Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 24 Oktoba 2012 11:06

Pamoja na Mahujaji 3 (1433)

Pamoja na Mahujaji 3 (1433)

Bismillahir Rahmanir Rahim

Hija ni ibada ni miongoni mwa ibada zenye adhama kubwa na zenye athari mno  na kwa mtazamo wa Kiirfani ina siri na hekima zisizo na kifani. Majimui ya ibada za Hija ni dhihirisho la fadhila na utukufu wa kiakhlaqi. Ibada hii inaweza kuwa kivuko bora kabisa cha kuelekea kwa Mwenyezi Mungu na nyumba bora kabisa ya utakasifu na kulea nafsi. Majimui ya amali za Hija ni uwanja bora kabisa wa uja na unyenyekevu. Kuhusiana na suala hili, mwana Irfani mkubwa wa zama hizi, Mirza Jawad Malaki Tabrizi anasema:

Lengo la kuwajibishwa Hija na ibada nyingine, ni kuimarisha engo ya kiroho ya mwanadamu na hivyo kumfanya mja huyu aondokane na mfungano wa ulimwengu wa mwili na kufikia ulimwengu wa kimaana na hivyo kuwa na ufahamu juu ya Mwenyezi Mungu na hivyo kuwa na urafiki na hali ya kuainisika na kujikurubisha na Mwenyezi Mungu na kwa muktadha huo kuwa katika ukarimu wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake."

Kwa hakika moja ya hekima muhimu katika Hija ni kupima kiwango cha uja na kuthibitisha na uja wa mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu. Baada ya Hujaji kuwa muhrimu katika eneo la Miqaat, wote kwa pamoja huingia katika mji wa Makka wakiwa na vazi moja jeupe la Ihramu. Huwezi kutofautisha baina ya tajiri na masikini. Kwa muktadha huo mandhari ya Hija hutawaliwa na rangi nyeupe, huku anga ya Makka ikitawaliwa na sauti za Talbiya zinazosomwa na Mahujaji.

Mtume Muhammad saw amenukuliwa akisema kuhusiana na thawabu za kusoma talibiya kwamba:

"Mtu ambaye atasoma talibya yaani Labbaika Allahumma Labbaika kwa siku moja hadi kuzama kwa jua, atafutiwa madhambi yake yote na kuwa kama siku ya kwanza alipozaliwa na mama yake."

Baada ya Mahujaji kuvaa vazi tukufu la Ihramu katika Miqaat, huwasili katika mji wa Makka. Makkat al-Mukarramah ni mahala alipokuwa akishuka Malaika wa Wahyi Jibril mwaminifu AS na kituo cha Mitume wakubwa wa Mwenyezi Mungu. Nuru ya Unabii wa Mtume wa mwisho ilionekana katika ardhi hiyo na Uislamu ambayo ni dini kamili, ilienea ulimwenguni ikitokea katika kitovu chake hicho yaani ardhi tukufu ya Makka. Mtume saw alipata taabu na masaibu mengi yaliyoambatana na mabalaa katika mji wa Makka vikiwemo vitimbi na maudhi ya akina Abu Sufiyan na akina Abu Jahal ; lakini hayo katu hayakuweza kumkwamisha, hivyo alifanya hima kubwa na kufanikiwa kuukuza mche mdogo wa Uislamu  aliokuwa ameupanda na kuwa mti mkubwa na wenye matunda mengi.

Baada ya Mahujaji kuingia katika ardhi ya Makka, huelekea katika Masjdul Haraam ambapo panapatikana pia Kaaba tukufu na hivyo hutia mguu katika haram ya Mwenyezi Mungu yenye amani. Haram ina maana ya mahala ambapo kila mtu anabakia katika usalama na amani. Watu na wanyama hubakia katika amani bali hata miti, maua na majani nayo husalimika na kila aina ya madhara. Kila kitu hapo huwa katika amani. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul Baqara aya ya 125 kwamba,  "Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Al-Kaaba) iwe pahala pa kukusanyikia watu na pahala pa amani."

Kwa msingi hu basi kila mtu atakayekuwa kando ya Kaaba, anakuwa yuko katika amani kimwili na kiroho na huwa na utulivu. Usalama na amani ya Nyumba hii ya Mwenyezi Mungu unatokana na dua aliyoiomba Nabii Ibrahimn AS kama inavyosema aya ya 126 ya Suratul Baqarah, "Na aliposema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho."

Mwenyezi Mungu aliijibu dua ya Ibrahim AS. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana kwa karne nyingi, al-Kaaba imesalimika na shari ya waitakiao mabaya. Kisa cha Abraha na jeshi lake la askari waliokuwa wamepanda tembo, ni jambo linaloweka wazi uhakika huu. Wakiwa hapo kwa hakika Mahujaji huwa katika wakati na lahadha muhimu kabisa. Mapigo yao ya moyo huenda mbio na kwa kasi; kwani ni lahadha za kuikaribia nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani Al-Kaaba. Kwa kuitazama Kaaba, Hujaji huhisi adhama ya nyumba hiyo ya Mwenyezi Mungu katika moyo wake.

Kwa hakika nyumba ya Mwenyezi Mungu yaani al-Kaaba, huwa na mvuto usio na kifani na huvizuta nyoyo za Mahujaji na kuifanya miili na roho zao kuwa na shauku ya kufanya tawafu. Kaaba ni nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo anaitaja kuwa kituo cha utulivu wa nyoyo. Vitabu vingi vya historia vimekubaliana kwa kauli moja kwamba, al-Kaaba ilijengwa katika zama za Nabii Adam AS. Baada ya Nabii Adam kuijenga Kaaba aliizunguka na kufanya tawafu. Hii ina maana kwamba, nyumba hii ilichaguliwa kwa ajili ya kumuabudu na kumdhukuru Mwenyezi Mungu kabla ya Nabii Ibrahim AS. Kwa hakika al-Kaaba ni nyumba ya Mwenyezi Mungu iliyobarikiwa na yenye uongofu. Mwenyezi Mungu anasema katika aya ya 96 ya Surat al-Imran kwamba, "Hakika Nyumba ya kwanza waliowekewa watu kwa ajili ya ibada ni ile iliyoko Makka, iliyobarikiwa na yenye uwongofu kwa walimwengu wote."

Kaaba ilikuwa sehemu na mahala pa ibada kwa Manabii wengi wa Mwenyezi Mungu. Nabii Ibrahim aliamrishwa na Mwenyezi Mungu aikarabati al-Kaaba. Mwenyezi Mungu anasema katika aya za 26 na 27 za Surat al-Haj kwamba, "Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut'ufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanaorukuu, na wanaosujudu. Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.

Kwa hakika fadhila muhimu ya Al-Kaaba ni kuwa, nyumba hii ni nyumba ya tawhidi na haina msukukumo mwingine usiokuwa wa Kimwenyezi Mungu katika kupatikana kwake na katika kuendelea kwake kuweko. Mahujaji wakiwa katika nyumba ya Mwenyezi Mungu hufanya tawafu katika mahala ambapo Malaika wanatufu na mahala ambapo Mitume wa Mwenyezi Mungu na mawalii wake walikuwa kando ya eneo hilo na kumhimidi Mwenyezi Mungu. Kaaba ina nafasi muhimu katika ibada za Kiislamu na vile vile maisha ya kijamii ya Waislamu. Kwa siku Waislamu husali mara tano Sala zao hali ya kuwa wanaelekea kibla yaani upande wa Kaaba. Hii kwamba, mamilioni ya Waislamu usiku na mchana husali Sala zao kwa nyakati maalumu wakiwa wote wameelekea kibla, yaani upande wa Kaaba huko Makka ni jambo ambalo huleta hali ya umoja na kuzikurubisha pamoja nyoyo zao. Mwenyezi Mungu amewataka Waislamu kuelekea Kaaba popote wawapo, kwani nyumba hiyo inapaswa kuwa kitovu cha umoja na mhimili wa mkusanyiko wa wana tawhidi. Umbo zuri la uja na kusalimu amri hunaonekana wakati Mahujaji wanapozunguka na kufanya tawafu katika al-Kaaba. Mtume saw amenukuliwa akisema kwamba, kila mtu ambaye atafanya tawafu mara saba katika nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba, basi huandikiwa jema kila hatua yake, hufutiwa dhambi na huongezewa daraja moja. Imam Ruhullah al-Musawi al-Khomeini RA anasema, falsafa ya kuzunguka na kutufu al-Kaaba ni kujikomboa kutoka katika minyororo ya dunia.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape uwezo na tawfiq ya kwenda kuhiji wale wote ambao hadi leo bado hawajafanikiwa kwenda kuhiji Makka. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh…

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …