Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 10 Mei 2015 15:06

Hadithi ya Uongofu (3)

Hadithi ya Uongofu (3)

Ni matumaini yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Kipindi chetu kilichopita kilijadili na kuzungumzia suala la kujitambua na jinsi suala hilo linavyomsaidia mtu kumtambua Mwenyezi Mungu. Aidha tuliashiria umhimu wa kujitambua pamoja na madhara ya mtu kutojitambua. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya tatu, tutazungumzia maudhui ya “kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu”. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Kumtaja, kumdhukuru na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni upepo mwanana ambao huletwa upya katika roho ya mwanadamu. Moyo wa mwanadamu hupata nishati na nguvu kwa kumtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na huufanya moyo kuwa na hali ya utulivu katika patashika, kwenye matatizo na mazonge. Kumdhukuru Allah humfanya mja apate uhakika na utulivu wa moyo. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 28 ya Surat Ra’ad kwamba:

“Wale walio amini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hakika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndio nyoyo hutua!”

Kuondolewa matatizo na mazonge ni jambo ambalo linafungamana na kumtaja na kumdhukuru Allah na kuacha jambo hili muhimu, humzuia mwanadamu kufikia katika lengo kuu katika ulimwengu huu na mwisho wa umri wake huwa hana jingine ghairi ya kujuta. Mwanadamu huyu hujuta kutokana na siku zilizompita ambazo angeweza kufanya jambo fulani la kheri lakini hakufanya. Hata hivyo majuto ni mjukuu kwani masiku yaliyopita si yenye kurejea tena.

Dhikr maana yake ni kutaja na kukumbuka. Kumdhukuru, kumkumbuka na kumtaja Allah kuna hatua na daraja zake ambapo hatua na daraja ya kwanza ni kumkumbuka Allah kwa kwa maneno na ulimi. Tab’ani, tunapaswa kuzingatia nukta hii kwamba, madhumuni ya kumtaja Allah ambako kunapelekea kupatikana utulivu wa nyoyo, ni kudhukuru ambako mwenye kufanya hivyo anapaswa kufahamu maana yake. Kinyume na hivyo, mara nyingi utamuona mtu anafanya dhikr na kumtaja Mwenyezi Mungu, lakini kitendo chake hicho sio tu kwamba, hakiendani na utajo na dhikr hiyo bali ni kinyume kabisa.

Kisha Imam Jaafar Sadiq as mmoja wa wajukuu wa Bwana Mtume saw anasisitiza kwa kusema: Tambueni kwamba, makusudio yangu sio kusema

سبحان الله والحمدلله و لا اله الا الله والله اکبر

Licha ya kuwa kufanya hivyo pia ni kumtaja na kudhukuru Allah, lakini makusudio yangu ni kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu katika halali na haramu ya Mwenyezi Mungu, ambapo kama Allah ameamrisha kufanya jambo fulani basi mja alifanye na kama kufanya jambo hilo ni haramu, dhambi na maasi aepukane nalo.”

Daraja nyingine ni kufanya dhikri na kumtaja Allah kwa moyo. Kwa maana kwamba, mja amzingatie Allah kwa moyo ambapo wakati mwingi matunda ya kitendo hiki huonekana kwa kufanya dhikri kwa ulimi. Hata hivyo daraja ya juu kabisa ya kumtaja Mwenyezi Mungu ni ile ambayo inafanywa na waja maalumu na wenye ikhlasi wa Mwenyezi Mungu ambao hushuhudia uwepo wa Mwenyezi Mungu katika lahdha zao zote za maisha. Waja wa namna hii hujihesabu kuwa wamepata dhambi hata katika lahadha ambayo wameghafilika na Mwenyezi Mungu. Hii hii hali ya kuzingatia uwepo wa Mwenyezi Mungu humfanya mtu kufanya amali njema na kuwa ni kizingiti imara baina ya mtu na dhambi. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana Imam Ali bin Abi Talib as anasema kuhusiana na suala hili kwamba: “Kumtaja Mwenyezi Mungu ni nguzo ya imani na kinga ya vishawishi vya shetani.”

Aidha anasema: Daima mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwani hiyo ni dhikri bora kabisa.

Kwa hakika kutokana na kuwa, sababu zinazopelekea mtu kughafilika na kukumbwa na mghafala ni nyingi mno katika maisha ya kimaada na vishawishi vya shetani vimemzingira mwanadamu huyu kutoka kila upande, ili kujiokoa, njia bora kabisa ni kuomba hifadhi kwa Mwenyezi Mungu, kumtaja na kumkumbuka Muumba.

Hata hivyo tunapaswa kutambua kwamba, kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni kufanya kila kazi na amali njema, iwe ni katika kumuabudu mwenyezi Mungu au katika uwanja wa kutoa huduma kwa wanadamu.

Imepokewa hadithi kutoka kwa Bwana Mtume saw ya kwamba amesema:  Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu amemtaja na kumdhukuru Muumba hata kama Sala, funga na kusoma kwake Qur’ani ni kidogo; na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu amemsahau Muumba, hata kama Sala, funga na kusoma kwake Qur’ani kutakuwa ni kwingi.”

Katika hadithi hii Bwana Mtume saw anabainisha kwamba, mtu ambaye anamtii Mwenyezi Mungu kimsingi amemtaja na kumkumbuka Mola Muumba hata kama ibada zake zitakuwa chache. Na mtu ambaye amemuasi Mola Muumba, kimsingi amemsahau Allah hata kama atakuwa mwingi wa ibada.

Imam Jafar Sadiq as amesema: Kila kitu kina mpaka ambapo mtu anapofikia hapo huwa ndio mwisho wake, isipokuwa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu, hili halina mpaka. Mwenyezi Mungu Mtukufu amezifanya faradhi kuwa wajibu na kila mwenye kuzitekeleza huo ndio mpaka na mwisho wake. Moja ya faradhi hizo ni mwezi wa Ramadhani ambapo mwisho wa funga ya mwezi huo wa Ramadhani ni Sikukuu ya eidul Fitr. Mwenyezi Mungu amefaradhisha ibada ya Hija na kila mwenye kuhiji amefikisha mwisho wa faradhi hiyo, lakini kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu pekee ambako Allah hakuridhika na udogo wake na hivyo hakuliwekea mpaka na mwisho jambo hilo.”

Kisha akasoma aya za 41 na 42 za Surat al-Ah’zab zinazosema kwamba:

“Enyi mlio amini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru. Na mtakaseni asubuhi na jioni.” Kisha akasema, Mwenyezin Mungu hajaweka mpaka wa kumtaja hata jambo hilo liwe na mwisho. Baba yangu Imam Muhammad Baqir (as) alikuwa akimtaja mno Mwenyezi Mungu, mimi nilikuwa nikienda pamoja naye na yeye alikuwa akimtaja na kumdhukuru Allah, nilikuwa nikila pamoja naye na yeye akimtaja na kumdhukuru Mwenyezi Mungu na hata alipokuwa akizungumza na watu hakuacha hata lahadha moja kumtaja Mwenyezi Mungu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi chetu kwa leo umefikia tamati tukutane tena wiki ijayo. Kwaherini.

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …