Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 28 Aprili 2016 14:32

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (33) na sauti

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (33) na sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuungana nami tena katika sehemu ya 33 ya makala ya chimbuko la utakfiri yanayozungumzia chanzo cha kuibuka makundi yanayowakufurisha Waislamu na kutenda jinai za kutisha dhidi yao. Katika kipindi kilichopita tulizungumzia uharibifu wa kutisha wa Mawahabi dhidi ya maeneo muhimu ya kihistoria, jinai iliyofanywa kwa kutegemea uelewa potofu wa aya za mutashabihaat na riwaya dhaifu. Aidha Mawahabi kwa kutegemea hadithi moja ya kubuniwa, walikutambua kujengea juu ya kaburi kuwa eti ni sawa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu, jambo ambalo halina ukweli wowote. Ni hadithi hiyo ndiyo iliyomfanya Taqiyyud-Din Ahmad Ibn Taymiyyah au mwanafunzi wake Ibn Qayyim al-Jawziyya au Muhammad ash-Shawkani katika kitabu chake cha Naylul-Awtwaar kuandika kuwa, kujengea kaburi ni sawa na kujenga sanamu la 'Lata na Uzza' jambo linalosababisha mtu kuwa kafiri. Kwa upande wa wapokezi wa riwaya hiyo inayotumiwa na watu wa kundi hilo la Kiwahabi ni dhaifu kutokana na kwamba wapokezi wake ni watu maarufu katika kubuni hadithi bandia katika Uislamu. Na suala la pili ni kwamba, madhumuni yake riwaya hiyo hayana msingi wowote na hivyo haithibitishi hata kidogo madai ya Mawahabi katika kuharamisha kujengea na kuzuru makaburi. Hii ni kwa kuwa, kwa mtazamo wao, kujengea kaburi ni suala haramu na kwamba kuharibu na kubomoa jengo kama hilo ni jambo la wajibu. Hata hivyo kama tulivyosema, riwaya hiyo haihusiani na madai hayo. Ibn Taymiyyah na wafuasi wake wanaamini kuwa, imani ya kubomoa jengo lililojengwa juu ya kaburi ni katika mambo ambayo yanatakiwa kutetewa. Ni katika fremu hiyo, ndipo watu hao wakaamini kuwa, kitendo cha Waislamu wa Kishia kujengea makaburi ya Mitume wa Mwenyezi Mungu, Maimamu, masahaba, watu wema na maulama wakubwa wa Kiislamu na kwenda kwenye maeneo hayo na kuyabusu au kuyaenzi kwa kukumbuka historia ya watu hao waliozikwa mahala hapo, ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu, bali pia ni dhambi kubwa zaidi ya kuabudu sanamu. Katika kujibu tuhuma hiyo kubwa dhidi ya Mashia tunaweza kwanza kusema kuwa, dini tukufu ya Kiislamu imesisitizia umuhimu wa kuheshimiwa mwanadamu hata baada ya kufariki kwake dunia. Kama ambavyo sheria inaamuru kwamba, mwili wa Mwislamu kwanza unatakiwa kuoshwa, kupakwa mafuta, kuvikwa sanda, kuswaliwa, kusindikizwa na hatimaye kuzikwa kaburini. Mbali na sheria, hata akili nayo inahimiza juu ya suala la kuyaheshimu makaburi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu na maeneo walikozikwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw) kutokana na nafasi yao adhimu mbele ya Allah.

***************************************************

Kwa msingi huo, ikiwa Mawahabi watathibitisha kwamba, Mashia wanayaabudu maeneo hayo badala ya Mwenyezi Mungu, kwa hakika kitendo hicho kitahesabika kuwa ni shirki ambayo Waislamu wote wanatakiwa kukabiliana nayo. Hata hivyo, tuhuma hizo hazina msingi wowote na kile kinachoonekana katika matamshi ya Mawahabi dhidi ya Mashia ni kuenenza chuki na propaganda za uongo zilizoibuliwa na Ibn Taymiyyah, Ibn Qayyim na masheikh wengine wa Kiwahabi. Na ikiwa makelele ya Mawahabi hao yanakusudia kuwa, kujengea makaburi na kuweka quba juu yake kunasababisha kuheshimiwa na kuwaenzi watu waliozikwa ndani yake, kwa hakika suala hilo si tu kwamba ni jambo jema na lenye umuhimu mkubwa, bali linatakiwa kuenziwa na kila Mwislamu. Hii ni kwa kuwa, kuyatukuza na kuyafanyia taadhima makaburi ya Mitume wa Allah, maimamu na mawalii wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa matukufu ya kidini ambayo Mwenyezi Mungu amesema ndani ya Qur’ani juu yake kama ninavyonukuu: “Hivyo ndivyo! Na anayeziheshimu alama za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyonyo.” Suratul-Hajj aya 32. Kwa ajili hiyo tunaweza kuwauliza Mawahabi kwamba, inakuwaje muwatuhumu Mashia kwa shirki kutokana tu na wao kuwaenzi Mitume wa Mwenyezi Mungu, Maimamu na mawalii, jambo ambalo kwa hakika linamfurahisha yeye Mwenyezi Mungu? Aidha ikiwa kujengea makaburi na kadhalika kujengea juu yake quba ni haramu na bidaa, ni kwa nini basi Waislamu wa mwanzo kabla ya ujio wa Mawahabi, walikuwa wakiyajengea makaburi hayo ya maulama na watu wao wakubwa? Je, kaburi la Imam Maliki Bin Anas halikuwepo Baqii likiwa limejengewa? Je, kaburi la Imam Shafi haliko nchini Misri likiwa pia limejengewa? Ama je, kaburi la Imam Hanafi halipo mjini Baghdad, Iraq katika hali ya kujengewa?


**********************************************

Ndugu wasikilizaji kama mtakuwa mnakumbuka katika vipindi vilivyopita tulisema kuwa Usalafi umegawanyika katika makundi tofauti, huku kila kundi likiwa na mielekeo inayotofautiana na ya lingine. Sehemu moja ya Usalafi ni makundi ya kitakfiri na kigaidi ambayo yanapinga Waislamu wengine wote na kuwaita kuwa ni makafiri ambao ni halali kuwaua. Ni vyema mkafahamu kwamba, kabla ya kuundwa genge linalofahamika kwa jina la Uwahabi katika ardhi za Hijazi, yaani Saudia ya leo, Masalafi wa wakati huo hawakuwa na imani ya kuwakufurisha Waislamu wengine na kuhalalisha kumwagwa damu zao. Na hata Ibn Taymiyyah ambaye anatajwa kuwa mwasisi wa fikra potofu za Uwahabi pindi alipokuja na mitazamo yake ghalati inayoenda kinyume na mafundisho asili ya Uislamu, na kuwataja Waislamu wengine kuwa makafiri, aliwekwa jela na kufariki dunia baadaye akiwa kifungoni na hivyo kuzima moto wa fitina katika ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo, fikra za Ibn Taymiyyah zilihuishwa tena na Muhammad Ibn Abdul-Wahhabi ambaye kwa mara nyingine tena alifanikiwa kuingiza katika Uislamu mafundisho potofu kama inavyoshuhudiwa leo. Kwa hakika jambo hilo halingekuwa rahisi kufikiwa, lau kama si njama na misaada ya Uingereza ambayo kwa kuangalia maslahi yake ya baadaye iliamua kuwunganisha pamoja, Muhammad Ibn Abdul-Wahhab na Aal-Saud na hivyo kukawa kumezaliwa jinamizi hatari katika ulimwengu wa Kiislamu. Ni baada ya hapo ndipo Mawahabi wakaanzisha mauaji na jinai za kutisha katika maeneo ya Bara Arabu sanjari na kuharibu kikamilifu athari za dini ya Kiislamu. Katika jinai hizo, Waislamu walitakiwa ima wakubali fikra potofu za Uwahabi au wakubali kuuawa kwa umati wao na familia zao. Haukupita muda mrefu mara Aal-Saud kwa kushirikiana na Mawahabi wakayabadili maeneo ya Hijazi kwa jina lao na ghafla kukazaliwa nchi inayoitwa Saudia ambayo kwa hakika hii leo imegeuka na kuwa muungaji mkono mkubwa wa makafiri duniani huku ikijishughulisha tu na kuibua fitina katika Ulimwengu wa Kiislamu. Hata hivyo uovu wa watawala wa Aal-Saudi haukukomea hapo, bali waliendelea kupenyeza zaidi ushawishi wao hata katika nchi nyingine za Kiislamu kwa lengo la kuibua vita, chuki na kuchafua amani ya nchi hizo. Katika sehemu nyingine, kugunduliwa mafuta huko Saudi Arabia na kadhalika uepo wa Uingereza na Marekani ndani ya nchi hiyo kwa ajili ya kuchimba nishati hiyo muhimu, kuliiongezea Saudia itibari kwa madola ya Magharibi. Ni baada ya hapo ndipo Riyadh ikaungana kistratijia na madola hayo ya Magharibi yakiongozwa na Marekani. Kwa utaratibu huo, Saudia ambayo ilikuwa ikipenyeza katika nchi nyingine za Kiislamu, iligeuka na kuwa mtekelezaji mkubwa wa siasa za madola ya Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati. Mabilioni ya dola ambayo nchi hiyo imekuwa ikiyapata kutokana na uchimbaji mafuta, hununulia silaha na zana mbalimbali za kijeshi na hivyo kustawisha viwanda vya utengenezaji silaha vya Marekani na Ulaya. Mbali na hayo, utawala wa Saudia hii leo ni mdhamini mkubwa wa mahitaji ya mafuta kwa serikali za Magharibi. Kwa maelezo mengine ni kwamba, silaha ambazo Saudia imekuwa ikizinunua kutoka kwa madola hayo ya Kimagharibi zikiongozwa na Marekani, ndizo zinazotumika katika kufanikisha siasa za madola hayo ndani ya eneo la Mashariki ya Kati hii leo.


*******************************************


Kudhidhiri na kusambaratika kwa nafasi ya nchi tofauti kieneo na kimataifa kunategemea sababu kuu mbili za ndani na nje. Nadharia ya Nixon Doctrine katika muongo wa 70 Miladia kuhusiana na eneo la Ghuba ya Uajemi inaakisi mihimili miwili ya kisiasa, au siasa za pande mbili. Kwa mujibu wa nadharia hizo serikali za Iran na Saudia zilitakiwa kuwa mihimili miwili muhimu kwa ajili ya kutekeleza siasa za Washington katika eneo hili kukiwemo kulinda na kusimamia shughuli ya kuzuia nchi nyingine za Ghuba ya Uajemi kuwa zenye nguvu. Marekani kwa kuzipatia misaada mingi ya kiuchumi na kijeshi nchi hizo mbili, ilikuwa ikiziandaa kuwa wenzo na wasila wa kudhamini usalama wake katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati kwa ujumla bila ya Marekani yenyewe kuwa katika eneo hili. Tunapozungumzia Iran, tunakusudia Iran ya wakati wa utawala wa Shah na ambayo ilikuwa kibaraka wa Marekani na madola ya Magharibi. Rais huyo wa zamani wa Marekani, alikuwa akiamini kuwa, kustawi kiuchumi na kupatikana marekebisho katika nchi za eneo la Ghuba ya Uajemi, ni miongoni mwa masuala muhimu yanayoweza kusaidia kupatikana usalama na amani katika eneo hili, hivyo Saudia na Iran ndizo zingeweza kufanikisha suala hilo nyeti kwake.

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala yanayoangazia macho wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 33, kinakomea hapa kwa leo. Tutakutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Allah. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati huo ninakuageni kwa kusema, kwaherini.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …