Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 19 Januari 2016 20:39

Shambulio la Saudia laua wanafunzi 9 nchini Yemen

Shambulio la Saudia laua wanafunzi 9 nchini Yemen

Shambulio la anga la ndege za Saudi Arabia limeuwa raia 10 wakiwemo wanafunzi 9 na mwanamke mmoja, kusini magharibi mwa Yemen.

Kanali ya televisheni ya al-Masira imeripoti kuwa, hujuma hiyo ya ndege za utawala wa Aal-Saud katika mkoa wa Taiz, kusini magharibi mwa nchi hiyo mbali na kuua, vile vile imesababisha idadi kubwa ya raia kujeruhiwa. Hii ni katika hali ambayo, shirika rasmi la habari la Yemen la Saba Net limeripoti kuwa, makumi ya raia wameuawa katika shambulio la anga la ndege za Saudia katika mji wa Haydan, kaskazini magharibi mwa mkoa wa Sa’ada. Kadhalika ndege hizo zimefanya mashambulio mengine katika maeneo tofauti ya mji mkuu wa nchi hiyo Sana’a. Mbali na maeneo hayo, habari zinasema kuwa mashambulio mengine ya Aal-Saud yamefanyika katika mikoa ya Ma’rib na Jawf. Serikali ya Riyadh imeshadidisha hujuma zake nchini Yemen siku chache baada ya Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) kutangaza kuwa muungano wa vita dhidi ya Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia unatumia mabomu ya vishada katika mashambulizi yake nchini humo. Hii ni katika hali ambayo tangu kuanza mashambulizi ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Yemen, zaidi ya watu 7,500 wamekwishauawa na wengine wapatao 14,000 wamejeruhiwa tangu Machi mwaka jana 2015.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)