Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 25 Aprili 2016 11:22

Kuendelea kusalia Darfur na majimbo matano kama ilivyokuwa awali

Kuendelea kusalia Darfur na majimbo matano kama ilivyokuwa awali
Kwa mujibu wa matokeo ya kura ya maoni ya kuainisha mustakbali wa Darfur, eneo hilo litaendelea kusalia na majimbo yake matano kama ilivyokuwa hapo zamani.

Matokeo ya kura ya maoni yaliyotangazwa na serikali ya Sudan hapo juzi Jumamosi, yameonyesha kwamba, asilimia 97 ya wananchi wa nchi hiyo wameamua eneo hilo la machafuko ya muda mrefu na ambalo liko magharibi mwa nchi hiyo liendelee na utaratibu wake wa sasa wa kiidara na chini ya majimbo yake matano. Kabla ya hapo pia weledi wa mambo walikuwa wametabiri kuwa, kupitia kura hiyo ya maoni iliyodumu kwa muda wa siku tatu, Darfur ingeendelea kusalia katika mfumo wa majimbo matano, mfumo ambao tangu awali ulikuwa ukipendewa na chama tawala cha Rais Omar al-Bashir wa Sudan. Kwa mujibu wa weledi hao wa mambo, Darfur kusalia katika mfumo huo, kunatoa fursa kwa serikali ya Khartoum kuzidisha udhibiti wake huko Darfur. Kura hiyo ya maoni imesusiwa na wapinzani wa serikali ya nchi hiyo. Mrengo wa upinzani unaamini kwamba, hatua ya serikali ya Sudan ya kuligawa eneo la Darfur katika maeneo matatu hapo mwaka 1994 na kisha kuligawa tena katika majimbo matano baadaye, ulikuwa mwanzo wa kuibuliwa machafuko ya mwaka 2003 sanjari na kushadidisha udhibiti wa serikali katika majimbo hayo. Itakumbukwa kuwa, kati ya tarehe 11 hadi 13 za mwezi huu, raia wa Sudan walishiriki katika kura ya maoni ambayo ilikuwa na lengo la ima majimbo ya Darfur kujitenga au kubakia katika mfumo wa hivi sasa. Mapigano katika eneo la Darfur yaliibuka mwaka 2003 yakiyahusisha makabila ya wabeba silaha yaliyokuwa yakiituhumu serikali kwa kufanya ubaguzi dhidi yao. Mapigano hayo hadi sasa yamesababisha zaidi ya watu laki tatu kuuawa na zaidi ya wengine milioni mbili na laki sita kuwa wakimbizi. Siku chache zilizopita, Rais Omar al-Bashir wa Sudan alitangaza kuwa, atakubaliana na matokeo yoyote juu ya hatima ya eneo hilo. Akihutubia bunge la nchi hiyo rais huyo alisema kuwa, chaguo la wakazi wa Darfur ni lenye kuheshimiwa na kwamba ni suala la lazima kukubali matokeo ya kura hiyo. Aidha alilipongeza jeshi la Sudan kwa kudumisha usalama na amani nchini humo na kusisitizia umuhimu wa jeshi hilo kufungamana na mwenendo huo. Matamshi ya Rais Omar al-Bashir yanakuja katika hali ambayo hadi sasa eneo la Darfur bado linashuhudia machafuko ya kila mara. Juzi askari wa Umoja wa Mataifa walioko eneo la Darfur walizitaka pande hasimu kujizuia kunako kuendeleza machafuko katika eneo hilo. Katika mapigano ya hivi karibuni ya kikabila huko magharibi mwa eneo hilo, askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wale wa Umoja wa Afrika "UNAMID' mbali na kutoa taarifa rasmi inayozitaka pande husika kusitisha mapigano, pia walizitaka pande hizo kudumisha usalama na uthabiti. Katika ripoti hiyo askari hao walielezea wasiwasi wao juu ya kushadidi machafuko ya hivi karibuni eneo la mashariki mwa Darfur likiwemo pia shambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi katika eneo hilo na kuzitaka pande zinazohusika katika kuchochea machafuko hayo kuacha mwenendo huo mara moja. Itakumbukwa kuwa, wiki iliyopita kundi moja la kikabila, lilivamia kambi ya jeshi eneo la Darfur mashariki na kuua watu watatu. Hii ni katika hali ambayo siku moja kabla ya kujiri hujuma hiyo watu 12 waliripotiwa kuuawa katika mapigano mengine ya kikabila eneo hilo. Mapigano hayo yamejiri ikiwa ni wiki moja imepita tangu serikali ya Sudan, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zikubaliane kuondoka kwa hatua askari hao wa kusimamia amani katika eneo la Darfur. Baada ya kikao cha pande tatu, Ali Al-Sadig Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Sudan aliwambia waandishi wa habari kwamba, imeamuliwa kufanyika kikao kingine hapo tarehe nane mwezi ujao wa Mei kwa ajili ya kuchunguza namna ya kuondoka askari hao wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo. Ameongeza kuwa, katika makubaliano hayo imeamuliwa askari hao waondoke eneo hilo kwa utulivu na kwa awamu.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …