Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 30 Juni 2015 20:05

Kikao cha usalama cha Algeria na Tunisia

Kikao cha usalama cha Algeria na Tunisia

Baada ya shambulio la siku ya Ijumaa lililofanywa na kundi la kigaidi la Daesh katika mji wa kitalii wa Sousse nchini Tunisia ambapo kwa akali watu 38 waliuawa wengi wao wakiwa ni watalii wa Kiingereza, Algeria na Tunisia zimetangaza kuwa, zitaandaa kikao kwa shabaha ya kuchukua hatua mpya za kupambana na ugaidi. Kikao hicho kitafanyika kwa maafikiano ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria na mwenzake wa Tunisia Rais Beji Caid Essebsi. Kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuhusika na shambulio hilo la Tunisia ambalo lilifanyika sambamba na mauaji ya huko Ufaransa na katika msikiti mmoja nchini Kuwait. Hivi sasa, Tunisia iko katika hali ya hatari kiusalama, na viongozi wa Tunis wamechukua hatua na mikakati mipya kwa lengo la kulinda amani na usalama wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hali ya mchafukoge na ukosefu wa usalama inayotawala nchini Libya itakuwa na taathira hasi za kiuchumi, kijamii na kijeshi kwa majirani wa nchi hiyo. Tangu kundi la kigaidi la Daesh lilipojipenyeza katika mji wa Sirte huko Libya, nchi hiyo imegeuka na kuwa maficho mazuri kwa wanachama wa kundi hilo na hivyo, kuwa tishio kwa nchi jirani na Libya kama Misri, Tunisia na Algeria. Fauka ya hayo, kuna baadhi ya wanachama wa makundi ya wanamgambo yenye mfungamano na Daesh ambao wamekuwa wakirejea nchini Tunisia kutoka Iraq, Syria na Libya. Habib Essid, Waziri Mkuu wa Tunisia amelitaja shambulio la kigaidi la tarehe 26 Juni kuwa ndilo tukio baya zaidi la kigaidi katika uhai wa kisiasa wa Tunisia na kuitaka jamii ya kimataifa kuisaidia serikali ya nchi hiyo katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo. Aidha amesisitiza kuwa, wanachama wa makundi yenye misimamo ya kufurutu ada walioko Libya nchi ambayo hivi sasa haina serikali kuu yenye nguvu wamekuwa wakipata mafunzo ya kijeshi na kurejea nchini Tunisia. Inakadiriwa kuwa, kuna Watunisia 3,800 ambao wanashiriki katika vita huko Iraq na Syria huku 1500 kati yao wakiwa nchini Libya. Kwa kweli inawawia vigumu mno viongozi wa Tunisia kudhibiti mipaka yake na majirani zake kama Libya na hawawezi kuwazuia wanachama wa makundi yenye misimamo mikali kurejea nchini humo. Shambulio la kigaidi katika mji wa Sousse ambalo linahesabiwa kuwa eneo mashuhuri zaidi kwa utalii, limetoa pigo kubwa kwa sekta ya utalii ya nchi hiyo. Baada ya shambulio hilo, takribani asilimia 80 ya safari za watalii wa kigeni za kuelekea Tunisia zilifutwa. Kutokea shambuliuo la pili la kigaidi nchini Tunisia katika mwaka huu kumewatia wasiwasi mno weledi wa mambo ambao wanaamini kwamba, kukaririwa mashambulio hayo kutalemaza kabisa sekta ya utalii ya nchi hiyo. Selma Elloumi Rekik, Waziri wa Utalii wa Tunisia anaamini kuwa, endapo sekta ya utalii ya nchi hiyo itasambaratika, basi uchumi wa Tunisia nao utaangamia. Kengele ya hatari imeanza kusikika kwani maelfu ya watalii wameondoka nchini humo na ni jambo lililo mbali kuweza kubadilika hali hiyo katika kipindi cha muda mfupi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Algeria ambayo ni miongoni mwa waungaji mkono wa Tunisia katika vita dhidi ya ugaidi, imeandaa mkutano wa pamoja na wa kiusalama na Tunisia. Viongozi wa Tunis na Algiers wana matumaini kwamba, kwa kuongezwa ushirikiano wa kieneo na kuweko mabadilishano ya taarifa za kiusalama wataweza kudhamini usalama kwenye mipaka na ndani ya nchi zao. Pamoja na hayo, madhali mizizi ya ugaidi haijang'olewa katika eneo la kaskazini mwa Afrika, haiwezekani kuwa na matumaini ya kupatikana amani na uthabiti katika eneo hilo. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, viongozi wa kundi la kigaidi la Daesh wanakusudia kupenya nchini Libya na kisha waasisi tawi la kundi hilo katika maeneo yote ya kaskazini mwa Afrika. Hivyo ushirikiano wa nchi mbili za Algeria na Tunisia kwa ajili ya kupambana na ugaidi utasaidia mno katika juhudi za kupunguza hatari za harakati za makundi ya kigaidi.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …