Kamanda Lamidi Adeosun kutoka Nigeria ameeleza kusikitisha kwake na kutowajibika ipasavyo nchi zinazoshiriki katika operesheni ya kupambana na kundi la Boko Haram na kusema nchi zote washiriki zinapaswa kutekeleza ahadi zao.
Lamidi Adeosun ambaye amewasili nchini Niger amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mahamadou Issoufou wa nchi hiyo na vilevile kamanda wa jeshi la nchi hiyo, Seynu Garba. Amesisitiza kuwa kwa sasa wapiganaji wa kundi la Boko Haram hawadhibiti mji au kijiji chochote na kwamba wamejificha katika maeneo ya mbali ya kandokando ya Ziwa Chad.
Kushadidi kwa mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram na kufeli kwa jeshi la Nigeria kukabiliana na kundi hilo kumewalazimisha viongozi wa nchi za eneo hilo kutoa wito wa kuwepo ushirikiano wa kikanda na kuwajibika zaidi katika suala hilo.
Wakati huo huo kundi la Action on Armed Violence (AOAV) lenye makao yake London nchini Uingereza limeripoti kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi ya kundi la Boko Haram imeongezeka katika mwaka uliopita nchini Nigeria. Ripoti ya AOAV imesema kuwa, idadi ya watu waliouawa na waliojeruhiwa na kundi la Boko Haram mwaka 2015 ilikuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake na kwamba utumiaji wa watu wanaojilipua kwa mabomu wa kundi hilo umeongezeka kwa asilimia 167. Ripoti ya taasisi hiyo imesema Nigeria unashika nafasi ya nne kati ya nchi zilizokuwa na wahanga wengi zaidi na majeruhi wa mashambulizi ya kigaidi katika mwaka 2015 ikizifuatia nchi za Syria, Yemen na Iraq, na Afghanistan inashika nafasi ya tano.
Kwa sasa makundi mengi ya kigaidi kama Boko Haram, al Shabab, al Murabitun, al Qaida na mengineyo yanafanya mashambulizi ya mara kwa mara katika nchi za Kiafrika na harakati hizo zinatishia usalama wa kikanda na kimataifa. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Mkutano wa Usalama wa Munich uliofanyika nchini Ethiopia ukajadili harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika na njia ya kukabiliana nayo.
Mkuu wa Mkutano wa Munich, Wolfgang Ischinger alisema katika mkutano huo wa Addis Ababa kwamba, mbali na masuala ya ustawi na misaada ya kibinadamu kwa bara la Afrika, kuna udharura wa kujadili suala la usalama barani Afrika.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom alisema katika mkutano huo kwamba, tofauti na miaka ya huko nyuma, matatizo ya Afrika na masuala ya usalama hayaishii barani Afrika na kwamba changamoto hizo zimevuka mipaka ya Afrika. Adhanom amesisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano kati ya Afrika na Ulaya kwa ajili ya kupanga stratijia kamili ya kupunguza misimamo mikali na kuimarisha uchumi na usalama.