Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 23 Septemba 2015 12:30

Ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu 1436 Hijria

Ujumbe wa Hija wa Kiongozi Muadhamu 1436 Hijria

Bismillahir Rahmanir Rahim


Na hamdu na shukrani zote zinamstahikia Allah, Mola Mlezi wa viumbe wote na rehema na amani ziwe juu ya Bwana wa viumbe wote Muhammad na Aali zake watoharifu na masahaba zake wateule na wote wanaowafuata kwa wema hadi Siku ya Kiyama.
Na amani iwe juu ya al Kaaba tukufu, kitovu cha tawhidi na mahali pa kutufu waumini na sehemu wanaposhuka malaika. Na amani kwa Masjidul Haram na Arafa na Mash'ar na Mina na amani kwa nyoyo zenye unyenyekevu na ndimi zinazomdhukuru na kumtaja Mwenyezi Mungu na macho yaliyofunguliwa na yanayoangalia mbali, na fikra zilizotambua njia yake, na amani iwe juu yenu mliopata bahati ya kutekeleza ibada ya Hija ambao mumepata taufiki ya kuitikia labeka mwito wa Mola wenu na kufanikiwa kukaa kwenye kitanga hicho kilichojaa neema.
Jukumu la kwanza kabisa ni kuizingatia labeka hiyo ya kimataifa, ya kihistoria na ya milele inayosema: انّ الحمد و النعمة لک و المُلک، لا شَریک لک لبیک. Hakika ya hamdu na shukrani na neema ni Zako Wewe tu Mwenyezi Mungu na ufalme, huna mshirika, labeka. Huu ndio mtazamo ambao hujaji anaupata katika hatua ya mwanzo kabisa ya kutekeleza amali hiyo iliyojaa maana na mambo mengi ndani yake, na kila anapoendelea kutekeleza ibada hiyo tukufu ndivyo hupata fursa ya kujiunganisha zaidi na amali hiyo na hatimaye hupata mafunzo ya kudumu na somo lisilosahaulika na kutakiwa kupangilia maisha yake kwa kuzingatia somo na mafunzo aliyoyapata kwenye amali hiyo. Kuweza kujifunza somo hilo kubwa na kulifanyia kazi ndiyo chemchemu iliyojaa baraka ambayo inaweza kuyaletea ufanisi maisha ya Waislamu na kuwafanya waishi katika maisha bora kabisa na kuwakomboa kutoka katika matatizo ambayo wanakumbana nayo katika kipindi cha hivi sasa na kwenye vipindi vyote vingine. Sanamu la ubinafsi, kiburi na tamaa na hawa za nafsi, sanamu la kupenda kufanya ubeberu na kukubali kufanyiwa ubeberu, sanamu la uistikbari wa kimataifa, sanamu la uvivu na kutojali majukumu na masanamu mengine yote yanayoangamiza roho ya heshima ya mwanadamu yanaweza kuvunjwa kwa mwangwi huo wa Kiibrahim iwapo utatoka ndani kabisa ya moyo na kuwa ndiyo ratiba ya maisha ya Waislamu na hatimaye mahala pa kuwa kibaraka na kuwa na matatizo na mashaka ya dunia patachukuliwa na ukombozi, heshima na amani.
Makaka na madada mahujaji kutoka kila taifa na nchi, zingatieni neno hilo lenye hekima nyingi na yaangalieni kwa mazingatio matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu hususan katika eneo la magharibi mwa Asia na kaskazini mwa Afrika na mutekeleze majukumu yenu kuhusiana na mambo hayo kwa kila mmoja kuzingatia uwezo na nafasi yake.
Leo hii siasa zilizojaa shari za Marekani katika eneo hili ambazo ndilo chimbuko la vita na umwagaji wa damu na uharibifu na watu kuwa wakimbizi na vile vile umaskini na kubakia nyuma kimaendeleo na hitilafu na mizozo ya kikaumu na kimadhehebu, kwa upande mmoja, na jinai za utawala wa Kizayuni ambao vitendo vyake vya uporaji katika nchi ya Palestina vimefikia kiwango cha juu cha ukatili na uafiriti na kuvunjiwa heshima mara kwa mara eneo takatifu la Masjidul Aqsa na kupigwa teke roho na mali za Wapalestina wanaodhulumiwa, kwa upande mwengine, ndilo suala lenu kuu na la kwanza kabisa nyote Waislamu na kuna wajibu wa kulizingatia vilivyo suala hilo na kutekeleza majukumu yenu ya Kiislamu kuhusiana na jambo hilo. Na maulamaa wa kidini na watu wenye vipawa na ushawishi wa kisiasa na kiutamaduni wana jukumu zito sana ambalo kwa bahati mbaya wengi wao wanasahau jukumu lao hilo.
Badala ya maulamaa wa kidini kuchochea moto wa mizozo na hitilafu za kimadhehebu, na badala ya wanasiasa kuchukua maamuzi wa pupa kuhusu maadui, na badala ya watu muhimu katika masuala ya kiutamaduni kushughulishwa na mambo ya pembeni yasiyo na maana, wanapaswa kukitambua kilio kikubwa cha ulimwengu wa Kiislamu na watekeleze ipasavyo jukumu lao ambalo watakwenda kuulizwa mbele ya uadilifu wa Mwenyezi Mungu, na wahakikishe wanalitekeleza kiufanisi. Matukio ya kuliza yanayoendelea hivi sasa katika eneo hili, huko Iraq na Sham na Yemen na Bahrain na katika Ukingo wa Magharibi na Ghaza na kwenye nchi nyingine za Asia na Afrika, ni matatizo makubwa yaliyoukumba umma wa Kiislamu hivi sasa na inabidi kuuona vizuri mkono wa njama za ubeberu wa kimataifa katika mambo hayo na kufikiria njia za kuyatatua. Wananchi wanapaswa kuzitaka tawala na serikali zao kutekeleza jukumu hilo, tawala hizo nazo zinapaswa kuwa waaminifu na kutekeleza ipasavyo jukumu lao.
Na Hija na mikusanyiko yake mikubwa ya Waislamu, ni mahala bora zaidi pa kujitokeza na kukabidhiana jukumu hilo la kihistoria.
Na fursa ya kujibari na washirikina ambapo inabidi mahujaji wote kutoka kila mahala waitumie vizuri fursa hiyo, ni moja ya amali muhimu kabisa ya kisiasa katika ibada hiyo iliyokusanya mambo yote.
Amma tukio chungu lililosababisha hasara katika Masjidul Haram mwaka huu limewahuzunisha sana mahujaji na mataifa ya mahujaji hao. Ni sawa kwamba waliotangulia mbele ya Haki katika tukio hilo walikuwa katika hali ya kusali na kutufu na kufanya ibada na hivyo wamepata mafanikio makubwa ya kurejea kwa Mola wao wakiwa katika ibada na Inshaallah watapata usalama na amani na rehema za Mwenyezi Mungu, na ijapokuwa hiyo ni faraja kubwa kwa wafiwa, lakini hilo halipunguzi uzito wa jukumu na mas'uliya ya waliopewa kazi ya kulinda usalama wa wageni hao wa Mwingi wa rehema. Sisitizo letu kuu na lisilotetereka ni kuwataka wahusika wote watekeleze vilivyo jukumu lao katika suala hilo.
Na amani iwe juu ya waja wa Allah walio wema.


Sayyid Ali Khamenei
4 Mfunguo Tatu, Dhulhija 1436
27 Shahrivar 1394 Hijria Shamsia

Zaidi katika kategoria hii: « Dondoo za Hija (10)

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …