Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Aprili 2008 15:15

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (6)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo. Hii ni sehemu ya sita ya mfululizo wa makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi. Ni matumaini yetu mtafaidika na makala hii. Karibuni.


***

Leo hii wanaadamu tunahitiaji fikra na mtazamo wa dini kuhusiana na jinsi inavyoweza kusaidia na kuwa na nafasi katika masuala mbalimbali hasa nafasi na taathira yake katika masuala ya kiroho na kinafsi ya mwanadamu kuliko kipindi kingine chochote kile. Wasomi na wananadharia wengi nao wanaamini kwamba, dini ina taathira ambayo haipingiki katika usalama na uzima wa roho na mwili na nyanja nyingine za maisha ya mwanadamu. Makala yetu ya juma hili itaanza kuchunguza taathira ya imani katika mtazamo wa mwanadamu kwa uwepo.
Kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu, mtazamo wa mwanadamu kwa ulimwengu au kwa maneno mengine mtazamo wa Muislamu kwa ulimwengu huu unasaidia kukinga na kuzuia mvurugiko wa mawazo kama vile, wasi wasi, kuhisi kuchanganyikiwa, kutokuwa na utulivu na kukata tamaa. Uislamu unaamini kwamba, endapo usalama na uzima wa kifikra hautapatikana basi uzima wa nafsi nao hauwezi kuwepo. Kwa maana kuwa, uzima wa fikra unakwenda sambamba au unategemea uzima wa nafsi. Vitu viwili hivyo hubainisha shakhsia ifaayo ya mwanadamu. Hapana shaka kuwa, aina ya mtazamo wa watu kwa maisha na yanayojiri ulimwenguni ni mambo ambayo huwa na taathira katika mienendo yao. Baadhi ya wataalamu wa masuala ya kisaikolojia wanaamini kwamba, hali ya kiroho na aina ya mtazamo wa wanadamu kuhusiana na maisha huchangia katika mienendo na miamala yao. Wanaamini kwamba, mwanadamu ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusiana na jinsi anavyoyatazama maisha. Kwa maneno mengine ni kuwa, wataalamu wengi wa Kiislamu na weledi wengi wa masuala ya elimu ya miamala na masuala ya kinafsi na kisaokolojia wanaamini kuwa, kumuamini Mwenyezi Mungu ni moja ya mambo yanayomfanya mja awe na mtazamo mzuri kuhusiana na masuala mbalimbali. Mja mwenye imani kwa kuwa na shakhsia salama hutambua kwamba, ulimwengu huu una muumba na si tu kwamba, kauumba ulimwengu huo bali ana mamlaka nao na vile vile kila kinachotokea kinatokea kwa udhibiti, usimamizi na uendeshaji wake. Kwa maana kwamba, yeye ndiye mwenye mamlaka kamili na ulimwengu huu na vilivyomo.
Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuonyesha mwanadamu njia ya kweli na nyoofu na endapo mja ataichagua njia hiyo ya kweli na haki, basi Mwenyezi Mungu humpa tawfiq na kumfanya afanikiwe katika uwanja huo. Kwa utaratibu huo, mja mwenye imani, kwa kufanya amali njema ana yakini na msaada wa Mwenyezi Mungu. Kwa mtazamo wa mtu kama huyo, licha ya nguvu na uwezo wote alio nao Mwenyezi Mungu lakini hamdhulumu yeyote. Fauka ya hayo, Allah huyapokea maombi ya waja wake na yuko nao karibu mno. Allah hukubali toba ya kweli kwa yule aliyefanya dhambi na kuamua kuomba msamaha na maghfrira na mja yoyote aliyeamua kuacha mwenendo mmbaya na kurejea kwa mola wake na kuahidi kutenda mema na kuacha mabaya hujumuishwa katika msamaha na bahari isiyo na mwisho ya rehma za Mwenyezi Mungu mwenye huruma kwa waja wake. Yeye ni mola ambaye ni chanzo cha vizuri vyote na mambo yote mazuri ya humu duniani. Kwa mtazamo huo mja katu hawezi kuiona dunia kuwa kitu kisicho na malengo maalumu. Dunia ni soko ambalo wengine hupata faida katika biashara yao ilhali wengine hupata hasara. Kwa hakika dunia ni mahala pa kila mtu kuonyesha jitihada zake katika kutenda mambo mema. Kwa maana kwamba, mwenye kujitahidi kutenda mema humu duniani na kujiepusha na yale yote yaliyokatazwa na dini tukufu ya Kiislamu basi hapana shaka kuwa, atachuma alichopanda na kupata ujira mnono kesho Akhera. Mwanadamu hana budi kufahamu kwamba, matendo yetu yote yapo chini ya uangalizi wa muumba wa ulimwengu huu. Ni kweli kwamba, matukio machungu na matamu humu duniani huacha athari mbaya au nzuri na kawaida huvuruga utulivu wa kifikra na kinafsi. Hata hivyo waja wenye imani thabiti huwa hawajihisi kuwa peke yao hata katika taabu na mashaka makubwa humu duniani. Hali hiyo inatokana na kuamini kwao kwamba, mola muumba wa ulimwengu huu daima yupo pamoja nao. Mwanadamu kwa kuwa na tegemeo na kimbilio hilo kubwa na lisilo na kikomo, hujiambia katika nafsi yake kuwa, sijaachwa peke yangu, na jitihada zangu katika ulimwengu wa uwepo hazitakuwa za hivi hivi tu. Kutokana na mja kuwa na mtazamo huo mzuri au chanya na kuyatazama mambo kwa uhakika wake, hujiandalia mazingira mazuri kwa ajili ya kuifanya nafsi yake kuwa nzima na salama na hivyo kuepukana na maradhi ya kifikra, kisaikolojia na kinafsi. Ni kwa kuzingatia hayo ndipo kila mwenye akili timamu atakubaliana nami kwamba, dini ina nafasi muhimu katika kila kitu na kila jambo la mwanadamu katika maisha yake ya kila siku.
Dakta William James mwanasaikolojia wa Kimarekani anasema kama ninavymnukuu: ''Imani ni nguvu ambayo inapaswa kuwepo kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu katika masuala mbalimbali maishani. Kutokuwa na imani ni kengele ya hatari ya kushindwa mwanadamu kukabiliana na taabu na matatizo katika maisha yake. Mwisho wa kunukuu.


***

Wapenzi wasomaji katika makala zetu zijazo tutazungumzia athari za imani juu ya Mwenyezi Mungu kinafsi na kifikra na katika mwenendo na miamala ya mwanadamu. Kwa leo Makala yetu ya Mwandamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi inaishia hapa, jiungeni nami katika makala nyingine. Mnaweza kututumia maoni yenu kupitia barua pepe yetu ya This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. .
 

Tuma maoni yako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …