Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Aprili 2016 21:45

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (32) na sauti

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (32) na sauti

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuungana nami tena katika sehemu ya 32 ya makala ya chimbuko la utakfiri yanayozungumzia chanzo cha makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine na kutenda jinai za kutisha dhidi yao.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia jinai na mauaji ya Mawahabi na njama za viongozi wa Kiwahabi katika kuvamia maeneo ya Waislamu na kudhabiti. Ndugu wasikilizaji hadi kufikia utawala, Abdul-Aziz Bin Saud, akiongozana na jeshi kubwa, aliua Waislamu zaidi ya laki nne.  Kwa mujibu wa historia, watu 4000 walikatwa shingo zao, ambapo pia jeshi lake liliwakata miguu watu wengine laki tatu na elfu 50, kwa kosa la kupinga kundi hilo potofu.  Miongoni mwa jinai nyingine zilizofanywa na Aal Saud na Mawahabi, ilikuwa ni kuharibu athari za Kiislamu na maeneo muhimu ya dini ya Uislamu. Kwa hakika viongozi hao wa Kiwahabi wana faili jeusi katika kuharibu maeneo matukufu ya Kiislamu ambayo Waislamu wa awali walikuwa wakiyazuru na kupata kumbukumbu ya Uislamu wa mwanzo. Awali kati ya miaka 1216 hadi 1222 Hijiria, Saud Bin Abdul Aziz, alifanya uharibifu mkubwa wa maeneo ya Kiislamu kwa kiasi cha kutisha. Katika kipindi chake, jeshi la Kiwahabi lilifanya hujuma mjini Karbala, Iraq na kubomoa kaburi la Imam Hussein (as), mjukuu wa Bwana Mtume Muhammad (saw), sanjari na kuwaua kwa halaiki Waislamu wa Kishia wa mji huo. Ahmad Zaini Dahlan mwandishi wa historia, anaandika katika kitabu chake cha 'Khulaswatul-Kalaam Fii Bayaan Umaraau Bilaadil-Haraam' juu ya uharibifu wa kutisha wa Mawahabi dhidi ya maeneo matakatifu ya Kiislamu kwamba: "Ilikuwa kabla ya mapambazuko ambapo Mawahabi na watu walioandamananao walianza kuharibu misikiti na athari za watu wema. Kwanza walianza kubomoa makaburi ya Baqii watu watakatifu na kisha wakaelekea eneo alikozaliwa Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kubomoa quba lililokuwa limejengwa juu yake. Baada ya hayo, Mawahabi hao waliendelea kubomoa na kuharibu kila athari inayohusiana na watu wema wa zamani. Wakati wa kubomoa makaburi hayo, walikuwa wakipiga ngoma na kuimba nyimbo za kejeli na hivyo wakawa wameyavunjia heshima makaburi ya waumini wa Kiislamu." Mwisho wa kunukuu. Ndugu wasikilizaji ni vyema mkafahamu kwamba, eneo la Baqii ni mahala walipozikwa watu watukufu kuanzia masahaba na watu wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw) wakiwamo pia wake wa Nabii huyo wa Allah. Aidha eneo hilo lilikuwa likitembelewa na Waislamu kwa kipindi chote cha historia. Uharibifu huo wa wafuasi wa genge hilo ulitekelezwa kupitia fatwa bandia zilizotolewa na viongozi wa Kiwahabi kama inavyoshuhudiwa pia hii leo.

************************************************************

Si vibaya kuashiria hapa kwamba, kila kaumu au dini huipa umuhimu maalumu athari yake ya kihistoria, hususan kama athari hiyo itahusiana na watu wa mwanzo wa kaumu au dini fulani. Tangu mwanzoni mwa kudhihiri Uisamu, wafuasi wa dini hiyo walijengea makaburi mengi ya Waislamu wa mwanzo ambapo pia katika kuwaenzi, walikuwa wakiyatembelea na kupata Baraka kutoka kwayo. Katika kadhia hiyo hakukutokea alim wala mtu yeyote aliyelitaja suala hilo kuwa ni haramu ambapo pia hata maulama wote wa Kiislamu wamekubaliana kuwa ni halali kujengea na kuyazuru makaburi hayo ya watu wema. Waandishi wakubwa wa historia kama vile Mas'udi katika kitabu chake cha Muruujudh-Dhahab na aliyekuwa akiishi katika kipindi cha karne ya nne Hijiria na kadhalika Ibn Jubair na Ibn Batwutwah ambao wote waliishi kipindi cha karne ya saba na ya nane Hijiria, wote kwa pamoja wameelezea kuwepo makaburi hayo yaliyojengewa katika enzi hizo. Ibn Jubair ambaye pia katika kipindi cha karne ya saba alitembelea eneo la Hijazi na kufika eneo la Baqii anaandika kwa kusema kama ninavyomnukuu: "Na kuba lililoinuka kuelekea juu lilikuwa karibu na Baqii." Mwisho wa kunukuu. Katika karne ya nane Hijiria ikiwa ni baada ya kupita miaka 150 ya safari ya Ibn Jubair huko Hijaz, Ibn Batwutwah alifanya safari mjini Madina na kuandika yale aliyojionea kwa macho yake katika mji huo mtukufu kama ninavyomnukuu: "Haram ya Maimamu katika makaburi ya Baqii imewekewa juu yake quba lililoelekea juu. Quba hiyo ni imara na yenye kuvutia sana." Mwisho wa kunukuu. Baada ya kipindi hicho Ibrahim Rifat Pasha mwandishi wa historia wa kitabu cha 'Mir'atul-Haramain' aliyetembelea haram ya Maimamu wa Baqii katika safari yake ya hija ikiwa ni miaka 19 kabla ya kuharibiwa na Mawahabi aliandika kwa lisema: "Na kaburi la Abbas na Imam Hassan Ibn Ali Bin Abi Twalib na maimamu wengine watatu yalikuwa chini ya quba ambalo lilikuwa kubwa zaidi ya maquba mengine yaliyokuwa eneo la Baqii." Mwisho wa kunukuu. Itakumbukwa kuwa, eneo la Baqii lilifanyiwa marekebisho mara tatu kwa kipindi chake cha historia. Kwa mara ya kwanza, mwaka 519 Hijiria lilijengwa na mtawala aliyefahamika kwa jina la Al-Mustansir Billah, huku likijengwa tena kwa mara nyingine mwishoni mwa karne ya 13 na mfalme Mahmud Ghaznawi. Hayo ni kwa mujibu wa vitabu vya historia kuhusiana na eneo la Baqii, mjini Madina.

********************************************

Hali ikiwa hivyo, kadhalika makaburi hayo ya Baqii yamefanyiwa uharibifu mara mbili. Mara ya kwanza yaliharibiwa na jeshi lililoongozwa na Abdul-Aziz Bin Saud hapo mwaka 1221 Hijiria baada ya askari wa mtawala huyo wa Kiwahabi kuuzingira mji wa Madina kwa kipindi kirefu. Katika mzingiro huo askari hao walifanya mauaji dhidi ya watu wengi wasio na hatia wa mji huo mtukufu wa Mtume (saw). Baada ya hapo Mawahabi waliwakusanya sehemu moja wahudumu wa mji huo wa Madina ambapo badala ya kuwapatia zawadi kutokana na kazi njema wanayoifanya, walianza kuwapiga na kuwanyanyansa kwa aina mbalimbali ya adhabu sanjari na kuwadhalilisha. Mwishoni mwa hujuma hiyo dhidi ya haramu ya Mtume (saw), wakati wavamizi hao walipokuwa wakielekea mjini Najdi yalipokuwa makao makuu ya Uwahabi, walienda eneo la Baqii huku Abdul-Aziz akitoa amri ya kubomolewa kabisa makaburi yote ya eneo hilo. Kwa mujibu wa waandishi wa historia, Mawahabi walitoka mjini Madina wakiwa na masanduku manne yaliyojaa vito vilivyochovwa kwa alimasi, yaquti za bei ghali na karibu panga 100 zenye ala zilizochovwa kwa dhahabu asilia na kupambwa na madini ya alimasi na yaquti. Ni kufuatia hali hiyo ndipo kiongozi mkuu wa utawala wa Othmania akampa amri mtawala Muhammad Ali aliyekuwa mfalme wa utawala huo akimtaka aliokoe haraka eneo la Hijaz na kulidhibiti kikamilifu. Kufuatia amri hiyo, ndipo kukajiri vita vikali mwaka 1227 Hijiria ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vibaya Mawahabi. Ni baada ya tukio hilo na kwa mali za Waislamu yakajengwa upya makaburi yaliyoharibiwa ya eneo la Baqii, sanjari na kujengwa quba kubwa ambalo lilileta mandhari ya kuvutia katika eneo hilo ambapo liligeuka na kuwa kitovu cha wafanya ziara wa Kiislamu duniani. Hata hivyo Mawahabi si tu kwamba, hawakuacha kuwa tishio dhidi ya makaburi hayo ya wajukuu wa Mtume (saw) na masahaba wake, bali waliendeleza njama zao chafu katika kuboa na kuharibu maeneo hayo kupitia fatwa zao bandia. Katika fremu hiyo mwaka 1343 Hijiria, Mawahabi walibomoa na kuharibu makaburi ya Abdul-Mutwalib (as), babu yake Mtume, Abi Twalib (as), ami yake Mtume, Bibi Khadija (as) mke wa kwanza wa Mtume na pia mahala alipozaliwa Nabii huyo wa Allah (saw). Aidha wafuasi wa genge hilo potofu waliharibu pia eneo alipozaliwa Bibi Fatwimat Zahraa (as) binti ya Mtume na eneo la faragha alilokuwa akilitumia Mtume (saw) katika kufanya ibada hapo mjini Makkah. Mwaka 1928 Miladia, Mawahabi waliharibu pia kaburi la Bi. Hawwah, mke wa Nabi Adam (as) mjini Jeddah na ilipofika mwaka 1975 wakafunika kabisa kwa zege kaburi hilo ili kuzuia watu wasiweze kuzuru eneo hilo, kama walivyoharibu pia makaburi ya watukufu wengine mjini hapo. Bomoabomoa ya Mawahabi haikuishia hapo, bali iliendelea ambapo waliazimia kubomoa kaburi la Mtukufu Mtume (saw), lakini kutokana kukhofia hasira za Waislamu, wakashindwa kufanya unyama huo. Mwezi Shawwal mwaka 1343 Hijiria, wafuasi wa kundi hilo kibaraka wa mkoloni Mwingereza waliharibu makaburi ya Hamza (as), mashahidi wa vita vya Uhudi, kaburi la Abdullah na Bi. Amina baba na mama yake Mtume (saw) na makaburi ya watu wengine wema na kuyasawazisha kabisa na udongo, huku wakipora vitu vya thamani vilivyokuwa juu ya makaburi hayo. Ni katika mwaka huo huo, ndipo wakavamia pia mji wa Karbala, Iraq na kutekeleza jinai kubwa za kutisha ikiwemo kupora vitu vya thamani kwenye kaburi la Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume na kuua karibu watu 7000 wakiwamo maulama na masharifu wa mji hapo.

****************************************

Kwa miaka kadhaa sasa, na kwa kufuata mienendo potofu ya Mawahabi waliopita, hii leo pia makundi ya kitakfiri na kigaidi nchini Syria, Iraq, Libya, Tunisia na nchi nyingine za Kiislamu, yanabomoa na kuharibu makaburi ya watu watukufu wakiwamo, masahaba, wajukuu wa Nabii wa Allah na kadhalika mawalii wa Mwenyezi Mungu. Wafuasi wa kundi hilo, kwa kutegemea aya za mutashaabihat na kwa uelewa ghalati wa baadhi ya riwaya, wanaamini kuwa kujengea kaburi ni shirki na bidaa na kwa msingi huo ndio wakaamua kuharibu bila ya utu mioyoni mwao makaburi ya mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala yanayoangazia macho wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 32, kinakomea hapa kwa leo. Tutakutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Allah. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati huo ninakuageni kwa kusema, kwaherini.

 

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …