Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 15 Septemba 2015 17:29

Dondoo za Hija (2)

Dondoo za Hija (2)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Wapenzi wasikilizaji Qur'ani tukufu imeiarifisha al Kaaba kuwa ndiyo nyumba ya kwanza ya Tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu na ya kale zaidi ya ibada ya wanadamu katika sayari ya dunia. Ni eneo ambako kwa miaka mingi Manabii, mawalii wa Mwenyezi Mungu na waja wake wema walifanya ibada hapo na kulipa utukufu na adhama eneo hilo. Kwa historia hiyo iliyojaa, utukufu al Kaaba imefadhilishwa na kutangulizwa mbele ya Baitul Muqaddas na kufanywa kibla cha walimwengu wote. Vilevile Mwenyezi Mungu SW ametumia historia hiyo ya al Kaaba kujibu malalamiko ya Wayahudi waliokuwa wakipinga suala la kubadilishwa kibla kutoka Baitul Muqaddas na kuelekea Makka takatifu. Sheikh Saduq (Mwenyezi Mungu amrehemu) anasema katika kitabu cha al Khisal kwamba: Hija ni mfano mdogo wa Uislamu mkubwa, kana kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kuuweka Uislamu wote katika ibada moja ili haji apate tajiriba ya Uislamu wote katika ibada hiyo. Kwa msingi huo Hija kati ya ibada zote nyingine, ina adhama ya aina yake na ni pana zaidi na yenye vifungu na vipengee mbalimbali.
Wito wa Tauhidi unaotolewa katika ibada ya Hija husafisha nyoyo na kuzitakasa, na amali zinazofanyika katika Mash'arul Haram huko Mina huwakumbusha wanadamu na kuwaonesha sura ya kifo na jinsi watakavyofufuliwa mbele ya Mola Qahari. Vilevile vikao na mikutano ya Waislamu katika ibada hiyo ya Hija huhuisha na kuimarisha utamaduni wenye utajiri mkubwa wa Kiislamu na kuondoa aina zote za mizizi ya utamaduni wa kiistiimari na kikoloni katika jamii za Waislamu. Ibada ya Hija huwahimiza Waislamu kutupilia mbali mifarakano na hitilafu zao na kuimarisha umoja na mshikamano. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kila mwaka Waislamu kutoka pembe mbalimbali za dunia hukusanyika katika eneo moja, wakati na kipindi maalumu wakiwa na vazi la aina moja na kufanya amali za aina moja na kushikamana na kamba imara ya Mwenyezi Mungu kwa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ya Uislamu. Kwa njia hii ndipo mahujaji wanapoweza kupata faida za ibada hiyo adhimu ambazo Mwenyezi Mungu SW ameziashiria katika aya za 27 na 28 za Suratul Hajj zinazosema: Na watangazie watu Hija, watakujia kwa miguu na juu ya kila mnyama aliyekonda kutoka kila njia ya mbali. Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jila la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu... Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …