mzee yule namna bora ya kutawadha. Hivyo wakamtaka mtu yule awe mwamuzi baina yao. Baada ya kila mmoja kutawadha kwa njia sahihi mbele yake, hatimaye yule mzee akafahamu kuwa yeye ndiye aliyekuwa mkosaji na hivyo akasema: “Nyote wawili mmetawadha vizuri, na mimi ndiye ambaye nilikuwa sijui kutawadha kwa njia sahihi. Mmenifanya niweze kufahamu njia bora ya kupata udhu.” Mwisho wa riwaya.

Aidha Imam Hussein anasifika kwa kuchunga haki za watu wengine. Imenukuliwa kuwa, mtu mmoja kwa jina la Abdu Rahman alimfundisha Surat al-Fatiha mmoja wa watoto wake. Baada ya kazi hiyo Imam Hussein akampatia kiasi cha dinari elfu moja, nguo elfu moja na zawadi nyinginezo kama haki yake kwa kazi yake hiyo bora. Wakati mwalimu yule aliposhangazwa na zawadi zile na namna gani mtukufu huyo alivyochunga na kuheshimu haki ya kimaanawi ya walimu, Imam akamwambia: “Zawadi hizi ni chache kwa adhama na utukufu wa kazi yako.” Mwisho wa kunukuu.

***************************************************

Moja ya sifa maalumu nyingine za mtukufu huyo, ni upole na mapenzi ya hali ya juu kwa watu wengine, hususan kwa watu wale ambao walikuwa wakikumbwa na misukosuko ya kimaisha au matatizo mengineyo. Kuhusiana na suala hilo imepokewa kuwa, Imam aliumzuru Osama bin Zaidi nyumbani kwake. Imam akamuona Osama katika hali ya huzuni nyingi na hapo akamuuliza sababu ya huzuni yake. Wakati huo Osama akaamua kuweka wazi kiini cha huzuni yake kwa kusema: “Nina haki za watu juu yangu. Ninadaiwa na ninatamani kabla sijafariki dunia, niweze kulipa deni la mtu na nisifariki nikiwa nina deni.” Baada ya hapo Imam Hussein akaamuru haraka deni la Osama lilipwe na baadaye akafariki dunia akiwa ni mwenye furaha.

Aidha mbali na hapo Imam Hussein alikuwa akibeba mgongoni kwake mahitaji ya watu masikini, wasiojiweza, mayatima na vipofu na kuyapeleka hadi kwenye milango ya nyumba zao. Ni kwa ajili hiyo ndipo alipouawa shahidi Karbala, mwili wake ulikutwa na athari zilizotokana na kubeba mizigo mizito. Wakati watu walipomuuliza Imam Sajjad sababu ya alama zile, alisema kuwa zilitokana na baba yake huyo kubeba sadaka kwa uficho majira ya usiku na kuwapelekea yatima na watu masikini katika jamii.

Wapenzi wasikilizaji muda uliotengewa kipindi chetu hiki maalumu cha kumbukumbu ya kuzaliwa mjukuu wa Bwana Mtume Imam Hussein (as), umefika tamati. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wapenzi wa Mtume Mtukufu (saw) na Watu wa Nyumba yake toharifu (as). Mimi ni Sudi Jafar Was-Salamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …