Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 10 Mei 2016 21:07

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 34 Na Sauti

Wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 34 Na Sauti

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika mfululizo wa vipindi hivi vinavyoangazia macho chimbuko la makundi yenye kuwakufurisha Waislamu wengine na kutekeleza jinai na mauaji ya kutisha dhidi yao hii leo ikiwa ni sehemu ya 34 ya vipindi hivyo.

Katika vipindi vilivyopita tuliashiria uharibifu wa kundi la Uwahabi dhidi ya maeneo muhimu ya Kiislamu kutokana na uelewa potofu wa mafundisho sahihi ya dini. Ndugu wasikilizaji kabla ya kuendelea na kipindi chetu cha leo ni vyema kuashiria nukta hii muhimu kwamba, licha wa Mawahabi kuharibu turathi za Kiislamu kama vile makaburi ya Mitume, wajukuu wa Mtume Muhammad (saw), masahaba, wake wa Nabii huyo wa Allah, maulama na watu wema, lakini kamwe wafuasi wa genge hilo hawaharibu vitu au maeneo ya kihistoria ya waasisi wa Uwahabi na daima huvilinda na kuvihifadhi vitu hivyo.

Katika kuendelea na kipindi hicho tulizungumzia nadharia ya Richard Nixon wa Marekani katika kuzifanya nchi mbili za Iran ya zamani na Saudia kutekeleza siasa zake katika eneo la Mashariki ya Kati. Hata hivyo kati ya nchi mbili hizo, Iran ilipewa nafasi ya mbele huku Saudia ikiwa katika nafasi ya pili. Kutokana na Saudia kuwa na idadi ndogo ya jamii ya watu, kusalia kwake nyuma katika sekta ya viwanda, kukosa kwake taasisi za kiutawala zenye uwezo, kadhalika kutokuwa na siasa zenye nguvu ni mambo ambayo yaliifanya nchi hiyo kukosa nafasi ya upolisi katika eneo licha ya utajiri wake mkubwa unaotokana na mafuta. Richard Nixon aliitaja sababu ya kuiweka Saudia katika daraja la pili katika siasa za mihimili miwili kama ninavyonukuu: "Kwa vyovyote iwavyo Saudia anaonekana kuwa muitifaki wetu asiyeaminika kwani watu wake wanaweza kubadilika wakati wowote na kurudi nyuma hasa kutokana na tawala za kufurutu mipaka za Kiarabu." Mwisho wa kunukuu. Hata hivyo haikufahamika ni tawala gani za kufurutu mipaka alizokuwa anazikusudia. Kwa kuzingatia ushindani na mivutano ya ndani iliyokuwepo baina ya tawala vibaraka za Kiarabu na Iran, siasa za uepo wa Saudia katika siasa za Nixon, kwa kiasi fulani hazikuwa kando na malengo ya Iran na pia maslahi ya madola ya Kiarabu ya Kusini mwa Ghuba ya Uajemi. Ni wakati huo ndipo Iran ambayo ilikuwa na nafasi ya kwanza, ikapewa upolisi wa eneo zima la Mashariki ya Kati. Katika mahojiano yake na gazeti moja la Uingereza tarehe 13 Septemba mwaka 1969 Miladia, Shah wa Iran alinukuliwa akisema kama ninavyonukuu: "Hakuna nguvu yeyote yenye ruhusa ya kupenya katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Iran inadhamini usalama wa meli kwa uhuru." Mwisho wa kunukuu. Sanjari na kuanza siasa mpya za eneo katika muongo wa 1970, Iran iliibuka na kuwa nchi yenye kuhitaji zana nyingi za kijeshi kati ya nchi zote za Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati kwa ujumla. Ni katika kutekeleza siasa na nadharia ya Nixon ndipo Marekani ikawa inaidhaminia Iran mahitaji hayo. Hakuna shaka kwamba, kufuata matakwa ya Washington, Marekani ilipewa kipaumbele katika siasa za kigeni za Iran latika kipindi cha kati ya mwaka 1970 hadi 1978. Mbali na silaha za Marekani Iran ya wakati huo ilikuwa pia mnunuzi mkubwa wa silaha kutoka Uingereza, Urusi ya zamani, Ujerumani na kadhalika utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

***************************************************

Nafasi iliyokuwanayo Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu, ilikuwa ni Zaidi ya ile iliyokuwanayo Saudia wakati huo. Hata hivyo Saudia nayo kupitia ajenda ya Nixon iliweza kutekeleza siasa zake katika eneo na katika nchi za Kiislamu pia. Pamoja na kuwepo baadhi ya juhudi za kukabiliana na fikra potofu za Uwahabi, lakini bado Mawahabi walijitahidi kueneza shule zao katika nchi masikini kama vile Pakistan ambapo katika shule hizo walitoa mafunzo ya taasubi, ukufurishaji na kwenda kinyume na mafundisho halisi ya Uislamu. Ndugu wasikilizaji, siasa za Marekani juu ya Iran zilibadilika na kufuata mkondo mpya baada tu ya kujiri mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa. Hii ni kwa kuwa, mapinduzi hayo, yalileta mtetemeko mkubwa katika siasa za eneo zima la Mashariki ya Kati, kama ambavyo pia zilitikisa tawala za kidikteta katika eneo hili. Kwa hakika mapinduzi ya Kiislamu yalifufua Uislamu asili wa Mtume Muhammad (saw) na kutupilia mbali Uislamu uliopitwa na wakati wa Kiwahabi ambao ni wa taasubi na ukufurishaji na ambao bendera yake imeshikiliwa na Saudi Arabia. Kwa kuzingatia muundo wa kiukoo wa utawala na nafasi ya mfumodume ambao unafuatwa na viongozi wa Saudia kupitia ajenda za Marekani katika nchi za Kiislamu, utawala huo ulijikuta ukikabiliwa na tishio la mapinduzi ya Kiislamu kama yale ya nchini Iran. Ni kwa ajili hiyo ndio maana baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini hapa, Aal-Saud wakafanya njama na hila kubwa katika kuhamasisha na kuzishajiisha nchi za Kiarabu kuunda kambi mpya dhidi ya Iran ya Kiislamu. Njama hizo zilibainika wazi baada ya uvamizi wa utawala wa Ba’athi nchini Iraq chini ya Saddam Hussein dhidi ya taifa hili. Kwa kipindi chote cha miaka minane ya vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran, ununuzi wote wa silaha uliofanywa na Saddam ulitokana na fedha za Saudia na watawala wengine madikteta wa Kiarabu. Mwishoni mwa vita hivyo utawala wa Ba’athi ulijizatiti zaidi kwa silaha na zana za kijeshi yakiwemo magari ya deraya na vifaru na hata idadi ya askari wake, kupita kiwango ambacho utawala huo ulijizatiti kabla ya kuivamia nchi hii. Kuhusu suala hilo Iraq, ilipata msaada wa fedha kutoka Saudia na Kuwait na baadhi ya nchi nyingine za Kiarabu, huku kwa upande mwingine kambi mbili za Mashariki na Magharibi nazo zikishiriki katika kuupatia utawala huo wa Saddam misaada ya namna hiyo. Aidha katika kuendeleza uadui wa Saudia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, watawala wa Aal-Saud kama ilivyo ada yao hii leo, walipunguza bei ya mafuta ili kutoa pigo kwa Iran ya Kiislamu. Aidha watawala hao waliimarisha zaidi uhusiano wao na Saddam kama alivyosema mfalme wa Saudia wa wakati huo, Khalid bin Abdulaziz Al Saud kupitia mazungumzo yake ya simu na Saddam hapo tarehe 25 Septemba mwaka 1980. Kufuatia hali hiyo, Saudia ikahesabiwa kuwa muungaji mkono mkubwa wa dikteta Saddam Hussein. Hadi kumalizika vita vya miaka minane dhidi ya Iran, Saudia ilikuwa imempatia Saddam Hussein zaidi ya dola bilioni 30 za Marekani. Ni kufuatia hali hiyo ndipo Saddam Hussein akadhani kwamba, baada ya vita hivyo, nchi yake ingeibuka na kuwa moja ya nchi kubwa zenye nguvu katika eneo na kuchukua upolisi dhidi ya nchi zingine. Katika fremu hiyo na kwa kuamini kuwa sasa hakukuwepo na nchi ya Kiarabu ambayo ingeweza kukabiliana na Iraq, akaishambulia Kuwait, moja ya nchi ambazo awali zilishiriki kumsaidia kifedha. Kwa hakika hujuma hiyo ya Saddam dhidi ya Kuwait ndiyo iliandaa mazingira ya kuondolewa kwake madarakani miaka kadhaa baadaye. Wakati hayo yakijiri, hali ya tahayuri iliyolikumba eneo zima la Mashariki ya kati na duniani kwa ujumla hasa baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, iliifanya Saudia kupatwa na mshtuko na hivyo kuanzisha njama za kuchukua nafasi ya mrengo wa kukabiliana na Uislamu asili wa kupigania uadilifu na uhuru ambao chanzo chake ni Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Ni katika hali hiyo ndipo Riyadh ikajikita tu katika kuenea fikra potofu za Uwahabi katika nchi za Kiislamu na hata ndani ya jamii za Waislamu katika nchi za Magharibi. Ni hatua hizo ndizo zilizoandaa mazingira ya kuibuka kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Qaidah, Taleban na kisha Daesh na makundi mengine ya kitakfiri na kigaidi yanayotenda jinai kila uchao dhidi ya binaadamu katika nchi tofauti za dunia.

************************************************

Matamshi ya mmoja wa maseneta wa Marekani mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2016 mbele ya baraza la mahusiano ya kigeni ya nchi hiyo kuhusiana na suala hilo yanabainisha ukweli huo. Chris Murphy, mmoja wa wajumbe wa chama cha Democrats katika kongresi ya Marekani kutoka jimbo la Connecticut alisema kama ninavyonukuu: "Katika shule za kidini nchini Pakistan, wanafunzi wanafundishwa maudhui za vitabu vya kufurutu ada. Ni maudhui ambazo zimejengeka juu ya misingi ya itikadi za Uwahabi." Murphy anaendelea kusema: "Wanafunzi kwenye shule hizo wanaambiwa kuwa kamwe vita vya msalaba haviishi na shule na mashirika ya misaada na idara za serikali zinatakiwa kujiandaa kwa vita vya Wamagharibi dhidi ya Uislamu... Mafundisho hayo ndiyo hutolewa katika maeneo tofauti ya dunia kwenye shule za Kiwahabi. Ni ambayo yalianzia nchini Pakistan hadi Kosovo. Nigeria hadi Indonesia nk." Mwisho wa kunukuu. Aidha anasema tena: "Mafundisho hayo ambayo yako mbali sana na uhalisia wa dini ya Uislamu yanajazwa katika akili za mamia ya mamilioni ya vijana. Mwaka 1956 kulikuwepo karibu shule 244 za kidini nchini Pakistan. Na sasa shule hizo zimeongezeka na kufikia elfu 24. Shule hizo zimeenea kote duniani. Msinifahamu vibaya. Kwani katika shule hizo si tu kwamba kunafundishwa ukatili na utumiaji mabavu wa kufurutu ada, bali kunafundishwa Uislamu ambao kirahisi unawalenga kuwabagua Waislamu wa Kishia na hata Wamagharibi. Mawahabi wanaeneza upototofu wao ndani ya Uislamu, ambapo hatimaye huwaita watu wengine kuwa ni makafiri wakiwamo Mayahudi au Wakristo na hata Waislamu wa Kishia, Masufi na kadhalika Masuni." Mwisho wa kunukuu. Ndugu msikilizaji maneno hayo sio maneno ya msomi wa Kishia nchini Iran, bali ni maneno ya mmoja wa viongozi wa kisiasa nchini Marekani.

*****************************************

Ndugu wasikilizaji kama tulivyosema, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa tishio kubwa kwa Uwahabi wa Saudia. Hii ni kusema kuwa baada ya Mapinduzi hayo ya Kiislamu, Saudia ilijikita tu katika kueneza ndani ya nchi za Kiislamu na jamii za Kiislamu huko Magharibi, Uwahabi wa kufurutu ada, mafundisho potofu ya Kiislamu na pia kuwakufurisha Waislamu wengine hususan Mashia. Hali ikiwa hivyo kwa Saudia, maadui wa Uislamu huko Magharibi mbali na kutumia nyenzo za kiuchumi, kisiasa na kijeshi katika kujaribu kuondoa mfumo wa Kiislamu nchini Iran, walitumia pia silaha ya kimadhehebu dhidi ya dhehebu lingine katika Uislamu. Katika fremu hiyo na ili kuzuia kuenea mafundisho sahihi ya Uislamu sanjari na kupotosha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran viongozi wa Marekani walijaribu kuchafua sura ya mapinduzi hayo katika jamii za Waislamu katika nchi vibaraka za Kiarabu. Katika hali hiyo hakukuwepo na harakati nyingine ghairi ya Uwahabi ambayo ingeweza kutekeleza ajenda hiyo ya Marekani. Hii ni kwa sababu, mbali na kundi hilo la Uwahabi wa Saudia, hapakuwepo kundi au dhehebu lingine ambalo lilikuwa linawakufurisha Waislamu na kuhalalisha damu zao. Ni kundi hilo pekee la Uwahabi ndilo linaloamini tu dhahiri ya Qur'an na suna za Mtume Muhammad (saw) sanjari na kwenda kinyume pia na akili salama na elimu ya falsafa na theolojia.

Wapenzi wasikilizaji kipindi cha makala ya utakfiri sehemu ya 34 kinakomea hapa kwa leo, msikose kusikiliza sehemu ya 35 ya makala haya wiki ijayo. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, kwaherini.

 

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …