Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 31 Mei 2016 20:41

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 35 na Sauti

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 35 na Sauti

Kama tulivyosema, mbali na Uwahabi unaotawala Saudia hakuna kundi lingine katika nchi za Kiislamu ambalo linawakufurisha Waislamu na kuwaua kigaidi. Ni genge hilo la Uwahabi baina ya Waislamu ndilo ambalo kwa kuwa na uelewa mbaya wa mafundisho ya Kiislamu na kutegemea dhahiri ya Qur'an Tukufu pamoja na suna za Mtume, na kwenda kinyume na misingi ya akili, falsafa na theolojia salama ikafikia kutenda vitendo hivyo vya kutisha.
Ndugu wasikilizaji ni vyema ifahamike kwamba, hakuna utambulisho rasmi unaobainisha misingi ya kufuata nyayo za Salaf Swaleh (watu wema wa zamani) miongoni mwa Masalafi. Ni kwa msingi huo ndio maana kukawepo matawi tofauti ya Usalafi ambayo hata hivyo kwa uhalisia wake ni makundi ya Uwahabi ambayo sanjari na kila moja kufuata misimamo yake, yanajinasibisha na harakati za Kisalafi. Kwa kuzingatia kuwa yana Imani ya Uwahabi ndio maana yakawakufurisha Waislamu wengine kwa sababu tu Waislamu hao hawakubaliani na imani ya genge hilo la Kiwahabi linalojinasibisha na Usalafi. Kwa kutumia mamilioni ya Dola zinazotokana na mafuta, Mawahabi wanaeneza tofauti na farqa baina ya Waislamu wa madhehebu ya Kiislamu duniani. Aidha Mawahabi sanjari na kuanzisha shule katika nchi masikini za Kiislamu na kuwavutia vijana kutoka nchi za Kiislamu kwenda kwenye shule hizo zinazotoa mafundisho ya Kiwahabi ndani na nje ya Saudia, walitakiwa pia kuwaonyesha Waislamu wa Shia au Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni hatari katika eneo la Mashariki ya Kati. Siasa hizo za Uwahabi za nchini Saudia zilikuwa zikidhamini malengo kadhaa ya madola ya Magharibi katika eneo hilo la Mashariki ya Kati hasa baada ya kufikiwa mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa. Hii ni kwa kuwa, kupitia propaganda za kuzibagua nchi za Waislamu sanjari na kuibua machafuko ndani ya nchi hizo, Wamagharibi walikuwa wakiimarisha soko lao la mauzo ya silaha katika eneo. Ni katika fremu hiyo ndipo ghafla eneo la Mashariki ya Kati likageuka na kuwa moja ya masoko makubwa kabisa ya mauzo ya silaha katika miongo kadhaa iliyopita. Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na katika eneo sanjari na kueneza propaganda za kuwaonyesha Waislamu wa Kishia au Iran kuwa tishio, walifanya njama pia za kujaribu kuitenga nchi hii, na kuonyesha katika fikra za walimwengu sura ghalati na isiyo halisi ya Uislamu unaolingania uadilifu unaosisitizwa na Mapinduzi ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla. Katika njia hiyo walijitahidi sana kuzuia kuenea ushawishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huku wakizuia pia kuenea ustawi wa mafundisho asili yaliyoletwa na Nabii Muhammad (saw). Katika hatua nyingine, kusambaratika kwa Urusi ya zamani na tawala za Kikomunisti za kambi ya Mashariki, kulisababisha mabadiliko makubwa katika mfumo wa kimataifa. Hivyo Marekani ilikuwa imepoteza adui na mpinzani wake mkuu. Ni mpinzani ambaye kwa muda mrefu Washington iliingia katika ulingo wa kueneza siasa zake kwa anwani ya tishio la Ukomonisti, huku ikiutaja kuwa hatari kwa walimwengu. Kuondoka kwa adui wa namna hiyo kuliifanya Marekani kubakiwa na ombwe kubwa katika siasa zake za kigeni, adui ambaye alikuwa akitumiwa kama wenzo wa kueneza siasa zake za kupenda kujitanua duniani hata baina ya waitifaki wake wa nchi za Ulaya. Baada ya hapo waitifaki wake wa Ulaya wakakosa maudhui ya uhalali wa kuundwa muungano wa kijeshi wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO ambalo ni mwamvuli wa usalama wa Marekani barani Ulaya. Ni hapo ndipo stratijia za Washington zikajikita tena katika kuibua tishio jipya kwa ajili ya kuhalalisha udharura wa kuwepo mrengo mmoja duniani kwa ajili ya kusimamia amani ya ulimwengu mrengo ambao ungekuwa chini ya Marekani.

******************************************

Ni katika wakati huo ndipo tishio la kijani likafanywa kuwa tishio jekundu ambapo sasa Uislamu uliarifishwa kuwa hatari, huku siasa za Marekani na waitifaki wake zikijikita katika kueneza chuki dhidi ya dini hii ya mbinguni, inayolingania amani na upendo. Pamoja na hayo, harakati hizo bado zilihitaji kuwepo sababu ya kuhalalisha kujitanua na kuingilia mataifa mengine kunakofanywa na Washingon ndani ya fikra za walio wengi. Kuutaja Uislamu kuwa ni dini ya ukatili na ugaidi, kulijiri katika fremu hiyo ambapo vyombo vya kipropaganda na kisiasa vilichukua nafasi ya kueneza uongo huo. Kila jambo ambalo lingeweza kusaidia kufikiwa malengo hayo ya Marekani na waitifaki wake, basi lilipewa umuhimu mkubwa katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi zikiwemo redio, televisheni na mitandao ya kijami. Wakati huo Uwahabi wa Saudia nao ulisaidia malengo hayo ya maadui wa Uislamu ambapo sanjari na kuonyesha sura ya Uislamu wa kufurutu mipaka na ulio kinyume na mafundisho asili ya dini hiyo, uliionyesha pia dini hiyo kuwa ya ukatili na mauaji kupitia vyombo hivyo vya Magharibi. Isisahulike kuwa, watawala wa Aal Saudi ndio waitifaki wakubwa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani na Ulaya katika eneo la Mashariki ya Kati. Hakuna shaka kuwa, Saudia ilidhihirisha Uislamu wa siasa kali na ukatili, ili kuwafanya walimwengu waweze kuichukia dini hii. Kama hiyo haitoshi, vyombo vya intelejensia vya Marekani, Uingereza, Saudia na Pakistan viliunda kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaaidah chini ya uongozi wa Osama Bin Laden huko nchini Afghanistan na Pakistan. Waafghanistan wa Kiarabu ambao walitumwa nchini humo kwa ajili ya kupambana na jeshi jekundu la Urusi ya zamani sasa wakakabidhiwa jukumu lao jipya kutoka kwa Marekani na Saudia. Ni watu ambao tayari walikuwa wamejazwa fikra za kufurutu ada na kufanya ukatili kupitia masomo waliyopewa katika shule za Kiwahabi nchini Pakistan. Baada ya wafuasi wa kundi la Taleban la Kiwahabi kudhibiti Afghanistan, nalo kundi la al-Qaaidah liliunda ngome nyingine kwa ajili ya kuendeleza malengo yake. 
Ndugu wasikilizaji mafundisho hayo ghalati na ya kufurutu ada ya wafuasi wa makundi hayo, yalitoa mwanya kwa Marekani kupitia kisingizio cha kukabiliana na ugaidi wa wanachama wa magenge hayo, kujipenyeza eneo la Mashariki ya Kati na wakati huo huo kukabiliana na Uislamu sahihi unaolingania uadilifu ulioenezwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ni kwa kuwa Uislamu huo ambao unafuatwa na wananchi wa taifa hili ambao ni mfano wa kuigwa katika eneo zima la Mashariki ya Kati na ulimwenguni kwa ujumla, ni tishio kubwa kwa tawala za kiukoo, kikabila na kidikteta zinazoungwa mkono na Marekani katika eneo. 

***************************************************
Ukweli ni kwamba, kundi la Taleban na al-Qaaidah ni zao la siasa za Marekani katika eneo kupitia malengo yake maovu. Weledi wengi wa mambo kwa kutegemea vielelezo vya namna makundi hayo ya al-Qaaidah na Taleban yalivyoanzishwa na kutumwa nchini Afghanistan, wametilia shaka tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Shaka hiyo inaongezeka zaidi hasa pale inapozingatiwa jinsi serikali ya Marekani ilivyotumia tukio hilo kwa ajili ya kuzishambulia kijeshi nchi za Afghanistan na Iraq na kufanya uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu na sheria za kimataifa kwa madai eti ya kupambana na ugaidi wa makundi yale yale ambayo yalianzishwa na Washington yenyewe. Nukta ya kuzingatiwa ni hii kwamba kati ya watekaji 19 wa ndege nne ambazo zilitumika kugonga minara ya kibiashara mjini New York na jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon mjini Washington, 15 kati yao walikuwa ni raia wa Saudi Arabia. Matukio hayo pamoja na mengine yanathibitisha wazi ukweli juu ya Saudia kutumikia siasa za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Hii ni kwa kuwa watawala wa Aal Saud wameambatanisha maisha yao na Marekani na tawala za Magharibi ili kwa njia hiyo waweze kudhaminiwa kuendelea kusalia madarakani nchini humo. Katika hatua nyingine na katika kupambana na Uislamu asili aliokuja nao Mtume Muhammad (saw), Aal Saud wanatekeleza pia siasa za uungaji mkono kwa tawala za kidikteta na kiukoo katika nchi za Waislamu na kadhalika kueneza makundi ya kitakfiri na Kiwahabi ndani ya nchi hizo. Ni kwa kutilia maanani siasa hizo, ndipo Saudia ikaanzisha makundi ya al-Qaaidah, Taleban, Daesh na Jab'hatu Nusra katika nchi za Afghanistan, Iraq na Syria na pia makundi ya kitakfiri katika nchi nyingine za Kiislamu na Kiafrika bila kusahau eneo la kusini mashariki mwa bara Asia. 
Ndugu wasikilizaji tulisema kuwa, baada ya kujiri Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Saudia ilijaribu kuunda muungano wa nchi za Kiarabu dhidi ya mapinduzi hayo. Uvamizi wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vya miaka minane na uungaji mkono mkubwa wa nchi za Kiarabu zikiongozwa na Riyadh kwa utawala dikteta Saddam Hussein katika uvamizi huo yote hayo yalifanyika katika mingi huo. Hata hivyo nchi hizo baadaye zilipata pigo kubwa kutokana na uungaji mkono huo kwa Saddam Huusein. Kwani muda punde baada ya vita hivyo Saddam alilazimika kurudi nyuma kutoka ardhi za Iran na kutambua mipaka ya kimataifa ya nchi hii ambayo awali alikataa kuitambua. Ili kufunika fedheha hiyo haraka Saddam Hussein akaivamia Kuwait ambayo awali ilikuwa moja ya waungaji mkono wake wakubwa. Hata hivyo pamoja na matukio yote hayo, lakini nchi hizo za Kiarabu zikiongozwa na Saudia bado hazijapata funzo wala ibra. Hii ni kusema kuwa, nchi hizo bado zinaendelea kusimama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zikisubiri kutoa pigo kwa nchi hii wakati wowote zitakapoweza. Katika mwenendo huo, Marekani na maadui wengine wa Iran ya Kiislamu wanaendeleza propaganda za kuchafua sura ya Iran kimataifa na kuituhumu nchi hii kuwa hatari kwa usalama wa Mashariki ya Kati. Chuki hiyo dhidi ya Iran imetekelezwa katika hatua kadhaa, zikiwemo za kijeshi, kisiasa na kiutamaduni. Ni hapo ndipo maghala ya kuhifadhia silaha ya nchi za Kiarabu hususan Saudia yakajaa silaha na zana za kijeshi kutoka Marekani na Ulaya. Katika upande wa kisiasa, Saudia na baadhi ya waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kimataifa wamekuwa wakitekeleza siasa hizo za Marekani na Magharibi kwa ajili ya kuitenga kisiasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, siasa ambazo zinaendelea hadi leo. 
Wapenzi wasikilizaji kipindi cha makala ya utakfiri sehemu ya 34 kinaishia hapa kwa leo, msikose kusikiliza sehemu ya 36 ya makala haya wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, kwaherini.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …