Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumamosi, 09 Januari 2016 11:11

UN yaionya Saudia kwa kutumia mabomu ya vishada

UN yaionya Saudia kwa kutumia mabomu ya vishada

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema anatiwa wasiwasi na mashambulio ya anga yanayofanywa na Saudi Arabia nchini Yemen na kutanabahisha kuwa utumiaji mabomu ya vishada unaweza ukahesabiwa kuwa ni jinai ya kivita.

Stephan Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa mbali na wito wa mara kwa mara uliotolewa na Katibu Mkuu wa umoja huo wa kusimamishwa vita upya nchini Yemen, Ban ametiwa wasiwasi mno na kushtadi mashambulio ya Saudia katika maeneo ya makazi ya raia katika mji mkuu wa Yemen Sana'a hususan yale yaliyolenga jengo la sherehe za harusi na kituo cha wasioona.

Stephan Dujarric ameongeza kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepokea ripoti za kushtusha za utumiaji mabomu ya vishada dhidi ya raia katika maeneo tofauti ya mji wa Sana'a na kuongeza kwamba utumiaji mabomu hayo kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu unaweza ukahesabiwa kuwa ni jinai ya kivita.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamethibitisha kutumia Saudia mabomu ya vishada katika maeneo ya makazi ya raia mjini Sana'a na kuelezea kitendo hicho kuwa ni jinai ya kivita.

Usiku wa kuamkia Alkhamisi, ndege za kivita za Saudia zilishambulia maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Yemen, Sana'a kwa kutumia mabomu ya vishada, ambapo kwa akali, raia mmoja aliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa. Watu wanne pia walifariki dunia na wawili waljeruhiwa wakati ndege za majeshi vamizi za utawala wa aal Saud ziliposhambulia eneo la al-Marzaq mkoani Hajjah.

Tangu Saudia ilipoanzisha uvamizi na mashambulio dhidi ya Yemen mnamo mwezi Machi mwaka jana hadi sasa, zaidi Wayemeni 7,500 wameuawa na wengine wapatao 14,000 wamejeruhiwa.../

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)