Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Aprili 2008 15:11

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (4)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu


Assalaam Alaykum wapenzi wasomaji. Makala yetu iliyopita iliishia kwa kukusimulieni kisa cha Rosellan Malchonov raia wa Russia ambaye kwa muda fulani aliamua kujitenga na dini na kutofikiria hata kidogo juu ya suala la kuweko Muumba wa ulimwengu huu.
Hata hivyo, mwishowe alirejea katika dini baada ya kujikuta kwamba, roho yake inahitajia chakula ambacho si kingine bali ni mawaidha na mafundisho ya kidini. Tulisimulia pia katika makala iliyopita jinsi alivyofanikiwa siku moja kufungua redio na kupata idhaa moja ya Kirusi iliyokuwa na kipindi cha kidini na kuvutiwa na vipindi hivyo na mwishowe kuifahamu dini tukufu ya Kiislamu kupitia vipindi hivyo.
Katika makala yetu ya leo tutaendele kustafidi na uzoefu pamoja na tajiriba yake. Rosellen Malchonov ambaye alikuwa ameathirika mno na mafundisho ya kimaanawi ya dini tukufu ya Kiislamu anaendelea kusimulia uzoefu na tajiriba yake kwa kusema, suala la tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu ni uhakika na ukweli mzuri kabisa nilioutambua. Ilikuwa fakhari kubwa mno kwangu kuutambua na kuudiriki ukweli na uhakika huo aali na nikaufanya uhakika huo kuwa nguzo ya kila kitu katika maisha yangu. Kila siku nikawa ninatafakari na kutadabari juu ya viumbe wa Mwenyezi Mungu na hapo ndipo nilipokuwa na yakini kuliko hapo kabla kwamba, kuzunguka kwa Dunia kuna malengo na hakufanyiki hivi hivi tu bila ya malengo maalumu. Basi mimi pia yanipasa katika maisha yangu kuwa na malengo na njia maalumu za kuendesha maisha yangu. Muujiza huo wa imani ulikuwa katika uwepo wangu na kwamba, kwa kumtaja Mwenyezi Mungu kila siku, nilikuwa nikipata nguvu mpya na nilikuwa nikitafakari juu ya malengo ambayo Mwenyezi Mungu ameyaweka kwa ajili ya mja kufikia saada na ukamilifu. Mwisho wa Kunukuu.
Tajiriba inaonyesha kwamba, kutekeleza kwa vitendo mafunzo ya Mitume na Wajumbe wa Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa njia zinazosaidia katika kuifanya nafsi na fikra za mwanadamu kuwa salama na mwishowe kumpatia saada na ufanisi. Misingi na njia zilizoainishwa na manabii kwa ajili ya kufikia ukamilifu na saada ya milele, nayo humuandalia mja mazingira ya kumfanya asalimike na matatizo ya mfadhaiko, jakamoyo, mvurugiko wa mawazo na matatizo ya kinafsi.
Hapana shaka kuwa, kujitenga na mafundisho pamoja na maamrisho ya dini ndiko kunakomfanya mwanadamu akabiliwe na matatizo ya kifikra na kinafsi na hivyo kumfanya aishi katika hali ya fukuto, masononeko na kukata tamaa. Kwa maneno mengine ni kuwa, kuacha mafundisho ya dini ni mambo ambayo humfanya mwanadamu akabiliwe na matatizo chungu tele yakiwemo ya matatizo ya kinafsi hali ambayo humfanya aanze kusumbuliwa na hali ya mfadhaiko, mvurugiko wa mawazo jambo ambalo kwa hakika humfanya mja huyo ajihisi si lolote si chochote na hivyo kuishi kwa kukata tamaa, bila malengo wala matumaini. Imani juu ya Mwenyezi Mungu muumba wa kila kitu, kudumu katika kumtaja na kutekeleza ibada ni miongoni mwa nukta muhimu za pamoja na za msingi katika dini za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kumfanya mja awe na utulivu wa kiroho.
William James mmoja wa wanafalsafa na wanasaikolojia mashuhuri anasema kuhusiana na njia za kuufikia utulivu na sifa za batini kama ninavyomnukuu.'' Wakati tutakapokuwa na mapenzi ya kweli kwa Mwenyezi Mungu muumba wa ulimwengu huu, basi uoga na ile hali ya ujeuri na kujiona itaondoka na badala yake tutapata utulivu na kuwa na sifa nzuri za batini. Kila lahadha itakapokuwa ikipita roho itakuwa ikipata nguvu na uchangamfu. Inaonekana kuwa, milango yote imefunguliwa kwa ajili yetu na njia ziko wazi kwa ajili yetu pia. Ni katika kivuli cha maanawi kama hicho ambapo mwanadamu huelekea katika mafanikio na saada ya kweli ambayo ni ya juu zaidi kuliko masuala ya kimaada ambayo huja na kwisha haraka wakati mwingine bila hata ya mja kuhisi. Mwisho wa kunukuu.
Inaonekana kuwa utulivu wa ndani au wa kinafsi ni tamanio na hitajio la daima la mwanadamu wa leo. Tajiriba inaonyesha kuwa, kila jamii inavyozidi kujitenga na dini na mienendo pamoja na maadili bora, ndipo pia maradhi na matatizo ya kinafsi, masumbufu ya rohoni na majakamoyo yanapoongezeka na hivyo kuharibu fikra na nafsi salama za wanajamii.
Kuna haja ya kuzingatiwa masuala ambayo yana taathira katika shakhsia ya mtu kama kinga ya awali kabisa kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi nafsi na masumbuko ya moyoni. Vyuo vyote vya kutibu matatizo ya kinafsi na kisaikolojia vinaamini kwamba, kuondokana mwanadamu na masumbuko ya kinafsi na mvurugiko wa mawazo na kupatikana amani na usalama katika nafsi yake humfanya mja atatue matatizo mengi ya kinafsi yanayomkabili. Kama ambavyo inasemekana kuwa, jitihada za pupa katika kuendeleza sekta ya viwanda, kujenga miji na kuwa na maisha ya kiteknolojia na ya kisasa yaani maisha ya kutegemea vyombo vya mashine kumekuwa na natija hasi na mbaya katika uzima na usalama wa kiroho wa wanadamu na hivyo kumfanya mwanadamu huyu akabiliwe na matatizo mapya ambayo hayakuwepo hapo kabla. Kwa maana kwamba, maisha katika miji mikuu ambayo imejaa majumba makubwa makubwa na magari mengi yanayoambatana na msongamano mkubwa katika barabara hizo zimewafanya wakazi wa miji hiyo kukabiliwa na matatizo ambayo huwezi kuyapata katika maeneo ya vijini.
Leo hii utapata kuwa katika miji mikubwa licha ya kuweko hayo yanayotajwa kuwa ni maendeleo lakini wakazi wa miji hiyo mikubwa mbali na kukabiliwa na hatari ya kukumbwa na magonjwa kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na viwanda, wanajamii hao wanakabiliwa na hatari ya kuwa na maradhi ya masumbuko ya moyo, wasi wasi, mvurugiko wa mawazo na mengineyo kutokana na kusimama kwa muda mrefu barabarani kutokana na msongamano wa magari wakati wa kwenda makazini na kurejea majumbani mwao. Uchunguzi uliofanywa na watafiti wa masuala ya kisaikolojia unaonyesha kwamba, endapo mja atazingatia na kufuata mafundisho ya dini na kuyafanya kuwa kioo cha maisha yake, basi jambo hilo humsadia kumpunguzia mfadhaiko, mvurugiko wa mawazo, talaka na hata kesi za kujiua watu.
 Tuma maoni yako

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …