Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 20 Oktoba 2012 12:55

Pamoja na Mahujaji 1 (1433)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika kipindi hiki maalumu kinachokujieni kwa mnasaba wa kuwadia msimu wa ibada ya Hija. Msimu wa Hija umewadia tena. Kwa mara nyingine tena imewadia safari ya uja na mapenzi kuelekea katika ardhi tukufu ya Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada tukufu ya Hija. Ni safari fupi lakini iliyojaa nembo na siri kubwa. Hija ni safari ya siku chache lakini yenye matunda na manufaa makubwa mno. Ni safari ya siku kadhaa lakini yenye kuwa na mafunzo ya karne kadhaa. Ardhi ya Makka ambayo ni ardhi ya Wahyi, katika wakati huu hufurika makundi kwa makundi ya Mahujaji waliowafikishwa kwenda kutekeleza moja ya ibada muhimu katika dini tukufu ya Kiislamu, ibada ambayo ni wajibu kuitekeleza mara moja tu katika kipindi cha umri wa mwanaadamu Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki maalumu, karibuni. QASIDA

Tumo katika masiku ya mwezi mtukufu wa Dhul Hija ua Mfunguo tatu.  Mwezi huu mtukufu unasadifiana na mkusanyiko na kongamano la mamia kwa maelfu ya wanatawhidi katika ardhi tukufu ya Makka ili watekeleze ibada isiyo na kifani ya Hija. Waislamu walio na uwezo na waliopata tawfiki wa kutoka kila kona ya dunia, katika masiku haya huelekea katika ardhi ya Makka na katika nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba. Mkusanyiko adhimu wa Mahujaji katika Hija ni kujibiwa dua ya Nabii Ibrahim AS ambaye siku ile alipomuacha jangwani mkewe Hajar na mwanawe Ismail alimuomba dua hii:

"Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuriya zangu katika bonde lisilo kuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu Mlezi, ili washike Sala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapata kushukuru."   

Ni karne nyingi zimepita tangu wafanya ziara wakiwa makundi kwa makundi walipoanza kuelekea katika nyumba ya Mwenyezi Mungu al-Kaaba, ili waweze kunufaika na matunda ya ibada ya Hija sambamba na kupata fursa ya kutwalii historia ya Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Mkusanyiko mkubwa huu wenyewe unaonesha kuweko siri kubwa katika Hija na wakati huo huo kila ibada miongoni mwa ibada za Hija, iwe ni kufanya Saii baina ya Safa na Marwa, ramiul jamaraat, kuchinja, kunyoa na kadhika ina hekima na falsafa yake maalumu. Hekima kubwa ya Hija ni kudhihirisha uja kwa Mwenyezi Mungu ambapo jambo hili linashuhudiwa dhahir shahir katika amali zote za Hija.

Kwenda sambamba mafundisho ya Mwenyezi Mungu ya Uislamu na fitra na maumbile ya mwanadamu, ni miongoni mwa sifa maalumu na za kipekee za dini ya Uislamu. Hili ni jambo linaloonesha hali ya kudumu na kuwa kimataifa sheria tukufu za Kiislamu. Kila ibada miongoni mwa ibada katika Uislamu ina siri yake ambapo kufahamu matunda matamu na ya thamani ya ibada hizo hakuwezekani isipokuwa kwa kufahamu na kudiriki kwa usahihi ibada hizo. Katika ibada ya Hija pia hali iko namna hii. Mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, hufika Makka wakitokea maeneo ya mbali tena baada ya kuvuka na kupita vizingiti vingi likiwemo suala la gharama kubwa ya ibada ya Hija ambapo wakiwa katika eneo la Miqaat huvua nguo zao za kawaida na kuvaa vazi tukufu la Ihram na hatua ya Hujaji ya kuanza kusoma talbiya yaani "Labbaika Alahumma Labbaika" anakuwa Muhrimu na kisha huenda Makka na kufanya tawafu. Hufanya sai baina ya Safa na Marwa. Baada ya hapo Hujaji hupunguza nywele na kukata kucha na kisha huelekea katika marasimu ya Hija ya Tamattui katika jangwa la Arafa. Hubakia huko kwa nusu siku na kisha baadaye Mahujaji hufanya harakati kuelekea katika Mash'ar al-Haram na kubaki huko kwa masaa kadhaa. Linapochomoza jua Mahujaji huelekea katika ardhi ya Mina. Baada ya kutekeleza ibada maalumu katika Mina hurejea tena Makka na kufanya tawafu, saii baina ya safa na Marwa na kufanya tawafu Nisaa. Kwa utaratibu huo Hujaji anakuwa amekamilisha ibada ya Hija na hurejea katika mji na nchi yake akiwa na furaha tele kutokana na kuwa na matumaini ya kupata ridhaa za Mwenyezi Mungu.

Hata hivyo swali la kimsingi la kujiuliza ni hili kwamba, Hija ni hizi ibada na amali za kidhahiri bila ya kuweko mabadiliko katika miamala, vitendo na tabia za Mahujaji? Hapana shaka kuwa, kila amali miongoni mwa amali za ibada ya Hija ina siri kubwa ndani yake.

Kwa hakika kila Hujaji akiwa katika ibada ya Hija hudiriki adhama ya ibada hii tukufu kulingana na kiwango chake cha imani na ufahamu wake na hivyo kustafidi na faida pamoja na sudi za kimaanawi zinazopatikana katika ibada hiyo ambayo ndilo kongamano kubwa kabisa la Waislamu kutoka kila kona ya ulimwengu. Kwa mtazamo wa mahujaji, ibada ya Hija ni fursa ya kuitakasa roho katika mafundisho ya tawhidi na kuifanya roho hiyo ifanye harakati kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Kama ambavyo Uislamu unataka kujenga jamii mpya baina ya Waislamu, ndivyo hali inavyoonekana na kudhihiri katika ibada ya Hija. Ibada ya Hija imejaa taamali kubwa juu ya maisha na historia ya watu waliotengeneza historia kama Nabii Ibrahim, ismail na Bi Hajar. Kila hujaji anayepata fursa ya kusafiri katika ardhi hiyo tukufu, anapaswa kujiondoa na uja usiokuwa wa Mwenyezi Mungu ili aweze kushinda majaribu na mitihani ya Mwenyezi Mungu kama walivyoshinda Nabii Ibrahim na Ismail (as). Hija katika Uislamu ni sawa na safari ya mtu kwenda kujitengeneza, safari ambayo inaambatana na ratiba maalumu na katika kipindi na wakati makhsusi. Hija ni ibada ambayo inataathira kubwa kwa aliyewafikishwa kutekeleza ibada hii na ndio maana Mahujaji wanausiwa kwamba, wanaporejea makwao wasiridhike tu kuitwa Al-Haj au Hajat bali wanapaswa kujitahidi kurekebisha mwenendo wao na kudumisha yale waliyojifunza katika ibada hiyo.  Mahujaji wa nyumba ya Mwenyezi Mungu pindi wanapotamka na kukariri Talbiya yaani "Labbaika Allahumma Labbaika" hutangaza utayarifu wao wa kuonyesha uja na taadhima yao mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja. Aidha kwa kusoma Talbiya Mahujaji hutangaza kuwa, wako tayari kupokea wito na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muktadha huo tunaweza kusema kwamba, ibada ya Hija humfanya mja azikwee na kuzifikia thamani za kimaanawi na kumuondoa kabisa katika mfungamano wake na masuala ya kimaada na kidunia.

Sharti muhimu na la kwanza katika ibada ya Hija ni nia safi na yenye ikhlasi moyoni. Moyo wa mwanadamu unapaswa kusafika na kila asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo mzigo wa dhambi unaweza kumfanya mja asihisi ladha tamu ya kunong'ona na Mwenyezi Mungu. Hivyo anapaswa kunuia kuacha dhambi kwa ajili ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu ambapo kwa hakika hili ni shartmu muhimu la kutakabaliwa ibada ya Hija. Hapana shaka kuwa, ibada ya Hija ambayo ni ibada ya kimaanawi na kisiasa, mwaka huu inatarajiwa kutawaliwa na anga maalumu kutokana na na kushadidi njama za maadui za kuvunjia heshima matukufu ya Kiislamu.

Na hadi hapa ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki maalumu cha Hija, ninakuageni nikikutakieni kila la kheri. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …