Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 06 Aprili 2016 15:55

Hadithi ya Uongofu (36)

Hadithi ya Uongofu (36)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hii cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia kuwa na haya na soni na kukunukulieni baadhi ya hadithi za Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu (a.s) kuhusiana na suala hili. Kuweni nami hadi mwisho wa dakika hizi chache ili kutegea sikio niliyokuandalieni kwa leo, hii ikiwa ni sehemu ya 36 ya mfululizo huu.

******
Moja ya kinga na vizuizi ambavyo huihifadhi jamii na kuizuia na mambo machafu na upotofu ni kuwa na haya na soni. Kiistilahi haya au soni ina maana ya hali fulani ya ndani ambayo hupelekea kuweko utulivu na unyenyekevu katika matendo na harakati, na hivyo kuleta hali ya utulivu kwa mwanadamu. Hali hii humzuia mtu kufanya mambo machafu na yasiyofaa. Kiujumla chimbuko la haya na soni ni woga wa kulaumiwa na kuumbuliwa mtu na watu wengine. Kadiri haya na soni inavyokuwa imara kwa mwanadamu, ndivyo hivyo hivyo shakhsia ya kiutu ya mtu huyo inavyokuwa na hadhi na wakati huo huo mtu wa namna hiyo huwa na umakini katika amali na matendo yake. Kwa muktadha huo, mtu ambaye amejipamba na haya na soni hujitenga mbali zaidi na mambo ambayo yanakinzana na shakhsia ya mwanadamu. Kwa mtazamo wa mbora wa viumbe Mtume Muhammad saw ni kuwa:
"Haya na soni kwa mtu yeyote yule, huwa sababu ya pambo na utanashati kama ambavyo kutokuwa na haya huufanya ujudi wa mtu kutokuwa na mzuri na usiopendeza."
Kujipamba na sifa ya haya na soni ni mithili mti mzuri ambao una matawi mengi na matunda ambayo yamening'inia. Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuwa: Kile ambacho ni chimbuko la haya na soni ni ulaini na upole, kumzingatia Mwenyezi Mungu katika dhahiri na siri, kujiweka mbali na mabaya, kusamehe na kadhalika..... Hizi ni faida za hekima ambayo inatokana na kujipambana na sifa ya haya. Ni jambo zuri lilioje kwa wale ambao wanazikubali nasaha za Mwenyezi Mungu na wanaogopa kuumbuliwa (kutokana na kutokuwa na haya).
Katika hadithi nyingi sifa ya haya na soni imetambulishwa kuwa ni makhsusi kwa ajili ya kiumbe mwanadamu. Hii ni kutokana na kuwa akili ni katika sifa za kipekee za kiumbe mwanadamu ambayo inalazimiana na haya na soni.
Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) anasema kuwa:
Jibril alimshukia Nabiallah Adam (a.s) na kumwambia, nimetumwa na Mwenyezi Mungu nije nikwambia uchague kitu kimoja kati ya hivi vitatu na vingine uviache. Nabii Adam akauliza, vitu hivyo ni vipi? Jibril akamjibu Adam AS kwa kumwambia, vitu hivyo ni akili, haya na dini. Adam AS akasema, mimi nimechagua akili. Jibril akaviambia haya na dini: Mwacheni, na nendeni zenu. Haya na dini vikasema, sisi tumeamrishwa tuwe pamoja na akili popote pale inapokuwa, na tusitengane nayo. Jibril akasema, basi kwa kuwa ni hivyo, fanyeni lile mliloamrishwa. Kisha Jibril akapaa mbinguni." Hii ni kutokana na kuwa, endapo akili itatenganishwa na dini ni rahisi mno kupotea au kuelekea katika upotofu.
******
Kwa hakika kuwa na haya na soni ambako humzuia mtu kufanya dhambi na mambo machafu, ni mti wenye matunda ya maarifa, akili na hekima.
Baadhi ya hadithi zimetambua juu ya kuweko mfungano baina ya haya au soni na itikadi ya mtu kwa Mwenyezi Mungu na zikabainisha kwamba, haya au soni ni jambo linaloambatana na imani ya mtu. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokewa kutoka kwa Bwana Mtume saw ambapo amenukuliwa akisema: Soni na haya ni tawi la imani na mtu ambaye hana haya basi hana imani. Imam Ja'afar Swadiq (as) amesema kuwa, Haya ni katika imani na imani itakuwa peponi. Aidha katika sehemu nyingine Imam Swadiq amenukuliwa akisema kwamba: Haya na imani viko pamoja na bega kwa bega, na kimoja kinapoondoka kingine humfuata mwenziwe.
Kwa msingi huo na kupitia hadithi hizo tulizonukuu inabainika wazi kwamba, haya ni matunda ya imani. Kadiri imani ya mtu itakavyokuwa imara, basi haya na soni hushuhudiwa katika vitendo vya mtu huyo na yeye huwa na hisia ya kuona haya na soni katika kutenda mambo mabaya kuliko mtu mwingine. Mkabala na hilo ni kuwa, kadiri imani ya mtu inavyokuwa dhaifu, basi mtu huyo huwa na ujeuri na kiburi cha kufanya dhambi kuliko mtu mwingine.
Katika baadhi ya hadithi imeashiriwa kuwa, kumzingatia Mwenyezi Mungu katika mambo yote na kuamini kwamba, yupo na ni mwenye kushuhudia matendo na amali zetu, ni jambo ambalo huwa na taathira katika kuimarisha hali ya kuona haya na soni.
Imam Sajjad Zein al-Abidiin anasema kuhusiana na hilo kwamba; Muogope Mwenyezi Mungu kutokana na uwezo na nguvu zake kwako na muonee haya na soni kutokana na kuwa kwake karibu na wewe." Imam Swadiq as anasema kuwa: Nimetambua kwamba, Mwenyezi Mungu anafahamu kila kitu changu hivyo nikawa ni mwenye kuona na haya.
Mtume saw anasema: Waoneeni haya na soni wale ambao wanakuoneni, lakini nyinyi hamuwaoni.
Katika hadithi hizi kumeashiriwa juu ya kuzingatia usimamizi wa wale ambao wanayaona matendo ya mwanadamu yaani Mwenyezi Mungu na Malaika. Mafuhumu ya haya ni kupatikana hali fulani ya Mwislamu kuhisi soni na aibu mkabala na msimamiaji na muonaji; na haya na soni hii sababu yake ni woga na khofu ya mtu kwa Mwenyezi Mungu.
******
Kwa kuzingatia hadithi tulizotangulia kuzisoma inafahamika wazi hapa kwamba, moja ya mambo muhimu kabisa ya kujenga hali ya haya na soni ni kudiriki uwepo wa anayesimamia na kuyaona mambo yetu yaani Mwenyezi Mungu na Malaika wake. Ni kwa kuzingatia ukweli huu ndio maana utapata kuwa, kikawaida miamala na matendo ya watu mbele ya wengine na wakiwa peke yao yaani katika faragha yanatofautiana.
Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 108 ya Surat Nisaai:
"Wanataka kujificha kwa watu, wala hawataki kujificha kwa Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapopanga njama usiku kwa maneno asiyoyapenda. Na Mwenyezi Mungu anayajua vyema wanayoyatenda."
Abu Dhar al-Ghiffari ananukuu kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba, siku moja mbora huyo wa viumbe aliniambia: Ewe Abu Dhar je unapenda kuingia peponi? Nikamwambia, ndio ewe Mtume wa Allah. Akasema: Basi punguza tamaa na matarajio yako, daima kumbuka kifo na mauti na muonee haya Mwenyezi Mungu. Abu Dhar anaendelea kusimulia akisema: Nikwambia, Ewe Mtume wa Allah, mimi nina haya na soni kwa Allah... akasema: Haya kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kukumbuka kaburi na masaibu yake, kulichunga tumbo na vyakula na vinywaji vya haramu, kuyazuia macho, masikio na ulimi wako na mambo mabaya na yaliyokatazwa; kwani mtu ambaye anataka utukufu wa akhera anapaswa kusahau mapambo haramu ya dunia.
Aina nyingine ya haya na soni inayopendeza ni mtu kujionea haya yeye mwenyewe na dhamira yake na kuacha kufanya mambo ambayo ni kinyume cha sheria hata akiwa katika faragha. Kwa maana kwamba, mtu hata akiwa katika faragha na na yu peke yake anapaswa kujionea haya yeye na dhamira yake na kuacha kufanya mambo machafu.
Imam Ali bin Abi Twalib as anaitambulisha aina hii ya haya na soni kuwa ni bora kabisa na anasema: Haya na soni bora kabisa ni wewe kuona haya katika nafsi yako mwenyewe na kutopiga hatua kuelekea katika jambo baya.
Wapenzi wasikilizaji kwa hadithi hiyo ya Imam Ali bin Abi Twalib ndio tunakamilisha kipindi chetu cha leo cha Hadithi ya Uongofu kwa wiki hii. Tukutane tena juma lijalo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabakaatuh

 

 

 

Maandiko yanayofanana

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …