Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 17 Mei 2015 16:51

Hadithi ya Uongofu (4)

Hadithi ya Uongofu (4)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibu katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Sehemu iliyopita ya kipindi hiki ilijadili umuhimu wa kufanya dhikr na kumtaja Mwenyezi Mungu na jinsi jambo hili lilivyo na tathira katika maisha yetu ya kila siku. Aidha tulisema katika kipindi chetu kilichopita kwamba, kumtaja, kumdhukuru na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni upepo mwanana ambao huleta upya na nishati katika roho ya mwanadamu. Moyo wa mwanadamu hupata nishati na nguvu kwa kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na huufanya moyo kuwa na hali ya utulivu katika patashika, kwenye matatizo na mazonge maishani.

Kumdhukuru Allah humfanya mja apate uhakika na utulivu wa moyo. Juma hili kipindi chetu hiki ambacho ni sehemu ya nne ya mfululizo huu, kitazungumzia faida na athari za kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Hatua ya mwanadamu ya kumzingatia Mwenyezi Mungu na kuwa na mafungamano na chanzo kisichokwisha cha nguvu Zake, huwa na taathira chanya katika maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu analitambua suala la kumtaja yeye kwamba, linapelekea nyoyo kupata nuru.  Jambo hilo limeashiriwa katika aya ya 210 ya Surat al-A’raf:

“Hakika wale wamchao Mungu, zinapo wagusa pepesi za Shet'ani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki.”

Kadiri moyo wa mwanadamu utakavyokuwa ukimtaja Mwenyezi Mungu, basi ni kwa kiwango hicho hicho moyo huo hung’arishwa kwa nuru ya Mwenyezi Mungu.  Kimsingi ni kuwa kuna mfungamano wa pande mbili.

Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 152 ya Surat al-Baqara kwamba: “Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru.”  Yaani kadiri mtu atakavyomkumbuka na kumtaja Mwenyezi Mungu kimaneno, kifikra na kivitendo basi huwa na thamani na umuhimu zaidi mbele ya Mola Muumba. Mtu wa namna hii huwa na nuru ya Mwenyezi Mungu katika ujudi na uwepo wake na hivyo nuru hiyo kummulikia na kumuangazia njia ya maisha yake suala ambalo humfanya afikie katika uongofu na kufaulu.

Suala la kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu halina zama na sehemu maalumu kama ambavyo halina pia kiwango maalumu. Kwa msingi huo basi, daima mwanadamu anapaswa kuhuisha uwepo wa Mwenyezi aliyeumba ulimwengu huu.  Aya ya 103 katika Surat an-Nisaa inasema:

“Mkisha sali basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu mkisimama, na mkikaa, na mnapo jinyoosha kwa kulala.”

Kupitia aya hiyo tukufu tunafahamu kwamba, mja hapaswi kudhani kwamba, akiwa katika Sala tu, basi hiyo ndio moja ya misdaqi muhimu  ya dhikri na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, la hasha, bali mwanadamu anapaswa kumzingatia na kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika lahadha na wakati wote wa maisha na ahisi kwamba, uwepo wa Mola Muumba upo na ni wenye kuhitajika wakati wote. Kwa maana kwamba, mwanadamu anapaswa kumkumbuka na kumtaja Allah wakati wowote, mahala popote na hapaswi kughafilika na hilo hata kidogo. Kama tulivyoashiria hapo awali kwamba, endapo mja atamkumbuka Mwenyezi Mungu, bila shaka Mola Muumba naye humkumba.

Mwenyezi Mungu ameashiria jambo hilo katika aya ya 152 ya Surat al-Baqarah kwamba:

“Basi nikumbukeni nitakukumbukeni, na nishukuruni wala msinikufuru”.

Imam Ali bin Abi Talib anaiashiria nukta hii katika wasia wake kwa mwanawe Hassan al-Mujtaba AS anaposema: Mtaje Mwenyezi Mungu katika kila hali.

Imenukuliwa katika hadithi kwamba, siku moja Bwana Mtume SAW aliwauliza maswahaba zake, kwa kuwaambia, je nikujulisheni kazi ambayo ni bora kabisa kidaraja kwenu, na ambayo inakukurubisheni zaidi kwa Mwenyezi Mungu na ambayo inakutakaseni, kazi ambayo ni bora kuliko pesa, dhahabu na fedha na ambayo ni nzuri zaidi ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Maswaha wakamwambia, tulijishe ewe Mtume wa Mwenyezi.

Mtume SAW akasema, kazi hiyo ni kumtaja sana Mwenyezi Mungu.”

Mbali na kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu kuwa ni jambo bora, bali hata vikao na mahafali ambazo ndani yake kunaandaliwa uwanja na mazingira ya kumtaja Mwenyezi Mungu navyo vina itibari na thamani maalumu. Kila kikao ambacho ndani yake kinaifanya roho na moyo kumzingatia na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, na ndani yake kunatajwa sifa za Mwenyezi Mungu, sio tu kwamba, huzingatiwa na waja wema na wasafi, bali Mola Muumba pia hukizingatia kikao kama hicho.

Mtume SAW amesema: Hakuna kundi la watu ambalo linajishughulisha na kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu isipokuwa Malaika huwa miongoni mwao na rehma za Mwenyezi Mungu huwa pamoja nao.

Aidha katika sehemu nyingine Mtume SAW amenukuliwa akibainisha umuhimu wa vikao vinavyomtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu akisema: Wakati wowote mtakapoyakuta mabustani ya peponi, basi yafanyeni kuwa sehemu yenu ya matembezi. Akaulizwa, ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni yepi hayo mabustani ya peponi? Akasema, vikao vinavyomtaja Mwenyezi Mungu.”

Maneno haya ya Bwana Mtume SAW yanabainisha nukta muhimu ya kimalezi na taathira muhimu viliyonayo vikao stahiki katika kumfanya mwanadamu aelekee katika ukamilifu. Watu wa kawaida katika hali ya kawaida huwa hawana raghba na hamu sana ya kutekeleza baadhi ya shaari na marasimu za kiibada, lakini pindi wanapokuwa na watu wengine hupata nguvu, hamu na nishati ya kutekeleza hayo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Bwana Mtume SAW anasema kuwa, kushiriii katika vikao vinavyomtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu au kila kikao na majlisi ambayo inafanyika kwa ajili ya kuhuisha nara na shaari za kidini huwa sawa na kuingia katika mabustani ya peponi. Kisha Mtume SAW anaongeza kwa kusema:

Mtu ambaye ana hamu ya kutaka kufahamu daraja yake mbele ya Mwenyezi Mungu basi na atizame daraja ya Mwenyezi Mungu kwake ikoje.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa msisite kujiunga nami katika kipindi kingine cha mfululizo huu wiki ijayo.

Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …