Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 15 Aprili 2016 12:10

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na hali ngumu na ya kusikitisha ya Wapalestina wa Gaza

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na hali ngumu na ya kusikitisha ya Wapalestina wa Gaza
Baada ya kupita miaka 10, eneo la Ukanda wa Gaza, Palestina inayokaliwa kwa mabavu lingali limewekewa mzingiro na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel; na kutokana na kuendelea kukumbwa na mashambulio ya ndege za utawala huo ghasibu, fursa la kulikarabati na kulijenga upya eneo hilo imebaki kuwa ndoto.

Hali ngumu na ya kusikitisha waliyonayo wakazi wa Gaza na magofu yaliyosalia kutokana na uharbifu uliosababishwa na moto wa vita uliowashwa na Israel vimeshatolewa tahadhari na indhari mara kadhaa na Umoja wa Mataifa.

Katika wakati huu, ambapo viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) wanaendelea na kikao chao huko Istanbul, Uturuki, matarajio ya Wapalestina wa Gaza ni kuona kikao hicho kinachukua hatua za maana kuhakikisha mzingiro iliyowekewa Gaza unaondolewa.

Kamati ya serikali ya Palestina inayohusika na kadhia ya mzingiro dhidi ya Gaza imeitaka OIC ionyeshe radiamali na kuchukua hatua kuhusiana na hali mbaya inayowakabili wakazi wa eneo hilo. Kupitia taarifa yake, kamati hiyo imewaomba washiriki wa kikao cha 13 cha viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu walifanye suala la kuondolewa mzingiro wa Gaza kuwa ajenda namba moja ya kufanyiwa kazi na kikao hicho. Kuondolewa mzingiro dhidi ya Gaza kunahitaji kufunguliwa tena na Misri kivuko cha mpakani cha Rafah na kurahishisha uingiaji na utokaji kupitia kivuko hicho kwa wasafiri na hasa wanachuo na wagonjwa watokao Palestina.

Tayari Waziri Mkuu wa serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina Rami Hamdullah ameeleza wasiwasi uliopo kutokana na kupiga hatua za mwendo wa kujikongoja mchakato wa kuijenga upya Gaza baada ya hujuma za mtawalia za utawala wa Kizayuni; na ametahadharisha pia kuhusu maafa ya kibinadamu yaliyolikumba eneo hilo.

Eneo la Ukanda liliteketezwa na kuharibiwa vibaya sana kutokana na mashambulio ya angani, nchi kavu na baharini ya vita vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika msimu wa joto wa mwaka 2014. Mashambulio hayo yalilenga na kuharibu vibaya maeneo ya makazi ya watu, vituo vya usambazaji maji, kinu pekee cha ugavi wa umeme cha Gaza, hospitali, shule, mashamba na hata makao ya shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA). Licha ya kupita miaka miwili, mzingiro dhidi ya Gaza ungali unaendelea huku utawala haramu wa Israel ukizuia kupelekwa huko vifaa vya ujenzi na zana zinazohitajika kwa ajili ya kulijenga upya eneo hilo.

Gaza ingali inahitaji misaada ya kimataifa kwa ajili ya kulikarabati eneo hilo, kwa sababu misaada iliyotolewa hadi sasa haijatosha kufanikisha lengo hilo. Zaidi ya nyumba laki moja za eneo hilo zimebomolewa katika hujuma na mashambulio ya jeshi la utawala haramu wa Kizayuni. Japokuwa katika kikao cha watoaji misaada wa kimataifa kilichofanyika mwezi Oktoba 2014 ilitolewa ahadi ya kuchangia dola bilioni tatu na nusu ili kusaidia ujenzi na ukarabati wa Gaza, lakini hadi sasa imetolewa asilimia 40 tu ya kiwango kilichoahidiwa.

Wakati huohuo mifarakano na migongano ya fikra inayoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu na kujiweka mbali na malengo ya asili ya kuundwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, ambayo sasa inajulikana kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, vimeufanya Ulimwengu wa Kiislamu ubaki kuwa mtazamaji tu wa jinai zinazoendelea kufanywa na makundi ya kigaidi na ukufurishaji katika nchi za Syria na Iraq na moto wa vita uliowashwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen huku baadhi ya nchi za Kiarabu zikishindana kuwania nafasi ya kwanza ya kuanzisha bila ya kificho uhusiano wa kisiasa na utawala haramu wa Israel.

Matarajio ya Wapalestina kwa kikao cha 13 cha viongozi wa nchi wanachama wa OIC kinachofanyika kwa kaulimbiu ya "Umoja na Mshikamano kwa ajili ya Uadilifu na Amani" ni kufikiriwa kwa uzito mkubwa hali ya maafa ya Gaza na kuchukuliwa hatua muhimu na za maana ili kuhatimisha masaibu ya Wapalestina wa eneo hilo.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …