Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 03 Mei 2015 18:43

Hadithi ya Uongofu (2)

Hadithi ya Uongofu (2)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. Katika sehemu ya kwanza ya kipindi hiki tulibainisha mambo jumla kuhusiana na hadithi, nafasi na umuhimu wake na kwamba, hadithi ni chanzo na marejeo ya pili ya Waislamu baada ya Qur’ani Tukufu. Tulisema kuwa, kuna hadithi nyingi zilizopokewa kutoka kwa Bwana Mtume saw na Maimamu watoharifu as, ambazo ni taa na muongozo kwetu katika masuala mbalimbali ya kiitikadi, kisiasa, kijamii na kadhalika. Katika sehemu hii ya pili ya mfululizo huu tutazungumzi suala la “kujitambua” na jinsi jambo hili lilivyokuiwa na umuhimu katika Uislamu na kutaja baadhi ya hadithi zinazozungumzi maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Watu wengi hufanya safari na kuelekea katika misitu, milima na maeneo mbalimbali kwa shabaha ya kwenda kujionea mandhari nzuri za miti, majani, milima mito, mabonde na kadhalika. Safari hizo za utalii wakati mwingine huwagharimu watu fedha nyingi na kuwachukulia muda wao mwingi. Hata hivyo utalii bora zaidi ni mtu kufanya safari ndani ya nafsi yake na kuona siri za kuwepo kwake. Kwa hakika kufanya hivi kuna umuhimu mkubwa kwa ajili ya kujitambua kuliko mtu kujielewa kupitia kutambua siri za ulimwengu na vilivyomo ulimwengunio. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 20 na 21 za Surat Ad-Dhaariyaat kwamba: “Na katika ardhi zipo Ishara kwa wenye yakini, Na pia katika nafsi zenu - Je! Hamwoni?

Kwa msingi huo basi kando ya kuutambua ulimwengu, maarifa muhimu zaidi ni mtu kujitambua mwenyewe.

Kwa hakika mtu kujitambua ni utangulizi wa kumtambua Mwenyezi Mungu. Imam Ali bin Abi Talib anasema: Nastaajabishwa na mtu ambaye hajitambui, vipi atamtambua Muumba wake.” Aidha Imam Ali as anasema: “Mwenye kuitambua nafsi yake amemtambua Mola wake.”

Kutokana na kuwa fitra na maumbile ya mwanadamu yamechanganyika na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu, wito wa kujitambua kwa hakika ni da’awa na ulinganiaji wa kumtambua Mwenyezi Mungu na kuwa na uhusiano na Mola Muumba. Imam Ali bin Abi Talib as anasema kuhusiana na hili kwamba: “Ewe Mola! Umezinawirisha na kuzifungamanisha nyoyo na mapenzi yako na umezifungamanisha akili na maarifa yako.”

Kwa hakika kujitambua huwa sababu na chimbuko la kuwa na mapenzi juu ya Mwenyezi Mungu na kumtambua Mola Muumba wa ulimwengu na vilivyomo. Hii ni kutokana na kuwa, uwepo wa mwanadamu ni uwepo ambao unafungamana na Mwenyezi Mungu na bila shaka kiumbe huyu hawezi kuwa amejiumba. Kwa mukatdha huo, mwanadamu anapojihusisha na suala la kujitambua huhisi kuwa na mfungamano na utegemezi kwa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 15 ya Surat Faatir: “Enyi watu! Nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.”

Wapenzi wasikilizaji, endapo mtu atajitambua yeye kabla ya kitu kingine chochote, ataweza kunufaika vizuri na mtaji wa uwepo wake na kuvifanya vipaji alivyonavyo vichanue, kwani nukta ya kuanza kujitambua ni kutambua mtaji wa uwepo wa mwanadamu. Mwanadamu akijitambua na kuwa na maarifa, huwa amejifungulia dirisha la mwanga na kwa kuona vikwazo na vizingiti vilivyoko katika njia ya kujitambua, huwa amepata njia kubwa kabisa ya kujiokoa.  Imam Ali bin Abi Talib (as) anasema:

Kila mwenye kuitambua nafsi yake, husimama kwa ajili ya kupigana nayo jihadi na kila ambaye hajaitambua (nafsi yake) basi huitelekeza.’

Kwa msingi huo, mtu ambaye hajajitambua na kujifahamu hawezi kuainisha mambo ambayo ni sababu ya yeye kufikia ukamilifu au chanzo cha yeye kuporomoka na kuangamia. Mtu wa aina hii, taratibu hugeuka na kuwa mtumwa wa shetani na mja mwenye kuabudu matamanio na hawaa za nafsi. Matokeo yake ladha za shetani huja na kuchukua mahala pa ladha za kiakili na kimaanawi na hivyo kivitendo huwa ni mwenye kumuabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu.

Imam Ali as anasema: Arif ni mtu mwenye kujitambua na akajiokoa kutoka katika minyororo ya ushawishi wa shetani na nafsi inayoamrisha maovu na kujisafisha na kila ambacho kinamuweka mbali na Mwenyezi Mungu na ambacho kinapelekea kuangamikia kwake.

Mwanadamu kupitia kujitambua, huweza kufahamu utukufu wa nafsi na adhama ya uumbaji huu mkubwa wa Mwenyezi Mungu na hudiriki kwamba, johari hii yenye thamani haipaswi kuikosa kirahisi rahisi. Sisitizo la dini Tukufu ya Kiislamu juu ya suala la kujitambua ni kumtaka mwanadamu atambue kile kilichoko na kudiriki daraja na nafasi yake katika ulimwengu wa ujudi na uwepo. Lengo la utambuzi huu ni yeye kujisogeza na kufikia daraja za juu anazostahiki.

Dini tukufu ya Uislamu inamtambua mwanadamu kuwa ni kiumbe ambaye mbali na kuwa na umbo na mwili wa kimaada, anayo roho na nafsi isiyo ya kimaada. Kimsingi ni kuwa, asili ya mwanadamu ni nafsi na roho aliyonayo, na kwamba, mwili ni wenzo tu kwa ajili ya kukua na kufikia ukamilifu wa mwadamu ambao umepatiwa roho. Kwa maana kwamba, roho inautumia mwili kwa ajili ya kufikia daraja ya ukamilifu. Kuna wakati kutokana na kughafilika, mwanadamu huacha kuzingatia asili yake, na badala yake huzingatia zaidi mwili, matakwa na matamanio yake. Kwa hakika mghafala huu ni kizingiti cha mwanadamu huyu kufikia katika ukamilifu wa kweli. Hii ni kutokana na kuwa, madhali mwanadamu angali katika usingizi wa mghafala na kughafilika, basi hawezi kufanya harakati kwa ajili ya kuelekea katika ukamilifu na saada yake. Imam Ali bin Abi Talib as, ambaye ni wasii na kiongozi wa Waislamu baada ya Mtume saw amenukuliwa akisema kuwa, “Usiwe jahili na mjinga wa nafsi yako, kwani asiyeitambua nafsi yake kwa hakika ni jahili na mjinga wa kitu kitu.”

Wapenzi wasikilizaji kiopindi chetu cha leo kinafikia tamati hapa ambapo kwa mukhtasari leo tulizungumzia kujitambua na umuhimu wake pamoja na madhara ya mtu kutojitambua. Aidha umebainisha kwamba, kujitambua ni hatua ya kuelekea kumtambua Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo.

Basi hadi tutakapokutana tena wiki ijayo ninakuegeni huku nikitaraji kwamba, mtajiunga nami katika sehemu nyingine ya mfululizo huu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi wabarakaatuh…

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …