Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Aprili 2008 15:12

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (5)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu


Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo. Hii ni sehemu ya tano ya mfululizo wa makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi. Ni matumaini yetu mtafaidika na makala hii. Karibuni.
Kwa mujibu wa mtazamo wa Uislamu kila mwanadamu anapozaliwa huwa na fitra na dhati au maarifa juu ya Mwenyezi Mungu. Uwepo wa mwanadamu ni kwa namna ambayo uwepo wake huo humuongoza kwa Mwenyezi Mungu. Hukuna tofauti baina ya wanadamu katika uwanja huo kuhusiana na suala hilo. Wanadamu wote pindi wanapozaliwa yaani wakati wa kuanza maisha yao mapya hapa duniani, huwa na mtazamo wa ndani wa kutafuta haki na kupata saada na ukamilifu.
Kutokana na mwanadamu katika dhati na asili yake kuwa na maarifa juu ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu huyu ana haja ya kuabudu na kumuomba Allah, hitajio ambalo halibadiliki kulingana na zama hizo ama zile. Hivyo basi kupuuza haja hiyo ya kiroho ndiko kunakomuongezea mwanadamu madhara na matatizo ya kinafasi na kisaikolojia. Kama tulivyoashria katika makala zetu zilizotangulia, imani juu ya Mwenyezi Mungu na kushikamana na mafundisho yake humuongezea mja usalama na uzima wa nafsi na fikra.
Tajiriba ya watu wengi inaonyesha kuwa, pindi mwanadamu anapokuwa na maumivu yake na akakata tamaa kwamba, misaada ya wengine inaweza kumsadia kupunguza maumivu yake ya kiroho na kimwili, kuna kitu au hisia ndani ya roho ambayo humuongoza kwa uwepo wa kudumu yaani Mwenyezi Mungu na kumuonyesha kwamba, ni kwa kumtegemea yeye tu ndipo anapoweza kuepukana na matatizo yote yanayomkabili.
Kwa maneno mengine ni kuwa, katika hali kama hiyo mwanadamu hujikuta anahitajia msaada wa Mwenyezi Mungu na kuamini kwamba, ndiye atakayemsaidia kumuondolea masumbuko ya nafsi, wasi wasi na mvurugiko wa mawazo. Mtu kujihisi kuwa, hana kimbilio na kwamba yeye si lolote si chochote ni kuzidi kujiongezea matatizo ya kinafsi na mvurugiko wa mawazo. Lakini kuamini kwamba, kuna Mola Muumba na kimbilio la kila mja, Mola ambaye ni chemchemi ya kila neema na kila jema, ni mhimili na nguvu kubwa ambayo inaweza kumsaidia mwanadamu aondokane na matatizo ya kinafsi na kuelekea katika utulivu wa fikra na akili.
Kuamini suala hili kuwa, kuna Mwenyezi Mungu mmoja ambaye anadhibiti na kusimamia kila kitu humfanya mwanadamu awe na matumaini na katu asikate tamaa. Aghalabu ya waumini huhisi uhusiano wao na Mwenyezi Mungu ni kama wa baina ya marafiki wawili na kwamba, kwa kumtegemea muumba wa ulimwengu huu wanadamu wanaweza kupunguza matukio na majanga yasiyodhibitika.
Ernest Adlfer tabibu na mpasuaji wa Kimarekani anasema, kwa uzoefu niliokuwa nao nilifikia natija hii kwamba, kuanzia sasa ni lazima sambamba na kumtibu mgonjwa kwa kutumia suhula za kitiba, upasuaji na kadhalika, inapaswa pia kumjenga kiroho kwa kukuza nguvu za imani yake kwa Mwenyezi Mungu. utafiti unaonyesha kuwa, asilimia kubwa ya wagonjwa katika miji mbalimbali nchini Marekani wanaokwenda kwa daktari huwa hawana dalili zozote zile za kidhahiri za maradhi ya mwili. Hata hivyo madaktari wanaona kuwa, chanzo halisi cha maradhi yao ni dhambi, kulipiza kisasi, kutokuwa na hali ya kusamehe, uoga, kuhisi kushindwa na hali ya kuchanganyikiwa kifikra. Mwisho wa kunukuu.
Leo hii wataalamu wa elimunafsia na wanasaikolojia wamegundua njia nyingi za kuzifanya fikra za mwanadamu pamoja na nafsi yake vibaki kuwa salama kwa kutumia dini pamoja na mafunzo yake. Wanaamini kuwa, kumuamini Mwenyezi Mungu ni nguvu isiyo ya kawaida ambayo humuongezea mja nguvu za kimaanawi na hivyo kumfanya aweze kustahamili na kuvumilia machungu na taabu za maisha.
Mwanadamu ambaye ana imani juu ya Mwenyezi Mungu kawaida huwa hashindwi kukabiliana na misukosuko ya maisha ambayo kwa kawaida hupanda na kushuka na daima huwa na nguvu ya kiroho ya kukabiliana na pirika pirika hizo za maisha. Imani ni rasilimali na kitega uchumi muhimu katika maisha. Watu wengi wanaonufaika na neema hiyo adhimu huishi katika hali ya utulivu na saada maishani. Watu wa aina hiyo huamini kwamba, usalama na uzima wa mwili, roho na hata kuwa na umri mrefu hutokana na imani yao juu ya Mwenyezi Mungu muumba, suala ambalo huwapatia pia matumaini na uchangamfu katika maisha yao ya kila siku na kuwaepusha na hali ya masononeko, unyonge na mchanganyiko wa mawazo na fikra. Carl Gustav Yung anasema katika kitabu chake cha Saikolojia na Dini kuwa, Mtu mwenye kuwa na tajiriba hii (imani) katika maisha yake basi ni mtu mwenye kito cha thamani, kwani imani ni chemchemi ya maisha, harakati na uzuri.
Ustadh Shahidi Mutahhari mmoja wa wanafikra wakubwa na mashuhuri wa Kiirani anasema, watu wenye kushikamana na dini vyovyote watakavyokuwa na imani thabiti, huwa mbali na maradhi ya kinafsi. Miongoni mwa athari za imani ya dini kwa mwanadamu ni utulivu. Imani ya dini huzifanya roho na nyoyo zenye wasi wasi kutokana na matukio mbalimbali katika ulimwengu huu kupata utulivu. Mwisho wa kunukuu. Kwa mtazamo wa mtu mwenye imani na maarifa ya kumtambua Allah, ulimwengu si mjumuiko wa vitu na sheria bali umbo linalobeba maana na malengo maalumu. Mwenye kumuabudu Mwenyezi Mungu hali ya kuwa na elimu na ufahamu.
Wapenzi wasomaji katika makala zetu zijazo tutazungumzia athari za imani juu ya Mwenyezi Mungu kinafsi na kifikra na katika mwenendo na miamala ya mwanadamu. Kwa leo Makala yetu ya Mwandamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi inaishia hapa, jiungeni nami katika makala nyingine. Mnaweza kututumia maoni yenu kupitia barua pepe yetu ya This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. .
 

Tuma maoni yako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …