Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 22 Aprili 2008 15:09

Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi (3)

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu


Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo. Hii ni sehemu ya tatu ya mfululizo wa makala za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya Kinafsi. Ni matumaini yetu mtafaidika na makala hii. Karibuni.
Leo hii tunaishi katika zama ambazo mwanadamu anaonekana kumili na kuzingatia zaidi mambo ya kimaada na kuacha masuala ya kimaanawi ambayo kimsingi ndiyo ambayo humpatia mja saada na ufanisi humu duniani na kesho akhera. Wimbi la kumili katika masuala ya kimaada na harakati kushindana kukusanya mali, kwa upande mmoja na kutofanikiwa mtu kuvipata vitu alivyokusudia kwa upande wa pili ni jambo ambalo huongeza mashinikizo ya kiroho na kinafsi kwa mja huyo na kumfanya awe katika hatari ya kukabiliwa na matatizo ya kinafsi na mvurugiko wa kimawazo.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya kinafsi wanaamini kwamba, mwanadamu akiwa na matumaini kupita kiasi ya kupata kitu fulani au kupiga hatua katika jambo fulani, hukumbwa na hali ya mfadhaiko na masumbuko ya kinafsi pindi anapolikosa jambo hilo au pindi anaposhindwa kuifikia hatua hiyo. Hapana shaka kuwa, vitu vya kimaada licha ya uzuri wa kidhahiri ulivyonavyo katu haviwezi kukidhi mahitaji ya ndani ya kinafsi na kiroho ya mwanadamu na wala haviwezi kumpatia utulivu wa kweli.
Na ndio maana leo tunaweza kuwajibu wale wenye mtazamo kwamba, ukiwa na mali unakuwa na utulivu kwa kuwaambia kwamba, kwa nini basi leo hii tunapata matajiri wengi hawana utulivu wa kweli wa kiroho na kinafsi. Baadhi ya wanadamu husoneneka na kupatwa na wasi wasi wa kinafsi kutokana na kukumbwa na hofu ya kuogopa kupoteza vitu wanavyovimiliki hali ambayo iko kwa matajiri na wengine hukumbwa na hali hiyo kutokana na kuvikosa vitu hivyo. Hapana shaka kwamba, kuwa na mtazamo wa kimantiki na kutazama mambo kwa uhakika wake humsaidia mja maishani na kuleta uwiano katika kukidhi mahitaji yake ya kimaada na kimaanawi na hivyo kumpunguzia matatizo mengi ya kimaisha yanayomkabili.
Hapana shaka kuwa, moja kati ya mambo ya lazima kwa ajili ya kuifanya nafsi kuwa salama ni kuwa na malengo na njia zifaazo katika kuendesha maisha. Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia na wananadharia wa mienendo wanaamini kwamba, dini ina nafasi muhimu katika kuboresha maisha ya mwanadamu. Kwa mtazamo wao wanaona kwamba, kuwa na udini moja kwa moja au kwa njia isiyokuwa ya moja kwa moja kunasaidia katika kuifaya nafsi na fikra zibaki kuwa salama.
Adabu, heshima na matukufu ya kijamii hasa imani na itikadi za kidini ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoonyesha shakhsia ya mtu. Taathira kubwa ya dini katika maisha ya mtu imewafanya baadhi ya watafiti na wachunguzi waliobobea katika taaluma ya saikolojia na matatizo ya kinafsi wafahamu na kugundua mambo mapya kuhusiana na matatizo ya kinafsi yanayomkabili mwanadamu katika zama zetu za leo.
Wakiwa na lengo la kutafuta matibabu kamili na bora zaidi ya kiroho na kimwili, wataalamu hao wamekuwa wakistafidi na mafunzo pamoja na maelekezo ya dini. Utafiti tofauti uliofanywa katika miongo kadhaa ya hivi karibuni unaonyesha kuwa, kwa kustafidi na dini inawezekana kupunguzwa maradhi ya masumbuko ya kimawazo na matatizo ya kinafsi. Utafiti mpya unaonyesha kuwa, watu ambao wanamtegemea Mwenyezi Mungu baada ya kutambua kwamba, kuna Muumba wa kila kitu, hupata ladha ya maisha, na ukiwatazama unaona kuwa ni wazima wa nafsi, akili na fikra ukiwalinganisha na watu wengine. Benjamin Rush mmoja wa wanasaikolojia anasema hivi baada ya kufanya utafiti kuhusiana na suala hilo.
''Dini na masuala ya kimaanawi yana umuhimu mkubwa katika kulea na kuifanya roho iwe salama kama hewa ilivyo na umuhimu kwa ajili ya kupumua. Dini humsaidia mwanadamu kufahamu vizuri zaidi maana ya matukio maishani hasa matukio yanayohuzunisha na yanayoleta masumbuko moyoni pamoja na hali ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu. Profesa Benjamin anaendelea kusema kwamba, dini humfundisha mwanadamu vipi ataweza kwenda sambamba na ulimwengu huu mkubwa na vilivyomo. Hali hiyo ya kwenda sambamba na matukio hayo humpatia mwanadamu utulivu ndani ya roho. Mwisho wa kunukuu.
Pengine si vibaya pia kusikia uzoefu na tajiriba ya watu ambao walikuwa mbali na dini na mafundisho yake. Rosellen Malchonov raia wa Russia ambaye kwa muda fulani aliamua kujitenga na dini anasema kama ninavyomnukuu. ''Kila mtu itafika kipindi atahitajia chakula cha roho iwe ni hivi sasa au baadaye. Hali kama hiyo imewahi kunipata mimi na nikawa na mapenzi na natija ya hali hiyo ambayo ilikuwa ni kuirejea dini''. Rosellan anaendelea kusimulia kipindi chake cha kujitenga na dini kwa kusema, mimi nilikuwa sifikirii hata juu ya kuweko Mwenyezi Mungu. Kidogo kidogo nikaanza kuhisi kwamba, maisha hayana maana yoyote kwangu. Sikuwa na malengo wala hamu ya kuendelea kuish tena. Kuna wakati masumbuko ya moyo na kifikra yalikuwa yakiniandama kiasi kwamba, nilikuwa nikidhani nimefikia mwisho wa maisha yangu. Lakini jioni moja wakati jua linaelekea kuzama, nilijipata nimefungua redio kwa sadfa tu na nikapata stesheni moja iliyokuwa na kipindi kilichokuwa kikizungumzia masuala ya dini kwa lugha ya Kirusi. Nikatulia na kuanza kusikiliza kipindi hicho. Kwa kweli maneno ya mtangazaji wa kipindi hicho yalikuwa mapya kwangu.
Ghafla nikahisi kama nuru imeingia katika akili na roho yangu. Kumbe kile nilichokuwa nikikisikia kilikuwa kikiitakasa roho na akili yangu na kila siku nikawa napenda mno kusikiliza kipindi hicho kilichokuwa kikizungumzia dini ya Kiislamu. Hivyo ndivyo nilivyoijua dini ya Kiislamu. Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasomaji kwa leo tunakomea hapa jiungeni nami juma lijalo katika mfululizo mwingine wa makala hizi za Mwanadamu, Dini na Suluhisho la Matatizo ya
Kinafsi. Kwa herini. Mnaweza kututumia maoni yenu kupitia barua pepe yetu ya This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. .

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …