Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 07 Aprili 2016 18:56

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (30) na sauti

Abdul-Aziz Aal-Saud akiwa pamoja na wakoloni wa Uingereza katika kupanga njama zao dhidi ya Uislamu Abdul-Aziz Aal-Saud akiwa pamoja na wakoloni wa Uingereza katika kupanga njama zao dhidi ya Uislamu

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami tena katika sehemu 30 ya mfululizo wa vipindi hivi vinavyoangazia macho wimbi la makundi yanayowakufurisha Waislamu na kutenda jinai za kutisha dhidi yao.

Katika kipindi kilichopita, tuliashiria namma ambavyo wakuu wa koo mbili za Ibn Abdul-Wahhabi maarufu kwa jina la Aal-Sheikh na za Ibn Saud maarufu kwa jina la Aal-Saud, walikuwa wakisaidiana katika kulinda maslahi yao huku wakiendelea kujitajirisha kwa mali za Waislamu.

Kwa kuchunguza historia ya Uwahabi inatubainikia kwamba, kile kilichowasukuma watu wa ukoo huo katika kuandaa jeshi la Kiwahabi, ilikuwa ni kupora mali za Waislamu hususan za Masuni na Mashia, jambo ambalo lilifungua mlango kwa makafiri kuweza kutoa pigo kwa umma wa Kiislamu. Aidha lengo lingine muhimu la Mawahabi katika kuwalingania watu kujiunga na genge hilo, ni kupanua wigo wa utawala wa ukoo wa Aal-Saud dhidi ya jamii ya Kiislamu duniani. Kwa kuzingatia kuwa Muhammad Ibn Saud katika kikao chake cha kwanza na Muhammad Ibn Abdul-Wahhab alimueleza kuwa, wasi wasi wake katika kumsaidia kueneza imani yake potofu ilikuwa ni kuhofia kwamba, baada ya kupata ushindi, Ibn Abdul-Wahhab angeweza kuachana na Aal-Saud na kujiunga na watawala wengine. Hivyo ukoo wa Ibn Abdul-Wahhabi maarufu kwa jina la Aal-Sheikh daima ulikuwa na jukumu muhimu la kuonyesha utiifu na kuulinda kwa kila hali ukoo wa Aal-Saud. Aidha suala hilo limekuwa likishuhudiwa katika vipindi vyote vya historia ya Uwahabi hadi hii leo. Kwa ibara nyingine ni kwamba, ikiwa tutahitaji kuugawa Uwahabi katika mtazamo wa kisiasa na kidini, hakuna shaka kwamba, tutagundua kuwa, kundi la Uwahabi lipo tu kwa ajili ya kutumikia malengo haramu ya utawala huo wa ukoo wa Aal-Saud na si vinginevyo. Masheikh wa kundi hilo la Uwahabi kupitia nara na kaulimbiu ya Tawhidi, wameweza kufikia malengo yao machafu ambapo kwa nara hiyo na kupitia misaada mbalimbali ya Uingereza, wameweza kuwatawalisha watu wa ukoo wa Aal-Saud juu ya bara Arab, lenye turathi za Kiislamu duniani.

****************************************

Kwa ajili hiyo tunaweza kusema kuwa, muungano uliopo baina ya utawala wa Aal Saud na Uwahabi ni muungano wa maslahi ya pande mbili. Mawahabi kupitia upanga na utajiri uliotokana na mauaji dhidi ya Waislamu, wameweza kuendeleza maisha yao, huku kwa upande wao Aal Saud sanjari na kutumia nara za kundi hilo la Uwahabi, wameweza pia kufikia utajiri mkubwa na kulinda utawala wao hadi hii leo. Kinyume kabisa na madai ya Mawahabi wa leo wanaowataja Waislamu wa Kishia kuwa eti ndio adui nambari moja wa genge hilo, ukweli ni kwamba wahanga wakuu wa Mawahabi tangu awali, wamekuwa ni Waislamu wa Kisuni wakiwemo hata wafuasi wa dhehebu la Uhanbali. Uhalisia wa mambo ni kwamba, lengo la Mawahabi kuwataja Mashia kuwa ndio maadui wao wa pekee sanjari na kuwashawishi Waislamu wa Kisuni washirikiane nao katika kuwaua Waislamu hao wafuasi wa Ahlu Bayt wa Mtume (saw), ni kutaka kuwahadaa Waislamu hao. Hii ni kusema kuwa, baada ya Mawahabi kutekeleza ajenda hizo dhidi ya Waislamu wa Kishia, hakuna shaka kwamba, watageuza makali ya upanga wao dhidi ya Masuni. Historia ya kundi hilo na mauaji makubwa dhidi ya Waislamu wa Kisuni katika vipindi tofauti vya upinzani wao kwa kundi hilo, inathibitisha ukweli huo. Ndugu wasikilizaji mnafaa kufahamu kwamba, Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, aliwataja Waislamu wote kuwa ni makafiri huku kundi la kwanza kutajwa kwa ukafiri likiwa ni la watu wa mji wa Najd. Kwa mujibu wa Ibn Abdul-Wahhab, wakazi wote wa mji wa Najd ni makafiri na kwa msingi huo, damu, wake na mali zao ni halali. Aidha alitangaza wazi kuwa, Waislamu pekee ni wale wenye imani aliyonayo yeye na Muhammad Ibn Saud. Ni kutokana na mielekeo hiyo ndipo Aal Saud wakaanzisha mauaji makali dhidi ya wakazi wa mji huo wa Najd. Itakumbukwa kuwa, wakati wa kujiri muungano wa pande mbili hizo, eneo la kwanza kukodolewa macho ya upanga wa Mawahabi kutaka kupora mali zake na kulitawala, ulikuwa mji wa Riyadh ambao ulikuwa karibu na eneo la Dariyah, makao makuu ya utawala wa Aal Saud enzi hizo. Vita kati ya watawala wa Riyadh ambao walikuwa wa Kisuni na Dariyah wa Kiwahabi, vilidumu karibu miaka 30. Hata hivyo uwezo mkubwa aliokuwanao, Daham bin Dawas, mtawala wa mji wa Riyadh, ulimfanya Muhammad Bin Saud kushindwa kumuondoa madarakani. Vita hivyo vikali mbali na kusababisha uharibifu mkubwa na kujeruhiwa maelfu ya watu, vilipelekea pia watu 4,000 kuuawa. Hata hivyo mwaka 1187 mwanaye, yaani Abdul-Aziz Bin Muhammad Aal Saud, aliunda jeshi kubwa la kichokozi na kuelekea Riyadh. Jeshi la Abdul-Aziz liliwaua kwa ukatili wakazi wote wa mji huo wakiwemo pia wanyama, huku wanawake wakitekwa nyara na kufanywa kuwa wajakazi. Ndugu wasikilizaji ni jambo lililo wazi kwamba hata kama mtu atakuwa na uadui kiasi gani, katu hawezi kukosa mapenzi kwa mji wake asili alikozaliwa kama alivyosema Mtukufu Mtume Muhammad (saw): "Kupenda watani ni miongoni mwa imani." Mji wa Uyainah ni mahala alipozaliwa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab na mahala walipoishi babu zake huku baba yake mzazi pia akiwa kadhi mkubwa wa dhehebu la Hanbali ambalo lilikuwa likifuatwa na wakazi wote wa mji huo kwa miaka mingi. Licha ya hayo, wakazi wa mji huo nao hawakupona kutokana na upanga wa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab na Muhammad Bin Saud waliokuwa na kiu ya kumwaga damu za wakazi wa mji huo kufuatia fatwa za ukufurishaji zilizotolewa na viongozi hao wa Uwahabi.

**********************************************

Baada ya Othman bin Muammar, mtawala wa mji wa Uyainah na aliyemuozesha binti yake Ibn Abdul-Wahhabi, kufahamu uhalisia wa fikra potofu za Uwahabi zinazopingana na mafundisho asili ya Uislamu na kufuatia mashinikizo ya maulama wa Kisuni wa miji ya al-Ahsa, Basra, Maka na Madina dhidi yake, aliamua kumfukuza kiongozi huyo wa Uwahabi mjini hapo. Akiwa bado na kinyongo kwa mtawala huyo, Ibn Abdul-Wahhabi alikimbilia kwa Muhammad Bin Saud, mtawala wa Dirayah ambapo akiwa hapo alimtaja Othman Bin Muammar kuwa ni kafiri na mshirikina na hivyo akatoa fatwa ya ulazima wa kuuawa kiongozi huyo wa Kisuni wa mji wa Uyainah. Baada ya fatwa hiyo baadhi ya watu wa karibu na Othman waliokuwa tayari wameathiriwa na mafundisho ya Muhammad Ibn Abdul-Wahhabi, wakamuua kiongozi huyo baada ya sala ya Ijumaa ndani ya mwezi wa Rajab sawa na mwaka 1169 Hijiria. Baada ya mauaji hayo, Ibn Abdul-Wahhabi alirejea tena mjini Uyainah na kuiharibu kabisa nyumba ya mtawala huyo. Hata hivyo wakazi wa mji huo hawakuridhia hujuma hiyo, na ni kwa ajili hiyo ndipo wakaanzisha harakati za kupambana na kundi hilo jipya la Uwahabi pamoja na kiongozi wake Ibn Abdul-Wahhab. Mapambano yao hayakuchukua muda kutokana na kusambaratishwa haraka na jeshi la Kiwahabi. Katika kuzima harakati hizo za upinzani, askari hao wa Kiwahabi walitekeleza mauaji makubwa dhidi ya wanaume na watoto wa mji huo huku wakiwateka nyara wanawake wao na kuwafanya kuwa wajakazi. Aidha askari hao wenye mioyo ya kikatili waliharibu nyumba sanjari na kuitia moto miti na mashamba ya wakazi wa mji huo waliouawa. Baada ya hapo mji wa Uywainah ukageuka kuwa magofu. Hali hiyo haikuishia kwa mji pekee wa Uyainah, bali kila mji ambao wakazi wake walijaribu kupinga fikra potofu za kundi la Kiwahabi, ulikumbwa na mauaji ya kutisha kutoka kwa askari wa kundi hilo na kisha wanawake wake kufanywa kuwa mateka na kuharibiwa kabisa. Ni kama ambavyo hii leo kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na makundi mengine yenye fikra sawa na genge hilo yanavyofanya dhidi ya wakazi wa maeneo na miji tofauti inayotangaza kupingwa fikra za Kiwahabi. Kwa hakika kundi hilo mbali na kuwa na fikra za kitakfiri katika kutenda jinai dhidi ya binaadamu, kadhalika limeiga ukatili wa kutisha kutoka kwa viongozi wa awali wa Kiwahabi na Aal-Saud. Aidha tunaweza kusema kuwa, jinai ambazo zinafanywa na makundi ya kitakfiri na kigaidi yakiwemo Daesh, huko Syria, Iraq na Libya, Boko Haram huko Nigeria, Cameroon na Chad, ash-Shabab huko nchini Somalia na Kenya, Answaru Sharia huko Tunisia na kadhalika, ni urithi wa karne iliyopita kutoka kwa waasisi wa genge hilo la Uwahabi. Jinai hizo kama tulivyosema, hazielekezwi tu kwa Waislamu wa Kishia kama wanavyodai wafuasi wa Uwahabi, bali tangu awali Ahlus-Sunna Wal-Jamaa wamekuwa wahanga wakuu wa mauaji hayo. Kwa kipindi cha miaka yote ambayo Mawahabi wamekuwa wakipata uungaji mkono kutoka Uingereza na kudhibiti kikamilifu eneo la Najd na maeneo mengine yaliyo kando na mji huo, Mawahabi wamekuwa wakitumia nguvu zao zote katika kuwaua Waislamu wa Kisuni. Kwa mujibu wa wanahistoria, wakazi wa miji ya Najd na Hijaz, hawakujiunga na Uwahabi kwa hiari yao wenyewe, bali kwa kulazimishwa na kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya kifo. Wataalamu wa historia ya Uwahabi hususan Ibn Bushr na Ibn Ghanam, wameelezea kwa kina vita vyote na mauaji yaliyofanywa na wanachama wa kundi hilo katika karne iliyopita. Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala yanayoangazia macho wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 30, kinakomea hapa kwa leo. Tutakutana tena wiki ijayo panapo majaaliwa ya Allah. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati huo nakuageni kwa kusema, kwaherini.

Bonyeza hapa chini kupata sauti ya kipindi hiki:

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …