Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 23 Aprili 2016 17:08

Rais Idriss Déby wa Chad atangazwa kuwa mshindi wa urais Chad

Rais Idriss Déby wa Chad atangazwa kuwa mshindi wa urais Chad
Jana Ijumaa Rais Idriss Déby alitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Chad kuwa mshindi wa uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo na hivyo kupata fursa ya kuendelea kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa tano mfululizo. Kwa mujibu wa tume hiyo ya uchaguzi, Rais Déby ameibuka mshindi kwa kupata asilimia 60 ya kura, huku mpinzani wake Saleh Kebzabo akipata asilimia 12 ya kura hizo.

Tayari Kebzebo amepinga matokeo hayo akisema kuwa, kulifanyika uchakachuaji mkubwa wa kura kwa maslahi ya Rais Déby. Wiki iliyopita waangalizi wa Umoja wa Afrika kwenye uchaguzi huo walinukuliwa wakisema kuwa, uchaguzi nchini Chad ulifanyika katika anga huru na salama. Uchaguzi mkuu huo ulifanyika tarehe 10 ya mwezi huu, ambapo baraza la kusimamia katiba linatakiwa kutangaza matokeo ya mwisho kufikia tarehe nane ya mwezi Mei ujao. Kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo kunajiri katika hali ambayo mivutano ya kisiasa nchini Chad ilianza muda mrefu uliopita ambapo imeshika kasi katika miezi ya hivi karibuni na kusababisha mapigano na utumiaji mabavu wa polisi dhidi ya wapinzani. Kwa muda sasa wapinzani wamekuwa wakikituhumu chama tawala cha Rais Idriss Déby kwa kupanga njama za kufanya wizi kwa ajili ya kumbakisha madarakani rais huo mkongwe. Itafahamika kuwa Rais Déby amekuwa madarakani tangu mwaka 1990, baada ya kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, dikteta Hissène Habré. Mwaka 2004 rais huyo alibadili katiba na kuondoa kipengee cha mihula miwili ya kuhudumu madarakani. Katika uchaguzi uliopita pia, wapinzani wake wa kisiasa walipinga matokeo ya uchaguzi huku wakiendeleza kampeni ya kupinga kugombea tena Rais Déby kwenye uchaguzi wa mwaka huu. Licha ya maandamano na migomo mbalimbali iliyofanyika miezi ya hivi karibuni nchini Chad ya kumtaka rais huyo kutogombea tena, bado Déby aliendelea kusisitiza kuwa, Chad ingali inamuhitajia yeye na kwamba ilikuwa lazima agombee tena. Wapinzani wanamtuhumu rais huyo kwa kufanya udikteta katika ulingo wa kisiasa ambapo amekuwa akiwakandamiza wapinzani wake kwa lengo la kutaka kuendelea kusalia zaidi madarakani. Kuongezeka matatizo ya kiuchumi nchini Chad, ufisadi wa serikali na ukandamizaji mkubwa wa kisiasa dhidi ya vyombo vya habari na wanaharakati wa masuala ya kiraia, ni mambo mengine yaliyowasukuma wapinzani kusisitizia umuhimu wa kupambana na Rais Déby. Katika upande mwingine baadhi ya weledi wa mambo wameelezea uungaji mkono wa nyuma ya pazia wa Ufaransa kwa mwanasiasa huyo. Hii ni kusema kuwa, licha ya kutajwa uchaguzi wa hivi karibuni nchini Chad, kuwa uliogubikwa na uchakachuaji mkubwa, lakini viongozi wa Ufaransa wameyapokea matokeo ya uchaguzi huo kwa mikono miwili. Mazungumzo kati ya serikali na asasi za kiraia nchini Chad yaliyoitishwa kufuatia kushadidi mgogoro na malalamiko ya kisiasa ya wiki moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa tarehe 10 mwezi huu yaliharibika punde baada ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuwatia mbaroni wanaharakati wanne wa asasi hizo. Ni kwa ajili hiyo ndipo mgogoro wa kisiasa ukashika kasi zaidi ndani ya taifa hilo la magharibi mwa Afrika. Hivi sasa na sanjari na kutangazwa Rais Idriss Déby kuwa mshindi wa uchaguzi uliopita, amewataka wafuasi wake kuheshimu sheria kama ambavyo amewataka pia kusherehekea ushindi wake bila ya kuvunja sheria na kulinda amani hasa baada ya baraza la katiba kutangaza matokeo ya mwishi mwezi ujao. Licha ya kugunduliwa akiba kubwa ya mafuta hapo mwaka 2006 mchini humo, lakini idadi kubwa ya raia wa taifa hilo wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa. Juhudi za kuboresha hali ya uchumi na kupunguzwa kiwango cha ukosefu wa nafasi za kazi ni miongoni mwa matarajio ya raia wengi wa nchi hiyo. Katika kampeni zake, Rais Déby aliahidi kuwa, kama angechaguliwa kwa mara nyingine kuiongoza nchi hiyo, angefanyia marekebisho katiba na kurejesha tena kipengee cha ukomo wa uongozi kwenye katiba hiyo. Hivi sasa inaonekana kuwa katika kutekeleza ahadi zake rais huyo atakabiliwa na kibarua kigumu mno katika kipindi hiki cha awamu ya tano ya uongozi wake nchini Chad.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …