Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 19 Aprili 2015 21:05

Kwa mnasaba wa siku ya kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS

Kwa mnasaba wa siku ya kuzaliwa Imam Muhammad Baqir AS

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Wapenzi wasikilizaji, katika usiku kama wa leo anga kimya na tulivu ya mji wa Madina iliajabia nuru iliyoangaza kwenye nyumba ya Imam Sajjad (AS); nuru ambayo mwanga wake ulitandawaa kwenye anga yote hiyo ya mji huo. Ilikuwa ni nuru ya sura ya umaasumu, ing'arayo na kumeremeta ya mwana aliyebarikiwa, wa Ahlul Bayt wa Bwana Mtume Muhammad SAW na kuenea hadi mbinguni. Wapenzi wasikilizaji, tunakoa mkono wa pongezi, kheri na baraka kwa mnasaba wa kuzaliwa ua la tano lenye manukato, la bustani ya uongofu na maarifa, Imam Muhammad Baqir (AS) kwa wapenzi wote wa kizazi kitoharifu cha Mtume SAW. Karibuni kusikiliza kipindi hiki maalumu tulichokuandalieni kwa mnasaba huo.


*******


Jina lililobarikiwa la Imam wa tano ni Muhammad. Lakabu ya mtukufu huyo ni Baqir au Baqirul Ulum, kwa sababu alipasua vina vya bahari ya elimu na kubainisha siri za elimu na maarifa. Lakabu nyengine za Imam Muhammad Baqir (AS) ni Shaakir, yaani mshukurivu, Saabir, mvumilivu na Haadi, muongozaji kulekea uongofu, ambazo kila moja kati yao zinabainisha sifa za mtukufu huyo. Amma kwa upande wa wazazi, mama yake ni Fatima, binti wa Imam Hassan al Mujtaba (AS) na baba yake ni Imam Zainul Aabidiin, Ali Ibn Hussein (AS).
Jabir ibn Abdullah al Ansari, alikuwa mmoja wa masahaba watiifu wa Bwana Mtume SAW. Siku moja sahaba huyo alifunga safari ya kwenda kumwona Imam Baqir (AS). Hamu na shauku isiyoweza kuelezeka ilimjaa sahaba Jabir, na japokuwa mwili wake ulikuwa haujiwezi tena kwa uzee, huku nuru ya macho yake nayo pia ikiwa imefifia lakini uso wake ulikuwa ukimeremeta kwa furaha. Wakati alipomwona Imam Baqir alisema:" Naapa kwa Mola wa Al Kaaba kwamba hulka na silka hizi ninaziona kwako ni za Mtume wa Allah; namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa umri na kuweza kukutana na wewe, na kukufikishia salamu za Mtume wa Mwenyezi Mungu. Siku moja nilipokuwa pamoja na Mtume, alinambia:"Ewe Jabir wewe utabakia hai mpaka uje kuonana na mwana katika kizazi changu ambaye ni miongoni mwa watoto wa Hussein. Jina lake ni Muhammad; yeye ataipasua na kuipembua elimu ya dini; na kwa hivyo atapewa lakabu ya Baqir. Wakati utakapomwona mfikishie salamu zangu".
Wapenzi wasikilizaji, zama alizoishi Imam Muhammad Baqir (AS) zilikuwa zama za kustawi na kuenea elimu za Kiislamu, ambapo mafaqihi na maulama wakubwa wa elimu za fiqhi na hadithi waliishi katika zama hizo; lakini Imam Baqir (AS) alikuwa na hadhi na daraja maalumu mbele yao. Sheikh Mufid, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa mwishoni mwa karne ya nne na mwanzoni mwa karne ya tano Hijria ameandika kuwa:"Masahaba waliokuwa wamesalia, wakubwa katika mataabiina pamoja na mafaqihi wakubwa wakubwa wamepokea hukumu za masuala ya dini kutoka kwa mtukufu huyo. Imam alikuwa akisimulia habari za watu wa zama zilizopita pamoja na Mitume, na watu wakipokea kutoka kwake habari za sira na Sunna za Mtume SAW".
Kwa mujibu wa Sheikh Tusi, mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia aliyeishi katika karne ya tano hijria idadi ya wanafunzi hodari na mahiri wa mtukufu huyo ilifikia 466. Imam alikuwa marejeo ya maulama wote wa Hijaz katika masuala ya fiqhi. Umashuhuri wake ulienea katika ardhi ya Hijazi kiasi cha kujulikana kuwa ni Bwana wa Mafaqihi wa Hijazi.


*******


Kwa kujulikana kuwa mfasiri bora wa Qur'ani Tukufu, Imam Muhammad Baqir (AS) alikuwa akitoa tafsiri sahihi ya aya za kitabu hicho kitukufu na kuwashinda wapinzani na wale waliokuwa na inadi. Alikuwa kila mara akitumia aya za Qur'ani kuthibitisha hoja zake na kuyaweka maneno matukufu ya Mwenyezi Mungu shahidi wa aliyokuwa akiyanena. Alikuwa akiwaambia watu:"Niulizeni juu ya kila nikisemacho kimetokea wapi ndani ya Qur'ani ili nikusomeeni aya inayohusiana na nacho".
Kuwasaidia wahitaji na wanaodhulumiwa pamoja na wanyonge katika jamii lilikuwa moja ya mambo ya msingi katika maisha ya Imam Baqir (AS), na kukidhi mahitaji yao ya kimaada na kiroho ilikuwa moja ya shughuli muhimu zaidi za kijamii alizokuwa akifanya mtukufu huyo. Alikuwa akiwakusanya na kukaa karibu nao watu hao, akisikiliza dukuduku lao kisha akiwapoza na kuwaliwaza kwa machungu waliyokuwa nayo. Imam Jaafar Sadiq (AS) amesimulia kuhusu sifa na mwenendo huo wa Imam Baqir kwa kusema:"Siku moja nilikwenda kwa baba yangu, nikamkuta anagawa dinari elfu nane za dhahabu kwa wahitaji wa Madina na akawakomboa na kuwaachia huru watumwa kumi na moja". Katika siku za mapumziko hususan Ijumaa, Imam Baqir (AS) aliutumia muda wake kwa ajili ya utoaji sadaka na kuwasaidia wahitaji pamoja na kuwashajiisha watu wengine kufanya jema hilo. Katika hadithi nyengine, Imam Sadiq (AS) amesema:"Japokuwa baba yangu alikuwa na uwezo mdogo wa mali kulinganisha na watu wengine wa ukoo wake, na matumizi yake ya gharama za maisha yalikuwa makubwa zaidi kuliko wao lakini kila siku ya Ijumaa alikuwa akitoa misaada kwa wahitaji hata kama msaada wenyewe ni wa kiwango cha dinari moja, na alikuwa akisema:"Zawadi ya sadaka na msaada kwa wahitaji katika siku ya Ijumaa ina fadhila zaidi kama ambavyo siku ya Ijumaa ina fadhila na utukufu zaidi kulinganisha na siku nyenginezo." Katika kuzungumzia sifa na akhlaqi za baba yake, Imam Jaafar Sadiq (AS) anasimulia tena kwa kusema:"Baba yangu alikuwa muda wote katika hali ya kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Wakati wa kula chakula alikuwa akimtaja Mwenyezi Mungu. Wakati alipokuwa akizungumza na watu hakuacha pia kumdhukuru Mwenyezi Mungu na ulimi wake ulikuwa muda wote ukitamka kalima ya Laailah illa Allah."
Dini tukufu ya Uislamu wapenzi wasikilizaji inalipa umuhimu mkubwa suala la tabia na khulka njema na kuamiliana mtu kwa wema na bashaha na waumini wenzake. Na jambo hilo linachukuliwa na dini hiyo kuwa moja ya thamani aali za kiakhlaqi. Imam Baqir (AS) amelizungumzia jambo hilo kwa kusema:"Tabasamu la mtu kwa ndugu yake muumini ni jambo lenye kupendeza mno; na kuondoa ukungu wa majonzi katika uso wake ni tendo jema, na hajaabudiwa Mwenyezi Mungu kwa kitu bora zaidi kuliko kuufurahisha moyo wa muumini." Mtukufu huyo alikuwa akiwanukulia watu maneno ya babu yake mtukufu Mtume SAW aliposema:"Kila mwenye kumfurahisha muumini amenifurahisha mimi, na kila mwenye kunifurahisha mimi amemfurahisha Mwenyezi Mungu".
Muhammad bin Munkadir, ambaye alikuwa mmoja wa maulama wa Kisuni amenukuliwa na Imam Jaafar Sadiq (AS) akisema:"Mimi nilikuwa siamini kama Ali Ibn Hussein ameacha kumbukumbu ya mtoto mwenye fadhila na elimu kama yeye mwenyewe, mpaka nilipokuja kumwona mwanawe Muhammad Ibn Ali.... Wakati mmoja joto lilipokuwa kali mno niliamua kutoka nje na kuelekea kandokando ya Madina. Nilipokuwa njiani nikakutana na Muhammad Ibn Ali. Alikuwa mtu mkakamavu. Wakati huo alikuwa ameshughulika kulima shambani. Nikajisemea moyoni mwangu:"Mtu mkubwa katika wakubwa wa Kikureishi, katika hali ya joto kama hii, ameamua kutoka nje kwa sababu ya kutafuta mali za dunia; acha niende nikampe mawaidha." Nikiwa na nia hiyo nikamsogelea na kumwambia:"Mwenyezi Mungu akutengezee mambo yako; wewe mkubwa miongoni mwa wakubwa wa Kikureishi umetoka nyumbani kwako katika joto hili na katika hali kama hii kwa sababu ya kuhangaikia dunia; ikiwa mauti yatakufika katika hali kama hii utafanya nini? Mtukufu huyo alinielekea na kuniambia:"Naapa kwa Mwenyezi Mungu, endapo mauti yatanifika nikiwa katika hali hii nitaondoka duniani katika hali ya kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu; kwa sababu ninafanya kazi katika joto kali hili, ili nisiwanyooshee mkono watu. Naam, mimi nahofia hali moja tu, nayo ni kufikwa na mauti nikiwa katika hali ya kufanya mambo ya kumwasi Mwenyezi Mungu mtukufu." Muhammad bin Munkadir anasema:" hapo nilimuelekea mtukufu huyo na kumwambia:"Mwenyezi Mungu akurehemu; mimi nilitaka kukupa mawaidha wewe, lakini ni wewe ndiye uliyeniadhi mimi".
Wapenzi wasikilizaji kwa mara nyengine tunatoa mkono wa hongera, kheri na baraka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku iliyozaliwa nuru ya elimu na imani, Imam Muhammad Baqir (AS), kwa wafuasi wote wa kweli wa mtukufu huyo . Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …