Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Mei 2015 20:32

Abul Fadhl Abbas AS, shujaa muungwana

Abul Fadhl Abbas AS, shujaa muungwana

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum. Tuko katika siku ya kukumbuka kuzaliwa Hadhrat Abul Fadhl Abbas AS na tunawakaribisha kusikiliza makala hii maalumu ambayo tumekutayarishieni kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS na ambaye alikuwa jemedari shujaa na nguzo muhimu ya Imam Hussein AS katika mapambano ya Karbala.

Abul Fadhlil Abbas Alikuwa mtu mwenye uso  wa kuvutia, aidha alikuwa na maadili bora na moyo mkunjufu. Dhahiri na batini yake zote zilijaa nuru ya kipekee na mvuto wa aina yake.  Dhahiri yake iliashiria batini yake. Alikuwa mtu mwenye nuru ya aina yake na miongoni mwa ukoo wa Bani Hashim alitambulika kwa uzuri wake ulioangazia kila mahala. Abul Fadhl aling'ara kama mbalamwezi na ndio sababu akapewa lakabu ya 'Mwezi wa Bani Hashim' yaani 'Qamar Bani Hashim'.  Abul Fadhl Abbas AS hakuwa mtu mwenye nguvu na kimo kirefu na nuru mithili ya mbalamwezi tu bali pia alikuwa shakhsia mwenye fadhila na karama.  Alikuwa na taqwa imara na imani sambamba na kuwa shujaa na bingwa mkubwa katika Uislamu.

Imam Ja'afar Sadiq AS ananukulu kutoka kwa Mtume Muhammad SAW kuwa: "Mashujaa waungwana  katika umma wangu  wana sifa 10, ni wasema ukweli, wenye kutekeleza ahadi, kufikisha amana, hawadanganyi, huwa warehemevu kwa mayatima, husaidia wasiojiweza, hutoa walichonacho, huzidi kwa wema, hualika wageni, na ni wenye haya."

Tunaweza kusema kuwa sifa ya ukarimu wa shujaa muungwana ni itikadi ya kimaisha. Shujaa muungwana katika Waarabu wa kale alikuwa ni mtu aliyefika katika kilele cha  ushujaa na ukarimu. Kila aliyejitahidi kukuza na kustawisha sifa hizo mbili alizidi kupanda daraja kama shujaa muungwana. Katika upeo wa kijamii shujaa muungwana ni yule ambaye daima hujitolea muhanga na kujinyima kwa ajili ya wengine. Shujaa muungwana hujitahidi kujinyima ili watu wengine wa kawaida waweze kuishi vizuri. Aidha hujitolea kuwasaidia waliodhulumika katika mapambano na madhalimu. Imam Ali AS alikuwa mwanzilishi wa ushujaa wenye uungwana.  Katika riwaya tunasoma kuhusu ushujaa, ujasiri na uungwana wa Imam Ali AS kuwa: "Siku moja alimwambia Abdulrahman ibn Muljim, 'wewe ndiye utakayeniua.' Ibn Muljim akasema,'basi niuwe ili nisitende kitendo hicho.' Ali AS alijibu, 'njia yetu ni kuwa  sisi husamehe baada ya dhambi, si kabla ya dhambi."

Moyo wa  kudumu wa ujasiri, kujitolea muhanga na ushujaa unaoandamana na uungwana ulidhihirika katika shakhsia ya Hadhrat Abul Fadhl Abbas AS mwanae Imam Ali AS. Alieneza katika jamii thamani za ubinadamu, maadili bora, haki na uadilifu na pia aliweza kuleta mabadiliko ya kifikra na kimaadili katika jamii. Hizi ni thamani ambazo daima wanaadamu wana hamu ya kuziona katika jamii hata kama huwa vigumu kuzitekeleza kivitendo.  Historia imesajili majina ya watu mashuhuri ambao walikuwa chanzo cha mabadiliko kivitendo. Lakini kile kinachomtenganisha Abul Fadhl Abbas AS na wengine ni ikhlasi safi na mapenzi ya kweli aliyokuwa nayo na hivyo kumpelekea afanikiwe katika kufikia uadilifu, haki na imani imara. Mapambano yake yaliandamana na subira na hatimaye mafanikio yake kuweza kufaidisha vizazi vilivyofuata. Imani yake, uono wa mbali na utiifu ni nukta zilizompa umashuhuri na hivyo kumfanya kuwa  mwanaadamu mwenye hadhi ya juu na anayestahiki kuwa kigezo. Aliweza kutajwa na Ahul Bayt wa Mtume SAW kuwa ni kigezo. Abul Fadhl Abbas AS alipitisha miaka 14 ya umri wake akiwa na Imam Ali AS; hicho kilikuwa ni kipindi ambacho Amirul Muminin alikuwa akikabiliana na maadui. Inasimuliwa kuwa Hadhrat Abul Fadhl alikuwa akishiriki katika baadhi ya vita akiwa barobaro wa takribani miaka 12. Hapo ndipo alipoanza kupata malezi ya kumuandaa kuwa shujaa muungwana.

Fahari kubwa zaidi ya Abbas bin Ali katika umri wake wote ilikuwa ni kuhudumia Uimamu na msingi wa wilaya haswa Imam Hussein AS. Alikuwa na nafasi ya kipekee kama nguzo muhimu na yenye kutegemewa na ndugu yake, Sayyid As Shuhadaa yaani Bwana wa Mashahidi, Imam Hussein AS. Alipambana kwa ushujaa na ujasiri bega kwa bega na ndugu yake na hivyo taswira yake ya kipekee ya ushujaa na uono wa mbali ikabakia milele.

Hadhrat Abul Fadhl AS alikuwa pia na shakhsia ya kipekee katika uga wa maarifa na elimu. Kuhusu hadhi yake ya kielimu imetajwa kuwa: "Abbas AS alikuwa faqihi wa wana wa Maimamu Alayhima Salam."

Alikuwa mtu mwenye uwezo uliotakasika na mwenye kudiriki kwa kina kwani chimbuko la elimu yake alikuwa ni Amirul Muminin Ali AS. Akiwa na umri wa miaka mitano alikuwa akikaa mbele ya baba yake kupata elimu na maarifa.  Adabu huwa inachukua muelekeo maalumu na maridadi inapoandamana na unyenyenyekevu na mapenzi.  Wanazuoni wanasisitiza kuwa malezi ya Kiislamu hasa adabu inamuwezesha mwanadamu kuwaheshimu na kuwazingatia wenzake. Hivyo hata wale wenye hadhi ya juu huwa ni wenye kuwaheshimu walio chini yao. Ali AS alisisitiza sana kuhusu thamani hii na alisema: "Hakuna turathi yenye thamani zaidi ya adabu."

Hadhrat Abul Fadhl Abbas AS alikuwa akitelekeza nasaha na muongozo wa baba yake kwa njia bora zaidi kiasi kwamba jina lake likawa linaandikwa katika dibaji ya vitabu vilivyokuwa na maudhui za ushujaa, adabu na unyenyekevu. Katika kipindi cha umri wake wote, mtukufu huyo kamwe hakuwaita ndugu zake kwa jina lao au jina la utani bali alikuwa akiwaita kwa ibara za heshima na adabu kama vile mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, bwana wangu, mawlana n.k. Alikuwa akiwatazama kama Ahul Bayt wa Mtume SAW, wasiotenda makosa au maasoum na maimamu. Baada ya kuwa kwanza ametambua hadhi yao hiyo ndio aliwatazama kama ndugu na familia.  Aliamini kuwa undugu haupaswi kupelekea kusahaulika hadhi ya Uimamu na hii kwa hakika ilikuwa ni nasaha ya Bwana Mtume SAW ambayo Abul Fadhl Abbas aliitekeleza kikamilifu.

Imani na kumkumbuka Mwenyezi Mungu daima ni siri kubwa ya watu mashuhuri duniani katika mapambano yao na maadui wa Mwenyezi Mungu. Hii ndio nguvu pekee ambayo ikitegemewa, huangusha na kusambaratisha makasri makubwa na maadui na madhalimu. Mwanzoni mwa Ziyara ya Abul  Fadhl Abbas AS ambayo imebainishwa na Imam Sadiq AS  amemtaja kwa sifa za mwenye imani imara kwa Mola Muumba na mwisho imetaja imani yake ya kipekee na mwenye busara na uono wa mbali.

Hata kama Abul Fadhl AS hakuwa maasumu au asiyetenda makosa, lakini imani yake imara ilipelekea apate umaasumu usio rasmi wa kivitendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na hivyo sawa na maasumina wengine akawa ni mwenye kuwa mbali kabisa na dhambi. Ni wazi kuwa kila daraja ya imani inavyozidi kupanda, ucha Mungu hustawi na kuwa wa kina zaidi.  Abul Fadhl Abbas alikuwa mja wa kweli wa Mola Wake Muumba na ishara za ibada zilidhihirika katika uso wake uliotakasika.  Athari ya sijda zake ndefu ilionekana katika paji lake la uso kiasi kwamba aliyemuua alisema hivi: "Alikuwa na uso uliotakasika na athari ya sijda ilinga'arisha paji lake."

Ingawa kujitolea, ushujaa na ujasiri wake ni wa zaidi ya miaka 1,300 iliyopita lakini historia ingali imepambwa kwa fadhila zake Abbas bin Ali AS. Baada ya kupita karne nyingi, ushujaa wake ulioandamana na uungwana unaendelea kunawiri mbele ya vizazi vyenye kiu ya ukweli na haki. Alibainisha mapenzi na kujitolea muhanga kwa njia ya kipekee. Salamu ziwe juu ya mwezi uliong'ara wa Bani Hashim.

Kwa mara nyingine tunatoa mkono wa baraka na fanaka kwenu nyote wapendwa Waislamu kwa mnasaba huu wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Abul Fadhlil Abbas, mwana wa Imam Ali AS, aliyekuwa jemedari mkubwa katika jeshi la Imam Husani AS kwenye mapambano ya Karbala. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe taufiki ya kupamba maisha yetu kwa sira na mienendo iliyojaa baraka ya watu watukufu katika Uislamu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …