Katika kudumishwa uchochezi huo Bahrain na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu hivi karibuni zimetoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran. Katika toleo lake la leo tovuti ya Gulf News imesema katika moja ya makala zake kwamba Mfalme Hamad bin Isah Aal Khalifa wa Bahrain na Mfalme wa VI wa Morocco wameituhumu Iran kuwa inaingilia mambo ya ndani ya Bahrain na nchi nyingine za Kiarabu pamoja na kuunga mkono ugaidi. Madai kama hayo yalitolewa siku ya Jumanne na mfalme huyohuyo wa Bahrain alipokutana na Rais Abdulfattah as-Sisi wa Misri huko Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Katika mazungumzo hayo mfalme huyo wa Bahrain aliunga mkono pendekezo la kuundwa jeshi la pamoja la nchi za Kiarabu kwa lengo la kupambana na kile alichokitaja kuwa tishio la usalama katika eneo.
Matamshi hayo kwa hakika yanaashiria kuwepo mpango wa muda mrefu wa kukabiliana na Iran ambao ulijadiliwa na kuzinduliwa huko Riyadh Saudia katika kikao cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi tarehe 22 mwezi huu, ambacho kilihudhuriwa pia na Rais Barack Obama wa Marekani. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita vikao vingi vimefanyika katika kiwango cha mawaziri wa Marekani na wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Ujemi kwa lengo la kufuatilia masuala ya kiusalama yaliyopitishwa na pande mbili hizo katika kikao cha Camp David nchini Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kikao hicho kilichofanyika mwezi Mei mwaka uliopita, Marekani na washirika wake katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ambazo ni nchi za Saudi Arabia, Imarati, Kuwait, Oman, Qatar na Bahrain, waliahidi kushirikiana kwa karibu kwa madhumuni ya kubuni muungano madhubuti wa kijeshi kwa lengo la kukabiliana na kile kilichotajwa kuwa changamoto za kieneo. Tarehe 20 mwezi huu pia Waziri wa Ulinzi wa Marekani alikutana na mawaziri wenzake wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi huko Riyadh Saudia na kusisitiza udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa kijeshi kati ya pande hizo dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa mpango uliopitishwa kwenye kikao hicho, kikao maalumu cha Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kitabuniwa na kupewa mafunzo ya kijeshi na askari wa Marekani. Ni wazi kuwa mpango huo utaipa Marekani kibali cha kuendelea kujiimarisha kijeshi katika eneo nyeti la Ghuba ya Uajemi. Ushirikiano huo wa kiusalama kwa shabaha ya kukabiliana na kile kinachotajwa kuwa changamoto za kiusalama katika eneo hivi sasa umejikita katika suala la kukabiliana na uwezo wa makombora ya Iran. Kuhusiana na suala hilo Marekani imezihakikishia nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwamba itaharakisha na kuzipa nchi hizo mfumo wa onyo la mapema dhidi ya makombora ya balistiki ili kukabiliana na kile kinachosemekana kuwa ni tishio la kieneo kutoka Iran.
Nchi za Ghuba ya Uajemi na hasa Saudi Arabia na Bahrain zinakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na makosa makubwa yaliyofanyika katika siasa zao. Kwa msingi huo zinafanya kila linalowezekana ili kufunika ukweli huo wa mambo kwa kuituhumu Iran kuwa ndiyo inayoingilia masuala yao ya ndani. Kwa madai hayo yasiyo na msingi wowote na kwa lengo la kudumisha stratijia hiyo ya kuipaka matope Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Saudia katika hatua ya kwanza ilituma askari jeshi wake huko Bahrain kwa lengo la kukandamiza maandamano na malalamiko halali ya watu wa nchi hiyo dhidi ya utawala dhalimu wa nchi hiyo unaokanyaga wazi haki zao za kimsingi na kisha kuivamia kijeshi Yemen kwa kisingizio hichohicho. Wakati huohuo utawala wa Aal Soud uliamua kuyapa misaada mikubwa ya kifedha na kijeshi makundi ya kigaidi, kitakfiri na Kizayuni yanayofanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya watu na serikali halali za Syria na Iraq na hivyo kuzua migogoro mikubwa ya kiusalama katika nchi hizo. Licha ya kutekelezwa siasa hizo hatari dhidi ya mataifa ya Kiislamu ya eneo lakini ni wazi kuwa hazitafua dafu bali zitazidisha tu migogoro katika eneo na hivyo kuharakisha kasi ya Marekani na utawala haramu wa Israel kufikia malengo yao haramu katika eneo. Kwa vyovyote vile nchi hizo za Kiarabu bila shaka ndizo zitakazokuwa washindwa halisi na wa mwisho wa stratijia hiyo ya kiusalama na kijeshi katika eneo.