Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatano, 20 Aprili 2016 19:12

Waasi wa Nigeria watishia kuhujumu vituo vya mafuta

Waasi wa Nigeria watishia kuhujumu vituo vya mafuta
Waasi wa eneo lenye utajiri wa mafuta la Niger Delta kusini mwa Nigeria wametishia kwamba watazidisha mashambulizi yao dhidi mabomba na vituo vya uzalishaji mafuta ghafi ya petroli nchini humo.

Kundi linalojiita Walipizaji Kisasi wa Niger Delta limetoa taarifa likimkosoa Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ambaye limesema anajali visima vya mafuta kuliko maisha ya wakazi wa Niger Delta. Kundi hilo pia limetangaza kuwa ndilo lililoshambulia mabomba ya mafuta chini ya bahari hapo mwezi Februari mwaka huu. Shambulizi hilo liliilazimisha kampuni kubwa ya mafuta ya Shell kusimamisha uuzaji nje bidhaa hiyo kwa wiki kadhaa.

Tishio la kundi hilo la 'Walipizaji Kisasi wa Niger Delta', limetoa tishio hilo katika hali ambayo siku chache zilizopita Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria alisema kuwa atawaadhibu vikali watu waovu wanaoharibu mabomba ya mafuta ghafi.

Aidha alisema ataunda kikosi cha kudumu kitakachokuwa na jukumu la kulinda mabomba na vituo vya uzalishaji mafuta nchini humo.

Eneo la Niger Delta liko kusini mwa Nigeria na lina majimbo tisa ambayo yanaongoza kwa hifadhi ya mafuta nchini humo.

Ni miongo minne sasa tokea Nigeria ivumbue mafuta na ianze kuyachimba na kuyauza katika masoko ya kimataifa. Lakini Wanigeria hawajafaidika ipasavyo na utajiri huo wa kitaifa wa nchi yao.

Nigeria ndiye mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ghafi ya petroli barani Afrika. Lakini wakaazi takribani milioni 186 wa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika bado wanaishi katika umasikini mkubwa. Kuna kiwango kikubwa cha umasikini katika majimbo ya eneo la Niger Delta hasa katika Bandari ya Harcourt ambayo ni kituo kikuu cha kusafirisha mafuta ya Nigeria katika soko la kimataifa.

Weledi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, mashirika ya uchimbaji mafuta ya nchi za Magharibi kama Shirika la Uingereza na Uholanzi la Shell na Shirika la Marekani la Chevron, mashirika ambayo yamekuwepo Niger Delta tangu mafuta yaanze kuchimbwa eneo hilo, ndio waporaji wakuu wa utajiri wa kitaifa wa watu wa Nigeria.

Shirika la Exxon Mobile pia sasa limejiunga na mashirika hayo mawili katika uporaji wa utajiri wa Nigeria. Mashirika hayo yote matatu yanatuhumiwa na watu wa Niger Delta kwa kuhusika na uporaji mkubwa wa utajiri wa eneo hilo.

Hali kadhalika kuenea na kukita mizizi ufisadi serikalini ni ukweli mchungu kwa watu wa Nigeria. Pamoja na kuwa kumeshuhudiwa ustawi wa kiuchumi nchini Nigeria, ufisadi umepelekea kukosekana uadilifu na usawa katika kugawa utajiri miongoni mwa Wanigeria wote hasa eneo la Niger Delta. Ufisadi miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu serikalini ni jambo ambao limepelekea kuenea utoaji rushwa na ufisadi katika sekta zote za jamii ya Nigeria.

Kwingineko, makabila ya waliowachache Nigeria kama vile Ogoni na Ijaw katika maeneo wanayoishi watu masikini Niger Delta yameanzisha mwamko wa kutetea haki zao za kijamii na kisiasa.

Mgogoro wa eneo la mafuta la Niger Delta ulianza mwaka 2004 ambapo kuliibuka makundi kadhaa ya waasi. Waasi hao wakiwemo wale waliojulikana kama MEND walitishia kushambulia na kuharibu vituo vyote vya uzalisha mafuta ghafi eneo hilo. Januari mwaka 2006 pia waasi wa Niger Delta walitishia kuwaua wafanyakazi wote wa vituo vya uzalishaji mafuta. Ingawa serikali ya wakati huo ya Nigeria mnamo mwaka 2007 ilitekeleza matakwa ya viongozi wa kabila la Ijaw, lakini tishio la uasi limeendelea kuwepo.

Baadhi ya makundi ya waasi yanaharibu mabomba na mafuta na pia kupora mafuta katika mabomba sambamba na kuharibu vituo vya uzalishaji mafuta na hata kuwateka nyara wafanyakazi wa kigeni wa mashirka ya mafuta ili kuishinikiza serikali.

Mwaka 2009 serikali ya Nigeria ilitoa msamaha jumla kwa waasi wote wa eneo hilo na hadi mwaka 2011 uasi ulipungua katika eneo hilo. Lakini tokea wakati huo hadi sasa kumeibuka makundi ya waasi kama kundi la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta ambayo yanaendelea kusababisha matatizo katika eneo hilo la kusini mwa Nigeria. Inaelekea kuwa, kuunda kikosi cha kudumu cha kulinda eneo hilo la kuchimba mafuta ni hatua isiyotosha na serikali inapaswa kutafuta njia muafaka ya kuwapa wenyeji wa eneo hilo haki zao za kijamii na kiuchumi.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …