Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 30 Machi 2016 13:14

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (29) na sauti

Chanzo cha utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya (29) na sauti

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujumuika nami tena katika sehemu 29 ya kipindi kinachoangazia macho wimbi la makundi yanayowakufurisha Waislamu wengine na kutenda jinai za kutisha dhidi yao.

Katika kipindi kilichopita tulizungumzia ushirikiano wa karibu wa Uingereza na watawala wa Aal-Saiud dhidi ya Waislamu, tukabainisha kuwa, njama za Uingereza za kuwasaidia Mawahabi kuweza kudhibiti haram mbili takatifu za Makka na Madina, ambazo ndio turathi muhimu za Waislamu, London ilikuwa ikizingatia malengo yake ya baadaye katika kuvunja nguvu za Waislamu kama inavyoonekana hii leo. Ndugu wasikilizaji, katika historia yote ya Uislamu kundi pekee ambalo liliwakufurisha Waislamu wengine na kuhalalisha damu zao, lilikuwa kundi la wafuasi wa genge la Makhawaariji. Makhawariji ndio ambao waliamini kuwa, Mwislamu anayefanya dhambi kubwa, basi anakuwa kafiri na anahukumiwa kuuawa. Mbali na hayo baadhi ya Makhawariji walifikia kuamini kuwa, ukafiri wa baba, unasababisha pia ukafiri wa mtoto na mke, na hivyo kuhalalisha damu ya mtoto na mke kadhalika. Ni kwa kuzingatia kuwa, imani hiyo ni kinyume cha uhalisia wa mafundisho ya dini ya Kiislamu, ndipo Waislamu wote wakawatambua wafuasi wa genge hilo potofu kuwa ni Makhawariji yaani watu waliotoka katika Uislamu, suala ambalo lilipelekea kundi hilo kutoweka kabisa duniani. Mbali na Makhawariji kundi pekee ambalo limefuata mafundisho hayo ni genge la Uwahabi ambalo wafuasi wake wanajiona kuwa ni wao pekee wateule kwenye uso wa dunia na kuwaona wapinzani wa fikra zao kuwa ni makafiri wasiostahiki kuishi. Kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu unaowataka wafuasi wake kuamiliana na mtu mwenye fikra tofauti kwa aina ya upole, wao Mawahabi wanahalalisha damu na mali za wapinzani wao. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Waislamu wakawataja Mawahabi kuwa ni Makhawariji wa sasa. Kwa mfano tu Makhawariji walimtuhumu Imam Ali Bin Abi Twalib (as) kuwa alitenda dhambi kubwa kufuatia mtukufu huyo kuridhia suluhu ya majadiliano ambayo awali ni wao wenyewe Makhawariji ndio walimlazimisha Imam Ali kuyashiriki. Hatimaye wafuasi wa genge hilo wakamuua mtukufu huyo tarehe 21 mwezi wa Ramadhani akiwa anasali kwenye mihrab ya msikiti wa mji wa Kufa nchini Iraq. Hali ikiwa hivyo kwa Makhawariji, Mawahabi nao walimuua kiongozi wa Kisuni wa mji wa Uyainah baada ya kiongozi huyo kumaliza sala ya Ijumaa mjini hapo. Mawahabi walitekeleza jinai hiyo dhidi ya kiongozi huyo baada ya kumtuhumu shakhsia huyo kuwa ni kafiri. Hii leo pia, Mawahabi wanawaua katika maeneo tofauti ya dunia na kwa hujuma za kujiripua wanawake na watoto wa Kishia na Kisuni kwa kisingizioa kile kile cha kwamba, eti wamekufuru au wameritadi. Kwa hakika kile ambacho kimetawala mioyo ya watu wa genge hilo potofu ni utumiaji nguvu na mabavu katika kuwalazimisha watu wengine kufuata kundi hilo. Hii ni kusema kuwa, hakuna mahala popote katika historia ambapo kundi hilo lilienea bila ya watu wake kutumia mkono wa nguvu na umwagaji damu mkubwa. Ni kwa msingi huu, ndio maana watu wa kundi hilo wakaitwa kwa istilahi ya watu wa upanga na majahili.

*************************************

Historia ya vita na jinai za kundi la Uwahabi, inathibitisha ukweli huo. Aidha kwa kuangalia tu dhahiri ya genge hilo la Uwahabi, mbali na kuchunguza undani wake, inambainikia msomoaji kwamba, vita na mapambano yote ya wanachama wa kundi la Uwahabi si tu kwamba havikuwa dhidi ya maadui wa Uislamu, bali ni kwamba vilikuwa tu dhidi ya Waislamu, hususan wafuasi wa dhemehebu la Hanbali na Mashia. Kinyume chake, kile kilichochangia ongezeko na ustawi wa kundi hilo potofu la Kiwahabi, ni uungaji mkono wa wazi wa makafiri na maadui wakubwa wa dini ya Kiislamu. Ukweli ni kwamba malengo muhimu ya Mawahabi katika kufanya vita na mapambano yao makali dhidi ya Waislamu, si kuondoa bidaa au uzushi katika dini kama wanavyodai, bali ni kupora utajiri na mali za Waislamu kupitia kile wanachokitaja kuwa eti ni kueneza Tawhidi. Ukweli huo mbali na kutajwa na maadui wa kundi hilo, umetajwa pia na wataalamu wa historioa ya Kiwahabi kama vile Ibn Bushr na Ibn Ghanam, ambao wao wameweka wazi malengo ya genge hilo potofu katika Uislamu. Kwa mujibu wa wanahistoria hao, kila mahala ambapo Mawahabi  waliweka mguu, basi walifanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya wakazi wa eneo hilo, sanjari na kupora mali zao, huku wake na mabinti wa wahanga wa jinai hizo wakifanywa na wavamizi hao kuwa vijakazi. Aidha askari wa Kiwahabi kila eneo wanapofika, hupora hata kitu kidogo sana cha Waislamu miongoni mwa mali na utajiri, na hata wale wanaoachwa wakiwa hai, basi hufariki dunia kutokana na njaa kali. Kila mji au eneo ambalo watu wake walikataa mafundisho batili ya kundi la Uwahabi, basi walilazimishwa kulipa kodi ya fedha kwa mtawala wa Kiwahabi. Katika maeneo mengi watawala wa ukoo wa Aal-Saudi walikuwa hata wakitwaa nyumba na makazi ya wananchi kwa nguvu na mabavu. Kwa mfano tu, wakati Abdul-Azizi alipofungua mjia wa Riyadh hapo mwaka 1187 Hijiria, alitwaa nyumba na mitende yote ya mji huo na kujimilikisha yeye na watu wa ukoo wake hadi hii leo.

*********************************************

Ahmd Mustafa Abu Hakimah, mwandishi wa kitabu cha ‘Lam’ush-Shihab Fii Sirat Muhammad Ibn Abdul-Wahhab’ anaashiria idadi kubwa ya orodha ya vitu vilivyotwaliwa na Mawahabi kama ngawira. Ni kwa ajili hiyo na kwa mujibu wa watafiti wengi wa historia, lau kama si uvamizi na mabavu ya wanachama wa kundi hilo, kamwe Uwahabi usingeweza kusalia hai hadi hii leo. Mali na utajiri vilivyotwaliwa kwa mabavu kutoka mikononi mwa Waislamu, ndivyo vilivyostawisha maisha ya viongozi na watawala madhalimu wa Kiwahabi katika ukoo wa kidikteta wa Aal-Saud hadi leo. Ibn Bushr anaelezea hali ya mji mkuu wa Mawahabi wa ‘Diriyah’ baada ya kuanza linganio la Muhammad Ibn Abdul-Wahhabi katika kitabu chake cha ‘Unwaanul-Majdi Fii Taarikhin-Najdi’ kwamba: “Kabla ya kuanza linganio la Ibn Abdul-Wahhabi watu wa Diriyah walikuwa wakiishi maisha magumu na dhaifu mno. Hata hivyo baada ya hapo tuliuona mji wa Diriyah katika zama za Ibn Saud ukiwa umejaa mali na silaha za ajabu kiasi kwamba vitu hivyo havikupatikana katika mji mwengine wowote ule. Aidha mji huo ulipambwa na mawe ya thamani, farasi wa bei, matukufu yote ya Kiarabu, nguo za fakhari na kila kitu kinachotambuliwa na mwanadamu kuwa cha thamani.” Ibn Bushr anaendelea kwa kusema kuwa: “Siku moja nilikuwa nimesimama katika eneo la muinuko lililoitwa Batin katika mji wa Diriyah. Upande wa magharibi wa mji huo kulikuwa na kasri za ukoo wa Aal Saud zililoitwa kwa jina la Twarif huku upande wa mashariki kukiwa na kasri za watoto wa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab, maarufu kwa jina la Aal-Sheikh na zilizoitwa kwa jina la Bajiri.” Mwisho wa kunukuu. Kwa mujibu wa mwanahistoria hiyo Ibn Bushr, theluthi moja ya mali zilizokuwa zikitoka eneo la al-Ahsaa, zilikuwa ni kwa ajili ya ukoo wa Ibn Saud na ukoo wa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab. Aidha mfalme wa Saudia alijenga kasri na kutenga ndani yake vyumba vingi ambavyo kila kimoja alimuweka mwanamke na watumishi wake maalumu wanaomfanyia kazi. Mara nyingi nguo za wake wa mfalme  huyo zilitokana na hariri kutoka India ambazo pia zilikuwa zimepambwa kwa dhahabu nyekundu au kijani. Au walivaa mavazi ya hariri ambayo mapambo yake yalitokana na dhahabu ya aina yoyote. Wapishi mahiri kutoka mji wa al-Ahsaa, walikuwa wakiwaletea chakula cha kila aina. Katika harusi moja pekee ya mwanamfalme wa ukoo wa al-Saud kulichinjwa ngamia 140. Muhammad Ibn Abdul-Wahhab naye alikuwa na hali nzuri ya kimaisha zaidi hata ya Ibn Saud mwenyewe. Hii ni kwa kuwa Ibn Abdul Wahhab alikuwa anapenda sana wanawake na katika umri wake alioa wake 20 ambao walizaa watoto 18. Kwa mujibu wa mwandishi wa historia wa kitabu cha ‘Lam’ush-Shihaab’ Ibn Abdul-Wahhb na kizazi chake, walikuwa na ardhi pana sana. Mbali na hayo walikuwa na fungu maalumu katika baytul-mali ambapo watawala wa maeneo tofauti kutoka ukoo wa Aal-Saud walikuwa wakituma hadaya na zawadi za thamani kwa ajili yao. Kwa hakika watoto wa Muhammad Ibn Abdul-Wahhab ambao hii leo wanaoitwa Aal Sheikh waliishi maisha ya starehe ya hali ya juu kutokana na mali za Waislamu wengine walizozipora kupitia fatwa za kuwakufurisha na kuhalalisha damu na mali zao. Hali hiyo iliendelea hata kwa vipindi vya baadaye. Kwa kipindi fulani ukoo wa Aal Saud ulikabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wasomi na weledi wa masuala ya kijamii nchini Saudia. Kwa kuzingatia hali hiyo watu wa ukoo wa Aal-Sheikh (watoto wa Ibn Abdul-Wahhabi) si tu kwamba walikabiliana na hali hiyo, bali pia walisimama kuwatetea kwa nguvu zao zote watu wa ukoo wa Aal-Saud sanjari na kuhalalisha ufisadi wa watawala hao.

Wapenzi wasikilizaji kipindi chetu cha makala yanayoangazia macho wimbi la utakfiri katika ulimwengu wa Kiislamu sehemu ya 30, kinakomea hapa kwa leo, tutakutana tena wiki ijayo panapo majaali ya Allah. Mimi ni Sudi Jafar Shaban, basi hadi wakati huo nakuageni kwa kusema, kwaherini.

Sauti na Video

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …