Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 20 Septemba 2015 12:27

Safari ya kuelekea kwenye ardhi ya wahyi

Safari ya kuelekea kwenye ardhi ya wahyi

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Tumo katika siku za mwanzoni mwa mwezi mtukufu wa Mfunguo Tatu Dhulhija. Hiki ni kipindi cha ibada ya Hija ambamo miji miwili mitakatifu ya Makka na Madina hushuhudia picha nzuri na za kuvutia.
Hija ni maonyesho ya mahudhurio ya mamia ya maelfu ya watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu Mmoja na mfano mdogo wa jamii wa kitauhidi. Ni maonyesho makubwa ya wanadamu wampwekeshao Mwenyezi Mungu wanaokutana katika eneo moja takatifu kuonesha mshikamano wa Umma mmoja wa Kiislamu chini ya bendera ya Tauhidi, mithili na mito inayomwaga maji na kukutana katika bahari moja kubwa. Imam Ali bin Abi Twalib (as) anatoa picha ya mandhari hiyo ya Umma mkubwa wa Waislamu katika ibada ya Hija kwa kusema: Waislamu wanakimbilia al Kaaba mithili ya watu wenye kiu wanaokwenda mbio kueleka kwenye chemchemi ya maji.... na wanasimama katika eneo walikosimama mitume wa Mwenyezi Mungu kuzunguka nyumba tukufu ya al Kaaba mithili ya Malaika wazungukavyo arshi ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji hao wanafaidika katika soko la ibada na kukimbilia katika miiadi ya kusamehewa dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ameifanya al Kaaba kuwa nembo ya Uislamu na nyumba na amani na salama kwa ajili ya waja wake wanaokimbilia amani na usalama", mwisho wa kunukuu.
Kwa kuwa mambo yote ya dunia hii yanadhibitiwa na Mwenyezi Mungu Mwenye hikima, hapana shaka kuwa kila kitu duniani kimetengenezwa kwa msingi wa hikima na falsafa makhsusi. Vivyo hivyo sheria na mafundisho ya dini yamejaaliwa kwa namna ambayo yanamwelekeza mwanadamu katika njia ya ukamilifu. Tunaweza kusema kwamba mafundisho yote ya dini yanatayarisha uwanja mzuri wa kustawi kiroho kiumbe mwanadamu na kumuweka mbali na mghafala na kusahau asili na marejeo yake.
Kwa mujibu wa aya za Qur'ani Tukufu, falsafa ya kuumbwa wanadamu ni kufanya ibada. Ibada inaimarisha uhusiano wa mwanadamu na Mola Muumba na kuwa na taathira kubwa katika ustawi wa kiroho na kimaanawi wa kiumbe huyo. Hija ni miongoni mwa ibada zinazomwelekeza zaidi mwanadamu katika thamani za kiroho na kumhamasisha kukata mahusiano na mifungamano yake ya kimaada na ulimwengu duni na wa chini. Ibada ya Hija inamuweka mwanadamu katika mabadiliko makubwa ya kiroho lakini mabadiliko hayo ya ndani ya nafsi na kujitenga na umimi, mapambo ya dunia na kadhalika hayafanyiki katika hali ya kujitenga, bali katika mshikamano na mkusanyiko wa umma wa mahujaji. Kwa utaratibu huo haji hujihisi kuwa na aina fulani ya mshikamano na mfungamano na mahujaji wenzake.
Ibada na amali za Hija kwa upande mwingine ni ibra na darsa kuhusu maisha ya shakhsia adhimu kama Nabii Ibrahim, Ismail na Hajar. Nabii Ibrahim (as) alijisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu na kuondoa moyoni mwake mfungamano mkubwa na wenye nguvu zaidi wa kidunia nao ni mfungamano wa baba na mwanaye. Kwa maneno mengine ni kuwa, Nabii Ibrahim aliamua kumchinja mwanaye pale alipoamrishwa na Mwenyezi Mungu ikiwa ishara ya kuchinja na kukata kabisa mahusiano na mifungamano yake ya kidunia katika njia ya Mwenyezi Mungu. Mahujaji waliokwenda kuzuru Nyumba ya Mwenyezi Mungu, al Kaaba, wanaiga na kufuata nyayo za Nabii huyo mkubwa wa Allah SW. Kwa hakika kujitenga na kukata uhusiano na kila kitu ghairi ya Yeye SW kunasawazisha na kutengeneza vizuri njia ya kuelekea kwa Mola Muumba. Kwa msingi huo iwapo haji na mtu aliyekwenda kuzuru Nyumba ya Allah atafanikiwa kukata na kujiweka mbali na mivuto mingine yote katika roho yake basi kwa hakika atakuwa amekurubia zaidi katika maana ya Hija mabruri.


>


Amali za Hija zimepangwa kwa namna ambayo zinaleta mabadiliko katika nafsi ya mahujaji hatua kwa hatua. Kwanza kabisa haji hujitenga na mavazi maridadi na yenye rangi mbalimbali na kuvaa vazi la rangi nyeupe linalojulikana kwa jina la Ihram. Vazi hilo la kawaida huwatenganisha mahujaji na kila kitu ambacho ni nembo ya ubora na hadhi kama vile shughuli ya mtu, cheo chake, utajiri na kadhalika. Hivyo haji huwa tayari amejitenga na aina zote za sifa na vyeo vya kimatabaka, kikaumu na kadhalika.
Inapoanza amali na ibada ya twawafu na kuzunguka Nyumba ya Mwenyezi Mungu, mahujaji huanza taratibu kutekeleza amali hiyo wakiitikia wito wa Mola Karima kwa maneno ya labeka Bwana wangu labeka. Wakati huo mahujaji wote huwa wakizunguka katika duara la Tauhidi na kumpekesha Mwenyezi Mungu. Amali hii ni ishara ya uwezo mkubwa wa dini ya Uislamu ambayo inawakusanya mamilioni ya watu sehemu moja na kuwaelekeza upande mmoja. Mahujaji wote huwa katika hali moja, wakiwa wameelekeza fikra zao zote upande mmoja na kuelekeza mwili, masikio na macho ya roho zao upande mmoja.
Katika harakati hii ya twawafu mahujaji hujifunza darsa nyingine ya kujiepusha na uhasama, tabia ya kujiona bora kuliko wanadamu wengine, kujiweka mbali na tabia ya kupenda jaha na ukubwa na fikra za kichokozi na kukanyaga haki za wanadamu wenzao. Kwa hali na hisi hizi, mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu huwa wanabeba ujumbe wa amani na urafiki kwa wanadamu wote na kuwatangazia walimwengu kwamba, maadamu msingi wa siasa za viongozi wa dunia ni kuabudu na kutanguliza mbele pesa, jaha, kupenda ukubwa na kujiona bora zaidi, basi itakuwa vigumu sana kupatikana amani na utulivu duniani.
Ibada na amali za Hija ni fursa kwa wanadamu kupata tajiriba ya kuishi pamoja kwa amani na usalama. Kwani mamilioni ya mahujaji huamriwa kuwa salama na warehemevu kwa kila kitu kinachowazunguka kuanzia wanadamu wenzao, wanyama, wadudu na hata mimea na miti.
Hivyo kwa msingi huo Umma wa Kiislamu unaweza kushuhudia manufaa mengi ya Hija katika nyanja mbalimbali za kiutamaduni, kijamii, kiuchumi na kisiasa. Haya pia ni miongoni mwa malengo makubwa ya Hija yanayotajwa na Mwenyezi Mungu katika aya za 27 na 28 za Suratul Haji pale anaposema: "Na pale tulipomuweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut'ufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanaorukuu, na wanaosujudu. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali."
Kwa kutilia maanani haya yote Waislamu wanaweza kutumia mkusanyiko mkubwa wa ibada ya Hija kwa ajili ya kubadilishana uzofu na hivyo kukurubia zaidi kwenye maana halisi ya Hija. Ni matarajio yetu kwamba mkusanyiko wa mamilioni ya Waislamu katika ibada hiyo kubwa ya mwaka huu katika miji mitakatifu ya Makka na Madina itawaamsha Waislamu na kuimarisha zaidi umoja na mshikamano wao hasa katika kipindi hiki kigumu ambapo baadhi ya makundi yenye uelewa finyu na usio sahihi kuhusu Uislamu yamezusha fitina kubwa na kuhalalisha damu za Waislamu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …