Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 15 Aprili 2016 16:19

Hadithi ya Uongofu (38)

Hadithi ya Uongofu (38)

Assalaamu alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika kipindi chetu kilichopita, tulizungumzia maudhui ya haya au soni na kueleza jinsi sifa hii ilivyo na taathira kubwa katika masuala mbalimbali maishani. Tulisema katika kipindi chetu cha juma lililopita kwamba, kama taathira ya haya au aibu isingekuwepo basi mgeni asingeheshimiwa na wala utekelezaji wa ahadi usingezingatiwa. Kama kuona soni au haya kusingekuweko, basi watu wasingekuwa wanawasidia wenzao na kutekeleza haja zao, kusingekuwa na msukumo wa kufanya mambo mazuri na watu wasingekuwa wanajitenga mbali na mambo mabaya. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 38 ya mfululizo huu kitazungumzia misdaqi na mifano ya kuona haya na soni na kukunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache kutegea sikio kile nilichokuandalieni kwa wiki hii. Karibuni.
Imam Ja'afar Swadiq (as) mmoja wa Maimamu watoharifu kutoka katika kizazi cha Bwana Mtume (saw) amenukuliwa akisema kuwa, haya ni nuru ambayo inatokana na imani, na aina fulani ya hali ambayo ni kizuizi na kinga iliyopo ndani ya ujudi wa mtu ambayo huwa mkabala na kila kitu ambacho kinakinzana na Tawhidi (kumpwekesha Mwenyezi Mungu) na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu."
Kutokana na hadithi hiyo ya Imam Swadiq (as) inabainika kuwa, mtu ambaye ana haya na soni pindi anapoona kitendo fulani, jambo fulani, uamuzi, tabasamu au kutazama kitu fulani kunakinzana au hakuendani sambamba na Tawhidi, basi hujitenga na jambo hilo. Hii ni kutokana na kuwa, mtu huyo anatambua kuwa, medani ya maisha ni yenye kushuhudiwa na Mwenyezi Mungu na suala la kuona haya na kujipamba na sifa hii ni jambo linalozingatiwa na familia na jamii kwa ujumla.
Moja ya njia muhimu za mawasiliano baina ya mtu na watu wengine ni kupitia njia ya mazungumzo au maneno. Maneno yana nafasi muhimu katika kupanga na kuratibu haya na soni katika jamii. Kuona haya na soni katika kuzungumza hujitokeza katika sura tofauti. Kimsingi ni kuwa haya katika kuzungumza ni kule kubainisha mambo kwa sura inayofaa na ya mahala pake. Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha katika aya mbalimbali kwenye Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani namna ya kuzungumza na akaainisha fremu ya ya kusema na kuzungumza vizuri na kunakofaa.
Katika aya ya 235 ya Surat al-Baqarah Mwenyezi Mungu ametaja neno "Qaulun Maaruf" yaani maneno mema. Qaulun Maaruf au maneno mema ni maneno ya haki ambayo sheria na Uislamu unayapenda. Katika sehemu nyingine Mwenyezi Mungu ametumia neno "Qaulun Hasan yaani kauli njema. Qaulun Hasan ni kauli njema au kauli yenye wema ndani yake. Katika aya hiyo Mwenyezi Mungu anawataka watu wazungumze na wenzao kwa wema.
Kuhusiana na haya ya ulimi au haya katika kuzungumza, kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Ahlul Bayt wa Mtume saw. Miongoni mwa hadithi hizo ni matamshi ya Imam Sajjad (as) yaliyokuja katika Risalatul Huquuq "Risala ya Haki" kuhusiana na haki ya ulimi ambapo anasema:
"Amma kuhusiana na haki ya ulimi ni kuzungumza kwa utukufu, kujizuia usitamke maneno machafu na uulazimishe ulimi uzungumze maneno mazuri na kwa adabu na kuutahadharisha kuhusiana na kutamka mambo yasiyo na maana wala faida, ulimi usitamke isipokuwa mambo ambayo yana manufaa na dini au na dunia yako, yaani maneno mazuri, usitiri na ukinge ulimi wako na kutamka mambo ambayo hayana faina na ambayo yana athari mbaya; kwani katika hayo mwanadamu hasalimi na madhara yake. Ulimi ni ishara ya akili ya mtu, na ni pambo la akili, na uzuri wa sira na mwenendo wa mtu hudhihirika katika ulimi wake (yaani katika maneno anayotamka)."
Mfano na misdaqi nyingine ya kuona haya ni jinsi ya kutembea. Kutembea kwa haya na soni au kwa staha na kujiepusha kuwa na mwendo wa kiburi ni ishara ya kuweko sifa ya haya na soni katika ujudi wa mtu. Hali hii inaonesha jinsi mtu huyo alivyojipamba na sifa ya kuona haya na soni ambayo imefikia hatua ya kumuathiri hata ndani ya nafsi yake. Licha ya kuwa kutembea kidhahiri inaonekana ni kitendo cha kawaida, lakini utembeaji wa mtu unaweza kubainisha hali ya ndani ya mtu na hata tabia yake na wakati mwingine hubainisha na kuweka wazi shakhsia yake. Bwana Mtume saw alikuwa akitembea kwa utulivu na kwa mwendo wa kati na kati na uliojaa staha huku haya ikiwa imetawala katika mwendo wake.
Mtume saw hakuwa akitembea kwa mwendo wa kasi hata apelekee kudharauliwa na wala hakuwa akitembea kwa mwendo wa taratibu sana na wa kuchosha. Mwenyezi Mungu anasema katika Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani aya ya 63 ya Surat al-Furqan:
Na waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanaotembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
Misdaqi na mfano mwingine wa kuona haya ambako ni sharti la adabu na ishara ya shakhsia ya watu wenye akili na waumini ni kuomba idhini pindi wanapotaka kuingia katika nyumba za watu wengine.
Mwenyezi Mungu ameliashiria jambo hili katika aya za 27 na 28 za Surat Nur pale anaposema:
Enyi mlio amini! Msiingie nyumba zisio nyumba zenu mpaka muombe ruhusa, na muwatolee salamu wenyewe. Hayo ni bora kwenu mpate kukumbuka. Na msipomkuta mtu humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa: Rudini! Basi rudini. Hivi ni usafi zaidi kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.
Inanukuliwa kwamba, Mtume saw alipokuwa akienda kwa binti yake Fatima (as) alikuwa akisimama mlangoni na kuomba idhini ya kuingia. Siku moja alikwenda kwa binti yake huyo akiwa pamoja na Jabir bin Abdallah akaomba idhini na kumuombea idhini Jabir pia.
Mfano na misdaqi nyingi ya kujipamba na sifa ya kuona haya na soni ni kuwaheshimu watu wazima na wazee. Kuhusiana na hili, Bwana Mtume saw anasema kuwa, pindi kijana anapomheshimu mzee, basi Mwenyezi Mungu hulifidia hilo pindi kijana huyo atakapokuwa mzee na mtu mzima. Anasema: Mwenyezi Mungu anaona haya kumuadhibu mzee.
Aidha anasema: Waheshimuni watu wazima, kuwatukuza na kuwaenzi watu wazima ni kumheshimu Mwenyezi Mungu Mtukufu, na yeyote ambaye hawaheshimu wazee basi si katika sisi.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati, tukukatane tena juma lijalo.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …