Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 14 Aprili 2016 15:10

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (31) na sauti

Abdul-Azizi Bin Saud enzi za uhai wake. Abdul-Azizi Bin Saud enzi za uhai wake.

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuungana nami tena katika sehemu ya 31 ya makala ya chimbuko la utakfiri yanayozungumzia chanzo cha makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine na kutenda jinai za kutisha dhidi yao. Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa, kwa kipindi chote cha historia ya Uwahabi, daima wahanga wakubwa wa jinai za kundi hilo wamekuwa ni Waislamu wa Kisuni, na kwamba madai ya viongozi wa leo wa Mawahabi kuwa, adui yao mkubwa ni Mashia, hayana ukweli wowote. Tukasema kuwa, baada ya Mawahabi kumaliza kuwaua Mashia, watageuza ncha ya upanga wao kwa Waislamu wa Kisuni na kuwaua kama walivyofanya huko nyuma, na hasa kwa kuzingatia kuwa, wafuasi wa genge hilo wanaamini kwamba Waislamu halisi ni wale wenye imani za Kiwahabi tu. Kufuatia hali hiyo, Hafidh Wahab mmoja wa watu wa karibu sana na utawala wa Aal-Saud anaandika katika kitabu chake cha 'Jaziiratul-Arab' kama ninavyomnukuu: "Kwa mujibu wa Abdul-Aziz Bin Saud, wakati babu yetu Muhammad Bin Saud alipokuwa akijishughulisha na vita dhidi ya makabila ya Hijaz, aliteka kundi moja miongoni mwa watu wa kabila la Matwir wa Kisuni. Kufuatia hali hiyo, baadhi ya viongozi wakubwa na wazee wa kabila hilo walikuja kuwaombea msamaha ndugu zao kwa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab ili watu wale waachiliwe huru. Hata hivyo Muhammad Bin Saud alitoa amri ya kukatwa vichwa watu wale. Na baada ya kutekelezwa amri hiyo, vichwa vya wahanga wale viliwekwa katika sahani za chakula na kisha vikaletwa mbele ya viongozi wa kabila lile la Matwir. Baada ya hayo Ibn Saud alitoa amri kwa wazee wa kabila la Matwir wale vichwa vya ndugu zao na walipokataa kufanya hivyo aliamuru nao wauawe na kukatwa vichwa." Mwisho wa kunukuu. Wakati watu wa makabila ya Waislamu wa Kisuni walipokumbwa na hujuma za kikatili za watawala wa kundi la Kiwahabi, waliamua kukimbilia katika maeneo ya Waislamu wa Kishia ya mashariki mwa maeneo ya Hijaz hususan Al-Ahsa. Itafahamika kuwa, Al-Ahsa ni mji ambao tangu zamani ulikuwa wa Waislamu wa Kishia huku kukienea pia mafundisho ya Ahlu Bayti wa Mtume (saw). Katika kipindi chote cha historia, Mawahabi walikabiliwa vikali na matatizo mbalimbali yanayotokana na muqawama wa Waislamu hao wa Kishia katika kupinga njama chafu za Mawahabi za kutaka kulitwaa pia eneo hilo. Hata hivyo watawala wa Aal Saud kwa kutumia nguvu nyingi zilizoendana na kutekeleza mauaji ya halaiki, ndipo wakaweza kuudhibiti mji huo wa Al-Ahsa. Aidha mkoa wa Al-Ahsaa au kwa jina lingine mashriki mwa Saudia, unahesabiwa kuwa mkoa mkubwa zaidi nchini humo, ambapo miji ya Hofuf, Dammam na Qatif imo ndani ya mkoa huo. Mbali na hayo ni kwamba, mkoa huo ni miongoni mwa maeneo muhimu yenye utajiri wa mafuta ndani ya Saudia. Uepo wa Waislamu wa Kishia na Kisuni katika eneo hilo, umewafanya Mawahabi kushindwa kupenyeza ushawishi wao, licha ya eneo hilo kuwa chini ya udhibiti wa utawala huo wa kikatili. Hii ni kusema kuwa, kila wakati ambapo Mawahabi walijaribu kutaka kuudhibiti kikamilifu mkoa huo wa Al-Ahsa ili kupenyeza mafundisho yao potofu, kulijiri mapambano makali dhidi ya watu wa kundi hilo na hivyo kukwamisha njama chafu za Mawahabi. Hii leo pia, mkoa huo unahesabika kuwa kitovu muhimu cha Waislamu wa Kishia nchini Saudia.

************************************************

Katika juzu yake ya kwanza ya kitabu cha ‘Unwanul-Majdi fii Taarikhin-Najdi’ Ibn Bushr anaandika kuhusu moja ya hujuma za kijeshi za Mawahabi dhidi ya moja ya maeneo ya mkoa wa Al-Ahsaa kama ninavyomnukuu: “Ilipotimia asubuhi askari wa Kiwahabi walipanda farasi wao na kuelekea moja ya maeneo ya mji huo. Mbingu ikawa nyeusi na ardhi ikapatwa na mtetemeko. Moshi na moto vikapaa angani. Wanawake wajawazito wa mji huo wakaporomoa mimba zao. Kisha Saud akavamia na kutia kambi ndani ya mji huo. Katika kipindi hicho mtu yeyote aliyetaka kumuua au kumtia jela basi alifanya alivyotaka. Aidha mfalme huyo alipora mali za wakazi wa mji huo na kama hiyo haitoshi akaharibu kabisa nyumba zao. Mfalme alishiriki binafasi katika mauaji hayo ambapo aliua watu wengi kwa mkono wake. Katika vita hivyo, mtawala huyo alipora mali nyingi za Waislamu ambazo ilikuwa vigumu kuweza kuzielezea.” Mwisho wa kunuu. Hata hivyo jinai za Aal-Saud kwa kushirikiana na Mawahabi katika eneo la Hijazi hazikuishia hapo. Hii ni kusema kuwa, tangu mwanzo wa kuasisiwa utawala huo wa Kiwahabi, viongozi wake walikuwa na fikra moja tu ya kutwaa na kudhibiti maeneo matukufu ya Waislamu wa Kishia hususan nchini Iraq. Kama walivyoyakalia kwa mabavu maeneo mengine ya ardhi za Waislamu, Mawahabi walifanya mashambulizi yao kwa nara ya kupambana na kile walichokidai kuwa ni kupambana na waabudu masanamu na kueneza Tawhidi. Katika hujuma hizo, Waislamu wa Kishia kama walivyokuwa wafuasi wa dhehebu la Hanbali na Waislamu wengine wa Kisuni, walituhumiwa kuwa ni makafiri. Katika kipindi cha utawala wa Abdul-Aziz wa kwanza, mtoto wake Saud ambaye alikuwa na jukumu la kushambulia maeneo ya Waislamu, aliandaa jeshi kubwa kwa ajili ya kufanya hujuma dhidi ya mji wa Karbala, Iraq. Ibn Bushr anasimulia vita hivyo kwa kuandika kama ninavyonukuu: “Mwaka 1216 Hijiria, akiongoza jeshi kubwa linaloundwa na watu wa Hijaz, Tihamah, Najd na viunga vyake, Saud alielekea mjini Karbala na kufika katika mji huo lilipo kaburi la Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Muhammad (saw). Baada ya hapo mtawala huyo wa Kiwahabi alitoa amri ya kubomolewa kuta zake na haraka askari wake wakaingia ndani ya mji huo. Askari hao waliwaua kwa umati watu ambao walikutwa sokoni au majumbani mwao.” Mwisho wa kunukuu. Mwakilishi wa Russia anaelezea uvamizi huo wa Aal-Saud kupitia ripoti yake aliyoiwasilisha mbele ya ubalozi wa nchi hiyo kwa kusema: “Ghafla Mawahabi elfu 12 walishambulia kaburi la Imamu Hussein na baada ya kupora vitu vya thamani walifanya kama walivyokuwa wakifanya dhidi ya miji mingine, na hakukusalia mtu aliyekuwa hai bila kuuawa na panga za wavamizi hao. Wazee, watoto wadogo na wanawake nao hawakupona kutokana na mauaji hayo ambapo askari wa Kiwahabi hawakuwa na huruma wala utu mioyoni mwao. Aidha askari hao hawakusitisha mauaji yao ambapo kutokana na umwagaji damu mkubwa, zaidi ya watu 4000 waliuawa huku ngamia 4000 nao wakichukuliwa kama ngawira. Kufuatia mauaji hayo haram ya Imam Hussein ilishuhudia uharibifu mkubwa huku ikijawa damu za wahanga wa jinai hizo za Mawahabi.” Mwisho wa kunukuu. Baada ya tukio hilo chungu, Saud aliendeleza mashambulizi mtawalia dhidi ya mji huo wa Karbala na kufanya jinai ingawa hakuweza kufikia malengo yake haramu ya kuufanya mji huo mtukufu kuwa wa Kiwahabi. Naye kwa upande wake Ibn Bushr mwanahistoria maarufu anaelezea matukio ya mwaka 1220 Hijiria yanayohusiana na hujuma ya Aal-Saud dhidi ya mji mwingine wa Najaf nchini Iraq kwa kuandika: “Baada ya Saud kuvamia mji huo wa Najaf mwaka huo, alikabiliwa na mapambano makali ya watu wa kujitolea wa mji huo wakiwemo maulama, wanafunzi na wakazi wake. Hatimaye mapambano hayo yakalitia hasara kubwa jeshi vamizi la Kiwahabi na kumpelekea Saud kuamua kurejea nyuma kutoka mjini hapo.” Mwisho wa kunukuu.

**********************************************

Utawala wa Abdul-Aziz kwa uungaji mkono mkubwa wa Uingereza uliweza taratibu kupanua wigo wa uongozi wake katika maeneo tofauti ya bara Arab. Hata hivyo bado mtawala huyo alikuwa na wasi wasi mkubwa juu ya kudhibiti haram mbili takatifu za Makkah na Madina. Kama tulivyosema katika vipindi vilivyopita, Uingereza ilifikia ukweli huu kwamba, Hussein ibn Ali al-Hashimi aliyekuwa mtawala wa mji wa Makkah, asingeweza kudhamini malengo ya London katika eneo hilo. Kufuatia hali hiyo, mwezi Disemba mnamo mwaka 1924 Miladia na kwa amri ya Abdul-Aziz, kukafanywa hujuma kubwa dhidi ya mji wa Ta'if. Itakumbukwa kuwa, mji wa Ta’if ni mji mkongwe na wenye historia ndefu na mzuri ambao uko karibu na mji mtukufu wa Makkah. Baada ya uvamizi huo askari wa jeshi la Kiwahabi chini ya Abdul-Aziz wakajihalalishia mji huo kwa kipindi cha miezi mitatu ambapo walifanya kila aina ya jinai. Katika kipindi hicho, maelfu ya wakazi wa mji huo walikimbia kukwepa ukatili wa Mawahabi huku wanawake na watoto wakijikuta wahanga wakubwa wa jinai hizo. Kudhibitiwa mji wa Ta'if ulikuwa mwanzo wa kuvamiwa mji mtukufu wa Makkah. Hata hivyo na pamoja na juhudi zote hizo za Abdul-Aziz bado hakuwa na imani kamili kwa Uingereza kama ingeendelea kumuunga mkono au la. Kuhusu suala hilo, mtawala huyo wa Kiwahabi alikuwa akihofia kwamba huenda London ingevutiwa na utawala wa Hussein ibn Ali al-Hashimi wa Makkah dhidi yake. Hasa kwa kuzingatia kuwa, tayari mtawala huyo wa Makkah alikuwa amekubali baadhi ya mapendekezo ya Uingereza kupitia njama na ushawishi wa Thomas Edward Lawrence maarufu kwa jina la Lawrence wa Saudia aliyetumwa na London kwenda kwake. Kufuatia hayo, mwezi Oktoba mwaka 1924 Miladia, jeshi la Kiwahabi likauvamia mji wa Makkah. Wakazi wa mji huo ambao tayari walikuwa wameshuhudia mauaji na jinai za kutisha za Mawahabi dhidi ya watu wa mji wa Ta’if, hawakuweza kukabiliana na askari hao vamizi kutokana na khofu iliyotawala mioyo yao. Kwa ajili hiyo, Mawahabi wakapora na kutwaa mali na utajiri wote wa wakazi wa mji huo mtukufu bila ya kuwepo upinzani wowote ule. Mwezi Disemba mwaka huo huo Abdul-Aziz akiwa na askari wengi, aliingia mji huo wa Makkah na mwaka 1925 na 1926 Miladia taratibu utawala wa Aal-Saud ukaenea katika miji ya Makkah na Madina.

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala yanayoangazia macho wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 31, kinakomea hapa kwa leo. Tutakutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Allah. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati huo ninakuageni kwa kusema, kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …