Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 20 Septemba 2015 11:04

Dondoo za Hija (6)

Dondoo za Hija (6)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 6 ya mfululizo huu wa makala fupifupi za Dondoo za Hija.
Hija ni ibada yenye siri na maajabu mengi. Imesisitizwa mno kuitekeleza ibada hiyo tukufu kwa kila mwenye uwezo. Ni ibada ambayo baadhi ya wakati Mwenyezi Mungu humtakabalia mja wake ibada hiyo kwa kutenda amali japo moja njema. Abdullah Mubarak anasema, Mwaka mmoja nilikwenda kufanya ibada ya Hija na baada ya kuhiji nilitoka nje ya Haram nikapumzika sehemu fulani, kilepe cha usingizi kikanichukua. Ndani ya usingizi huo mfupi nikaona Malaika wawili wanashuka kutoka mbinguni, mmoja akamuuliza mwenzake, mwaka huu ni nani aliyetakabaliwa Hija yake, mwengine akajibu ni mtu mmoja mkazi wa Dimishq (Damascus, Syria) aitwaye Ali bin Muwaffaq, yeye hakuja kuhiji lakini Hija yake imetakabaliwa.
Abdullah akasema: Niliposhituka kwenye kilepe hicho cha uzingizi, nilijiambia, lazima niende Dimishq kumzuru Bwana huyu. Nilifunga safari hadi Dimishq na nilipobisha hodi, Bwana mmoja alinifungulia mlango na baada ya salamu nilimuuliza: Wewe waitwa nani? Alinijibu: Ali bin Muwaffaq. Nilimuuliza: Wafanya kazi gani? Alijibu: Kutia viraka. Nikamsimulia yaliyojiri kwenye kilepe changu cha usingizi na sababu za kuazimia nyumbani kwake na kumgogotezea anieleze alilofanya hata akatakabaliwa Hija yake bila ya kwenda kuhiji. Naye hakufanya ajizi kunielezea kisa chake. Alisema: Kwa muda mrefu nilikuwa na nia ya kwenda Hija. Nilidunduliza fedha zangu hadi mwaka huu zikatimia dirhamu mia tatu. Siku moja nikiwa najiandaa kwenda Hija, mke wangu ambaye alikuwa mja mzito, alitamani chakula fulani. Akaniambia, nenda ukaninunulie chakula kile, nami kwa minajili hiyo nikatoka nyumbani. Nikiwa njiani nilikutana na mama mmoja mjane aliyefiwa na mumewe na kuniambia, siku kadhaa usiku na mchana zimepita bila ya kutia chochote tumboni, mimi na wanangu. Leo nimepata mzoga wa mnyama, nimeamua kukata pande la nyama kwenda kupoza njaa ya wanangu. Niliposikia hayo, moyo uliniuma sana. Nilisema: Hija yangu imekaribia mno. Pamoja na hayo, chukua wewe hizi dirhamu mia tatu uzitumie kuwalisha chakula cha halali wanao.
Abdullah Mubarak akasema: Niliposikia kisa hicho nilisema, Mola wangu yajaalie niliyoyaona ndotoni yawe kweli na mtakabalie Hija yake mja wako huyu mwema.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …