Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 21 Oktoba 2012 11:43

Pamoja na Mahujaji-2 (1433)

Pamoja na Mahujaji-2 (1433)

Assalam Alaykum Warahmatullah Wabarakatuhu

Katika siku hizi tunashuhudia taswira ya mjumuiko wa wanaadamu katika ardhi takatifu za Makka na Madina ambapo nguvu ya Uislamu inadhihirika wazi. Waliofunga safari kuelekea katika kibla cha nuru wote kwa pamoja, pembizoni mwa al Kaaba wanamtukuza Mola Muumba kwa kusema:

Labbayka Allāhumma Labbayk. Labbayk Lā Sharīka Laka Labbayk. Inna l-Ḥamda, Wa n-Niʻmata, Laka wal Mulk, Lā Sharīka Lak.

Wapenzi wasikilizaji, Waislamu ambao wanaelekea katika Hijja wanapaswa kuwa na ujuzi kamili kuhusu safari hii ili wasitekeleze amali za Hija pasina kuwa na maarifa.

Kuifahamu kwa njia sahihi ibada tukufu ya Hija humuwezesha hujaji kupata muongozo kuhusu uhakika na ukarimu wa Mola Muumba na hivyo kuimarisha raghba yake katika utekelezaji wa ibada hiyo.

Wakati wa kuvaa Ihramu, hujaji anapaswa kusafisha nia yake na hivyo kutekelza ibada hii kwa ajili ya Mwenyezi Mungu pekee. Aidha anapaswa kuondoa hisia zote za kuwa mbora zaidi ya wengine katika masuala ya kidunia.

Katika ibada ya Hija tunashuhudia mamilioni ya watu kwa pamoja wakiwa wamejifunga vazi jeupe ambalo halijashonwa. Wote kwa pamoja, wakiwa mbali na vitu na masuala ya kidunia, wanaizunguka al Kaaba. Wamefika hapo kuitikia mwito wa Mwenyezi Mungu ambaye katika Qur’ani Tukufu sehemu ya aya ya 97 ya Surat Al I’mran anasema: “…Na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu imewajibikia watu wahiji kwenye Nyumba hiyo, kwa yule awezae njia ya kwendea…”

Kabla ya kuvaa Ihramu hujaji anatakiwa kufanya ghusli maalumu. Kwa hakika ghusli hii inaleta utakasifu.

Hekima ya Ihram ni kuwa wakati hujaji anapofika katika sehemu ijulikanayo kama Miqaat anaanza kutafakari kuhusu ni vipi aingie katika eneo takatifu la Mwenyezi Mungu na kutekeleza yote yampasayo katika Hija. Hapo anaweka nia ya kutekeleza amali zake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Imam Sadiq AS  amenukuliwa akisema: “Kuwa muhrimu ni kujiepusha na kila jambo linalokuweka mbali na Mwenyezi Mungu na kukufanya usimche..” (Misbah al Shariat Bab 22).

Ihramu huvaliwa katika maeneo ya Hija yajulikanayo kama Miqaat. Mahujaji wakiwa Madina wakati wanakusudia kuelekea Makka huvaa Ihramu katika msikiti mashuhuri wa Shajara ulio karibu na Madina.

Msikiti huo ulipewa jina hilo kutokana na kuwa Mtume SAW katika zama za mwanzo wa Uislamu alivaa Ihramu chini ya mti uliokuwa eneo hilo.

Hija ni ibada iliyona amali mbalimbali zenye taathira za ajabu. Ibada ya Hija ni kiunganishi baina ya dunia na akhera. Katika ibada hii mwanadamu anajitayarisha kukubali na kuufahamu ukweli kuhusu mkusanyiko wa Siku ya Kiyama. Safari ya kimaanawi ya Hija hufanyika baada ya kuaga familia na aghalabu ya mahujaji husafiri kutoka miji na nchi za mbali. Kwa hakika safari hii ni mithili ya safari ya kuelekea ulimwengu wa malakuti. Kwa kuvaa vazi jeupe la Ihramu na kujiunga na halaiki kubwa ya watu wavao vazi hilo, sambamba na kutekeleza amali mbalimbali za Hija, ni tukio linaloshabihiana na Siku ya Kiyama.

Mahujaji kwa kuvaa vazi la Ihramu wote kwa pamoja na kwa kutupilia mbali vitu vya kidunia kama vile vyeo, utajiri n.k huwa wanakusudia kutambua uhakika pasina kuwepo na vishawishi vya kidunia. Wakiwa katika safari hii ya kimaanawi, mahujaji huwa katika mazingira yaliyotakasika na huweza kutambua uhakika wa kuwepo kwao na hivyo kufahamu upungufu walionao. Hujaji katika Nyumba ya Allah SWT wakati akiwa amevalia Ihramu anapaswa kujiweka mbali na masuala kama vile kujifakharisha, ubinafsi na kujihisi kuwa bora zaidi ya wengine. Tokea lahadha anapovaa Ihramu, mwenye kuhiji anapaswa kuwa mwangalifu sana kuhusu mwenendo na maneno yake yote. Kwani kuna mengi anayokatazwa mwenye kuvaa Ihramu. Kwa hakika katika maeneo matakatifu ya Mwenyezi Mungu, shetani huwa amepigwa marufuku hapo. Maeneo hayo huwa ni ya amani na utulivu.

Ili mahujaji waweze kuhisi athari ya kina kuhusu Hija hutakiwa kubadilisha hali yao ya kidhahiri na kuondoka katika mazingira ya kiduni. Yule mwenye kuvaa Ihramu anapaswa kuingia katika maeneo matakatifu na awe na tabia inayoenda sambamba na hadhi ya eneo alilofika.

Ni kwa sababu hiyo ndipo Imam Sajjad AS wakati alipokutana na mtu ajulikanaye kwa jina la Shibli ambaye baada ya kuhiji alifika mbele ya mtukufu huyo ambapo Imam alimuuliza: “Je umetekeleza Hija?: Akasema ‘Ndio Ewe Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu’. Imam akasema: “Je ulifika katika miqaati na kutoa nguo zako zilizoshonwa na kufanya ghusli. Shibli akajibu kwa kusmea:  "Ndio. Imam akamuuliza: Je wakati ukiwa Miqaat ulifanya nia ya kujivua nguo za maasia na ukaidi na badala yake ukavaa vazi la utiifu kwa Mwenyezi Mungu? Shibli akajibu kwa kusema: “La”. Imam akamuuliza: ‘Wakati wa kufunga mkataba wa Hija je ulikusudia kuacha mkataba wowote usiokuwa wa Mwenyezi Mungu? Shibli hapo pia akajbu la, naye Imam akasema: ‘Haukuvaa Ihramu, haukutakasika na wala haukutia nia ya Hija!”

Mambo ambayo ameharamishiwa aliyevaa ihramu humuwezesha mwanadamu kuimarisha uwezo wake wa kupambana na matamanio ya nafasi. Kwa mfano mambo yaliyoharamishwa wakati wa Ihramu kama vile marufuku ya uwindaji, kusema uongo na mabishano ni mambo ambayo mwanadamu akijizuia kuyafanya huweza kufika katika hali ya juu ya utukufu.

Iwapo tutachunguza falsafa na sababu ya kuharamishwa baadhi ya mambo yaliyokatazwa wakati wa Ihramu tunaona kuwa masuala kama vile kulinda mazingira, wanyama na kuheshimu haki za viumbe wote ni kati ya malengo ya sheria za Ihramu.

Kwa kujizuia kutenda vitendo kama hivyo mwanadamu huwa anapita katika kipindi cha mafunzo ambayo humuwezesha kufikia takwa kivitendo. Kila moja ya amali za Hija humlea mwanadamu na kumuwezesha kujilinda kutokana  vishawishi na matamanio ya kinafasi na hivyo kufanikiwa kujidhibiti.

Mambo yote yaliyoharamishwa wakati wa Hija ni dhihirisho kuwa ibada hii humjengwa mwanadamu na kumuwezesha kuwa na Takwa.

Mtu aliyevaa Ihramu na kuingia katika eneo takatifu hujitahidi kuwa na takwa.

Ukiangazia yaliyoharamishwa wakati wa Hija utaona mengi yaliyokatazwa ni yale ambayo yanahusu mtu kujidhuru mwenyewe katika maisha yake au kuwadhuru wanadamu wenzake na wanyama.

Kwa  hivyo mtu ambaye ametekeleza  ibada ya Hija ipasavyo, anapovua vazi la Ihramu na kurejea nyumbani anapswa kuwa ameshabadilisha mwenendo wake na asiwe ni mwenye kuwadhuru wengine. Anapaswa kuchunga na kudhibiti matamanio yake ya kijinsia. Anapaswa kuchunga fikra na maneno yake na kuendesha kila kitu katika maisha yake kwa ajili ya Allah SWT.

Mpenzi msikilizaji yanayopaswa kuzingatiwa katika vazi la Ihramu ni kuwa kati ya mengine linapaswa kuwa safi na lililotahirika na lisiwe la kughusubiwa. Wanaume wanapaswa kutumia Ihramu na wasiwe na wamevaa vazi lolote lililishonwa. Kwa kawaida Ihramu huwa ni taulo mbili nyeupe na huvaliwa kwa njia maalumu. Baada ya kuvalia Ihramu hujaji husali sala ya rakaa mbili na kisha hapo hutamka talbiya ifuatavyo: Labbayka Allāhumma Labbayk. Labbayk Lā Sharīka Laka Labbayk. Inna l-Ḥamda, Wa n-Niʻmata, Laka wal Mulk, Lā Sharīka Lak.

Mtume SAW alisema: “ Mwenye vazi la Ihramu akifanya hivyo kwa imani na matumani ya kupata thawabu za Mwenyezi Mungu na kusema mara saba “Labbaik” Mwenyezi Mungu atachukua ushahidi wa maelfu ya Malaika kuwa amesalimika kutoka moto wa Jahannam na unafiki.”

Mwenye kuhiji anapotamka Labbaik huwa yuko tayari kuizuri Nyumba ya Allah SWT na kutufu hapo ili lahadha kwa lahadha aweze kuimarisha uhusiano wake na Allah.

Bottom of Form

 

 

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …