Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 10 Aprili 2016 16:17

Hadithi ya Uongofu (37)

Hadithi ya Uongofu (37)

Ni matumaini yangu kwamba, hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale yanapokufikieni matangazo haya ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tunakutana tena katika sehemu nyingine ya mfululizo huu wa Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha juma lililopita kilizungumzia kuwa na haya na soni na jinsi sifa hii ya kimaadili ilivyo na umuhimu katika kumzuia mtu kutenda dhambi na mambo machafu. Sehemu ya 37 ya kipindi hiki juma hili itakunukulieni baadhi ya hadithi zinazohusiana na haya na soni pamoja na kueleza aina ya haya na soni. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi.

Haya au soni ni miongoni mwa maudhui za kikhlaqi na kimadili ambazo zimetajwa katika Kitabu Kitukufu cha Qur'ani. Haya ni aina fulani ya kizuizi na kinga ya mtu inayomfanya asitamke au kufanya kila kitu kilichoko moyoni mwake. Watu ambao hawana haya wala soni na ambao hufanya dhambi mbele ya kadamnasi, kwa mtazamo wa Uislamu, hawana heshima, hadhi wala shakhsia.
Imam Ja'afar Swadiq (as) alimwambia Mufadhwal bin Omar kuhusiana na kuwa na haya au aibu pamoja na athari zake kinafsi kwamba:
Kama taathira ya haya au aibu isingekuwepo basi mgeni asingeheshimiwa na wala utekelezaji wa ahadi usingezingatiwa. Kama soni au haya isingekuweko, basi watu wasingekuwa wanawasaidia wenzao na kutekeleza haja zao, kusingekuwa na msukumo wa kufanya mambo mazuri na watu wasingekuwa wanajitenga mbali na mambo mabaya. Soni au haya haina taathira tu katika kutekeleza majukumu ya kiakhlaqi, bali ina nafasi muhimu sana katika kutekeleza faradhi na mambo ya wajibu kisheria. Kwani kuna watu laiti hali ya haya na kuona aibu isingekuweko na laiti wasingekuwa wanaogopa kulaumiwa basi wasingechunga haki ya baba na mama na vile vile wasingetekeleza haki ya wana ndugu. Kama haya isingekuweko, amana za watu zingerejeshwa kwa wahusika na kusingefumbiwa macho amali yoyote ile ambayo inakinzana na heshima." Mwisho wa kunukuu.
Sifa zote njema sambamba na kuwa ni lazima kuzitekeleza na kuzifanyia kazi, wakati huo huo kwa namna fulani zinahesabiwa kuwa ni fadhila na utukufu. Endapo wakati wa kutekeleza sifa hizo zinazopendeza mtu atavuka mpaka wa kufanya mambo kati na kati, basi badala ya kuwa ni sifa za kusifiwa huwa ni sifa zinazokemewa.
Kuhusiana na sifa ya kuona haya au soni, hali ya mambo iko hivi hivi. Bwana Mtume (saw) ameigawa haya au soni katika makundi mawili. Haya ya kiakili na haya ya kijinga. Haya ambayo chimbuko lake ni akili ni haya na soni ya kusifiwa na inayotakiwa na katika Uislamu inahesabiwa kuwa na fadhila. Aina nyingine ya haya au soni ni ile ambayo inakemewa na ambayo si ya kiakili yaani ni ya kijinga na chimbuko lake sio akili. Haya hii ni ile hali ya kuona soni na aibu mahala ambapo mtu hapaswi kufanya hivyo. Chimbuko la aibu ya namna hii ni udhaifu wa nafsi na tabia ya kujiona mnyonge na dhalili mbele ya watu wengine. Kwa maneno mengine ni kuwa ni hali fulani ya nafsi ya kujiona duni kwa wengine.
Katika hadithi nyingine inayofanana na ile tuliyotangulia kuisoma, Bwana Mtume (saw) anasema: "Kuna aina mbili za haya. Ya kwanza ni ile inayotokana na udhaifu na uduni wa kutoweza kufanya kitu na aina ya pili ni ishara ya ukamilifu, Uislamu na imani." Kwa muktadha huo, haya na soni ambayo ni ishara ya udhaifu wa mtu sababu ya hilo, ni ujinga, ujahili na ufinyu wa kufikiri mambo. Na mkabala wake ni haya na soni ambayo inaashiria nguvu, Uislamu na imani na sababu ya hilo ni kuweko akili salama katika uujidi wa mtu ambaye amejipamba kwa sifa ya haya. Ni kutokana na ukweli huo, ndio maana Amir al-Muuminina Ali bin Abi Twalib anaona kuwa, watu wenye akili zaidi ni wale ambao wamejipamba zaidi na sifa ya haya na soni.
Ukweli wa mambo ni kuwa, wakati mwingine mtu huona haya au soni mahala ambapo hapaswi kufanya hivyo na hata hatua yake hiyo haina uhalali wa kiakili na hata wakati mwingine hatua yake hiyo hukemewa na kukatazwa. Hii ni kutokana na kuwa, anaona haya na aibu mahala ambapo hapaswi kufanya hivyo. Haya inayokatazwa ni ile ambayo inatokana na ujinga na ujahili wa mtu. Kwa mfano mtu kuona haya kufanya jambo fulani ambalo watu wa kawaida katika jamii wanaliona kuwa ni baya na lisilofaa ilihali akili au hata sheria hailitambui jambo hilo kwamba, ni baya. Kwa maneno mengine ni kwamba, mtu huyu amewaonea aibu watu na kufumbia macho, akili, mantiki na hata sheria. Au kwa mfano, mtu hapaswi kuona haya au kuona aibu katika kusema haki au kuibainisha. Moja ya sababu za kuacha kuamrishana mema na kukatazana mabaya ni kuona haya na aibu mahala ambao hapastahiki. Tab'an mtu anapaswa kuchunga heshima na adabu katika kubainisha haki, lakini sharti hilo halipaswi kumzuia aache kusema haki.
Imam Ali bin Abi Twalib (as) amesema: Kila ambaye anaona haya kusema maneno ya haki, basi ni mchache wa kufikiri.
Mwanadamu anapaswa kutambua kwamba, kuna wakati anapotaka kusema jambo fulani la haki, shetani humshawishi katika nafsi yake na kutaka kumuonesha kwamba, jambo analotaka kulisema litampunguzia heshima yake. Lakini la msingi ni kwamba, mwanadamu anapaswa kuelewa kwamba, kusema neno la haki hata kama kidhahiri ni kuchungu au hata huenda kusimpendeze anayeambiwa haki hiyo, lakini atapata izza na heshima ya Mwenyezi Mungu kwa kusema haki. Hivyo basi kuona haya au kuwa na soni mahala ambapo si pake ni kufanya jambo pasina ya kutumia akili na inaonesha jinsi mtu anayefanya hivyo alivyokuwa ni mchache wa kufikiri.
Kwa hakika hukumu na sheria ziko kwa namna ambayo wakati mwingine katika baadhi ya mambo mtu huona haya kusema au kuuliza. Aina hii ya aibu na haya hupelekea kutotekelezwa sheria za Mwenyezi Mungu. Hali iko hivyo hivyo katika masuala ya kielimu. Mtu hapaswi kuona haya kutokana na uchache wa elimu aliyonayo bali anapaswa kufanya hima kwa ajili ya kutafuta elimu. Imam Ali (as) anasema kuhusiana na hili kwamba: Mtu asiyeone haya kujifunza lile ambalo halijui.
Katika jamii tunayoishi hii leo tunaona kuwa, kuna watu wengi ambao wanaona aibu kutamaka neno "sijui". Ukweli wa mambo ni kuwa, katika kujifunza na kutafuta elimu, suala la kuona haya au aibu halina maana yoyote. Imam Ali as anasema: Wakati unapokuwa huna ujuzi na welewa wa kitu fulani, basi unapoulizwa usione haya wala aibu kusema "sijui."
Sehemu nyingine ambayo mtu hapaswi kuona haya ni wakati wa kuomba radhi baada ya kufanya kosa. Endapo mtu atafanya jambo ambalo halifai, anapaswa kuomba msamaha na hapaswi hata kidogo kuona haya kufanya hivyo. Aidha wakati mtu anapotafuta au anapopigania haki hapaswi kuacha hilo kwa kuona haya na soni.
Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) amesema kuwa: Mtu hapaswi kuona haya katika mambo matatu: Kuhudumia wageni, kusimama (kwa ajili ya kuonesha heshima) anapoingia baba au mwalimu na kupigania haki hata kama mchango wake katika hilo ni mdogo.
Katika mambo mengine ambayo mtu katika hayo hapaswi kuona haya ni suala la kutafuta riziki ya halali. Mtu anayefanya kazi kwa ajili ya kuihudumia familia yake na kuiletea utulivu kupitia kipato cha halali, hapaswi kuona haya hata kama kazi hiyo itaonekana na watu wengine katika jamii kwamba, sio kazi nzuri.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia kikomo tukutane tena wiki ijayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh...

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …