Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Alkhamisi, 25 Oktoba 2012 11:25

Idul Haji na Hija Kuu

Idul Haji na Hija Kuu

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika makala hii maalumu inayokujieni kwa mnasaba wa sikukuu ya Idul Haji. Ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kuwa nasi hadi mwisho wa kipindi chetu cha leo.  XXXXX

Siku ya tarehe 10 Dhilhaji inasadifiana na sikukuu kubwa ya Waislamu kote duniani. Sikuu hii adhimu inakumbusha tukio la kujitolea na kujisabilia kwa Nabii Ibrahim na mwanaye Ismail (as) kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu SW na kujisalimisha kwake.

Sikukuu ya Idul Adh'ha ambayo hufanyika baada ya mahujaji kusimama katika uwanja wa Arafa ni idi na sikukuu ya kujikomboa kutoka kwenye makucha ya dunia na anasa zake. Ni siku ya kuthibitisha uja na kujisalimisha mbele ya Mola Karima. Ni siku ambayo mahujaji huchinja na kukata kabisa mahusiano yao na asiyekuwa Mola Mlezi na kusherehekea wakimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikiwa kukamilisha ibada ya hija na kushinda vita dhidi ya Shetani mlaaniwa.

Siku moja Nabii Ibrahim al Khalil (as) aliota akimchinja mwanaye kipenzi Ismail kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu. Baada ya ndoto hiyo kukariri mara tatu Nabii huyo adhimu wa Mwenyezi Mungu alielewa kwamba, anapaswa kumtoa mwanaye mhanga na kama dhabihu kwa ajili ya kutimiza amri na matakwa ya Mola Mlezi. Hivyo alichukua azma ya kumchinja mwanaye kipenzi na kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kushauriana na mwanaye Ismail na kumweleza kisa kizima. Alimwambia: Mwanangu mpenzi, nimeota kwamba ninawajibika kukuchinja, waonaje?

Ismail ambaye kama alivyokuwa baba alikuwa amezama katika kumpenda Mola Karima, alimjibu baba yake kwa kusema: "Tekeleza uliyoamrishwa na utanipata mimi ni miongoni mwa wenye kusubiri." (suratu Saaffat-102)

Moyo na imani hii kubwa ya kusalimu amri kikamilifu mbele ya matakwa na amri ya Allah ya baba na mwanaye ilimkera mno Shetani mal'uni na akaamua kujifunga kibwebwe kwa ajili ya kuvuruga na kuwazuia kutekeleza mtihani huo wa Allah. Alianza kwenda kwa baba, Ibrahim na mwanaye Ismail akijaribu kuwashawishi wasitekeleze amri hiyo ya Mwenyezi Mungu bali hata kutumia mbinu za kumwendea mama yake Ismail, alimradi waja hao wema washindwe mtihani huo mkubwa. Hata hivyo Iblisi mal'uni hakufanikiwa. Imepokewa katika hadithi kwamba Iblisi alimwendea Nabii Ibrahim akiwa Mina katika Jamara ya Kwanza na mtukufu huyo akampiga mawe saba na kumfukuzia mbali. Iblisi alimfuata tena Nabii Ibrahim katika Jamara ya Pili akijaribu kumshawishi asitekeleze amri ya kumchinja mwanaye. Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu pia alimfurusha kwa kumrushia mawe saba na akakariri hivyohivyo katika siku ya tatu.

Hatimaye siku muhimu iliwadia. Baba aliyekuwa akimpenda mno mwanaye kipenzi alimlaza mtoto kwenye ardhi na kuweka kisu kikali kwenye shingo yake. Alianza kuchinja na kujaribu kukata shingo ya mwanaye ili kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu lakini kadiri alivyochinja kisu kilikataa kukata na kikawa butu. Alishikwa na mshangao mkubwa na kuwa bumbuazi. Aliweka tena kisu hicho kikali kwenywe shingo ya mwanaye Ismail na kuanza kuchinja kwa nguvu zaidi huku Malaika wa Mwenyezi Mungu wakiangalia kitendo hicho cha ikhlasi, imani na kujisabilia kwa mshangao. Katika hali hiyo Ilisikika sauti kutoka mbinguni ikimwambia Nabii Ibrahim: Hakika umesadikisha na kutimiza ndoto ewe Ibrahim, na hivi ndivyo tunavyowajazi watendao wema. (Saaffat 104-105) Hapa Mwenyezi Mungu SW alimtuma kondoo ili Nabii Ibrahim amchinje badala ya mwanaye Ismail.

Tukio hilo la kumtoa Ismail kama dhabihu lina darsa na somo kubwa la kuridhia na kusalimu amri kikamilifu mbele ya matakwa na amri za Mwenyezi Mungu. Baba aliamrishwa kumchinja mwanaye kipenzi na wote wawili wakasalimu amri mbele ya matakwa ya Mola wao na kuchinja matamania na matakwa ya nafsi zao katika uwanja wa Mina licha ya vishawishi vya Iblisi mal'uni.

Mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu kabla ya kuchinja wanyama kama mbuzi, ngamia na kadhalika wanapaswa kuziweka nafasi zao katika madhabahu na kuzitoa mhanga. Kwa msingi huo Mwenyezi Mungu SW anasema katika aya ya 37 ya Suratul Hajj kwamba: Nyama na damu za wanya hao wanaochinjwa hazimfikii Mwenyezi Mungu, lakini inamfikia Yeye takwa na uchamungu wenu." Hivyo basi hekima na manufaa yaliyomo katika ibada hii ya hija ambayo ni takwa, inarejea kwa mahujaji wenyewe. Takwa na uchamungu humkurubisha zaidi mwanadamu kwa Mola na kuisafisha nafsi yake. Imam Sadiq (as) anasema: "Wakati unapochinja mnyama wa dhabihu kata koo na mshipa wa matamanio ya nafasi na tamaa." Nukta ya kuvutia katika hadithi hii ni kule kushabihisha tamaa na koo la matamanio. Huenda ni kwa sababu ya takwa, ikhlasi na uchamungu unaopatikana katika amali hii ya kutoa dhabihu wakati wa hija ndio maana Idi hii ya al Adh'haa ikatambuliwa katika hadithi za Kiislamu kuwa ndio Idi kubwa ambayo husherehekewa na mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu baada ya mashaka mengi ya kutekeleza ibada ya hija na kujiepusha na vishawishi vya kidunia na nafsi.

Mpenzi msikilizaji kila amali ya ibada ya hija ina siri na hekima zake ambazo zote zinalenga kulea na kutakasa nafsi ya mwanadamu. Kuanzia amali ya kuvaa Ihram, talbia, kutufu al Kaaba, kukimbia baina ya Safa na Marwa, kusimama Arafa hadi kutoa dhabihu na kadhalika vyote ni kwa ajili ya kutakasa nafsi ya mjaa na kumkurubisha kwa Allah SW.

Baada ya kutoa dhabihu, haji hulazimika kunyoa nywele zake au kupunguza nywele na kukata kucha zake. Kwa kawaida nywele huwa sehemu ya mapambo ya mwanadamu lakini mahujaji wanapomaliza kutoa dhabihu na kuchinja mnyama hulazimika kunyoa nywele zao na kuweka umaridadi wao wa kidhahiri katika madhabihu ya upendo na kuikurubisha nafsi kwa Mola wake. Kwa hakika amali hii huchinja ghururi na kiburi cha mja ambaye baada ya hapo hurejea Makka kwa ibada zaidi.

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa dua ya siku ya Arafa ya Imam Ali bin Hussein Zainul Abidin (as) akizungumzia jinsi mahujaji wanavyonyoosha mikono na kumtaradhia Mola katika siku hiyo. Anasema katika sehemu moja ya dua hiyo kwamba: Ewe Mola, Hii leo ni siku adhimu ambapo waja wako wanaokupwekesha wamekusanyika katika sehemu moja kutoka maeneo mbalimbali ya dunia. Wote wanakuomba Wewe na wamekunyooshea mikono wakiwa na matarajio na rehma zako na kuogopa adhabu na ghadhabu zao. Unawatazama katika hali hiyo na kuwatimizia haja zao. Ewe Mola Mlezi msalie Muhammad na Ali zake na utushirikishe katika dua za waja wako wema wanaokuomba wewe katika siku hii.

Ewe Mola wa walimwengu, tumekuja na haja zetu mbele yako na kuweka vikapu vya umaskini na ufukara mbele ya mlango wa nyumba Yako. Mola Mtukufu! Msalie Muhammad na Ali zake na utupe rehema zako. Tuonee huruma na utughufirie madhambi yetu. Aamin ya Rabbal Alamin. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.

                                           

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …