Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 24 Aprili 2016 07:19

Amnesty I: Jeshi la Nigeria lilitekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu mwezi Disemba mwaka jana

Amnesty I: Jeshi la Nigeria lilitekeleza jinai za kutisha dhidi ya Waislamu mwezi Disemba mwaka jana
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limelitaja jeshi la Nigeria kuwa muhusika wa mauaji ya umati ya mamia ya Waislamu wa nchi hiyo.

Ripoti iliyotolewa na shirika hilo hapo jana imesema kuwa, mwezi Disemba mwaka jana Jeshi la Nigeria lilitumia mabavu na kuvunja sheria katika kuwaua kwa umati mamia ya Waislamu wasio na ulinzi wakiwamo wanawake na watoto wadogo, na kisha kufanya njama za kuficha jinai hizo. Ripoti ya Amnesty International pia imeongeza kuwa, madai ya jeshi la Nigeria kwamba wafuasi wa harakati ya Kiislamu inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria, walikuwa wamepanga njama za kumuua kamanda mkuu wa jeshi hilo, hayana msingi wowote na kwamba ni ya kujibunia tu. Itakumbukwa kuwa, kati ya tarehe 12 na 14 za mwezi Desemba mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika kituo cha Kiislamu cha mji wa Zaria na kuua zaidi ya watu 350. Shirika la Msamaha Duniani limewahoji watu kadhaa walioshuhudia jinai hiyo na kuongeza kuwa, askari hao wa jeshi la Nigeria walivamia pia kituo cha matibabu kilichokuwa kinamilikiwa na Waislamu hao ambapo kulikuwepo makumi ya wagonjwa waliokuwa wamelazwa kituoni hapo na kuwamiminia risasi bila ya huruma. Na kama hilo halitoshi, askari hao wasio na utu waliwachoma kwa moto baadhi ya watu waliokuwa hai katika tukio hilo na hivyo kupafanya mahala hapo kuwa na mandhari ya kutisha sana. Afisa mmoja wa Shirika la Msamaha Duniani amenukuliwa akisema kuwa, ni jambo lililo wazi kwamba, jeshi la nchi hiyo si tu kwamba lilitumia nguvu ya kupindukia dhidi ya watu wasio na ulinzi wala hatia, na hasa wanawake na watoto wadogo na kuua mamia katika hujuma hiyo ya kinyama, bali pia lilifanya njama za kujaribu kuficha jinai hiyo. Ripoti ya shirika hilo la haki za binaadamu duniani imetolewa baada ya kuhojiwa makumi ya watu walioshuhudia jinai hizo, familia za wahanga, wafanyakazi wa vituo vya afya vya eneo hilo na picha zilizochukuliwa na kusambazwa na satalaiti za eneo la kaburi la umati nchini humo. Uchunguzi wa Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International umetolewa ikiwa ni baada ya kiongozi mmoja wa jimbo la Kaduna nchini Nigeria kuieleza kamisheni ya uchunguzi kuwa, askari wa nchi hiyo waliizika kwa siri miili ya watu 347 katika kaburi moja. Aidha wiki iliyopita, kiongozi mwingine nchini humo alisema kuwa, jeshi hilo liliwazika watu 347 katika kaburi moja la umati na kwa kibali cha mahakama moja ya nchi hiyo. Jana Shirika la Habari la France Press likilinukuu shirika hilo, lilitangaza kuwa, askari wa Nigeria waliwaua kwa makusudi zaidi ya Waislamu wa Kishia 350 kwa kuwafyatulia risasi na kisha kuwazika katika kaburi moja la umati huku likiharibu kabisa nyaraka na ushahidi wa jinai hiyo. Hivi sasa na baada ya kutolewa ripoti hiyo, vyombo vya habari vya nchi hiyo ndio kwanza vimeanza kuakisi hali ya Waislamu wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Kabla ya hapo Mustafa Muhammad, mjumbe wa harakati ya Kiislamu nchini humo alinukuliwa akisema kuwa, hali ya Waislamu wa nchi hiyo imezidi kuwa mbaya hasa kwa kuwa serikali inawatambua Waislamu hao kuwa wapinzani wake. Muhammad ameongeza kuwa, mfumo unaotekelezwa na jeshi hilo ni wa kuwakandamiza Waislamu sanjari na kuwaweka katika mashinikizo mazito. Mwezi wa 12 mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika kituo cha Kiislamu cha mji wa Zaria kinachomilikiwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky baada ya kuwatuhumu kuwa walifunga njia ya msafara wa mkuu wa jeshi. Tangu wakati huo, kiongozi huyo wa kidini na mke wake wanaendelea kushikiliwa na jeshi hilo, na kwa mujibu wa baadhi ya duru za habari, afya yake imezidi kudhoofika. Kwa mara kadhaa jeshi hilo kwa kisingizio cha kupambana na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram, limekuwa likiwanyanyasa Waislamu nchini humo. Suala la msingi ni kwamba baada ya kutolewa ripoti ya Amnesty International Msemaji wa jeshi la nchi hiyo Sani Osman, ameitaja ripoti hiyo kuwa ya pupa na isiyo na itibari. Kwa hakika ripoti hiyo inaweza kuwa ushahidi tosha wa kuadhibiwa wahusika wa jinai hiyo dhidi ya Waislamu sanjari na kuzilipa fidia familia za wahanga wake.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …