Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 10 Julai 2015 20:37

'Mapambano, Njia Pekee ya kukomboa Quds'

'Mapambano, Njia Pekee ya kukomboa Quds'

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema, mapambano ndio njia pekee ya Wapalestina kuwashinda maghasibu na kukomboa ardhi zao hasa Quds Tukufu. Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran ameashiria kupita zaidi ya miongo sita tokea ardhi za Palestina zikaliwe kwa mabavu na kusema: "Vikao, mazungumzo na mikataba kuhusu Palestina hadi sasa haijakuwa na faida yoyote kwa Wapalestina." Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amefafanua zaidi kwa kusema: "Iwapo kumepatikana mafanikio hadi sasa katika njia ya kuikomboa Palestina, hii ni kwa sababu tu ya kufuata njia ya Intifadha na mapambano. Ni utamaduni huu wa mapambano uliowezesha taifa la Iran kupata ushindi miaka 36 iliyopita na kubakia imara hadi sasa." Ayatullah Khatami amesema jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika miaka yote ya kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina kama vile mauaji ya kikatili huko Sabra na Shatila na Ukanda wa Ghaza ikiwa ni pamoja na kubomoa mahospitali na misikiti ni ushahidi usiosahaulika wa utambulisho ulio dhidi ya binadamu wa utawala wa Kizayuni. Amesema licha ya kuwepo himaya ya madola makubwa ya dunia, utawala wa Kizayuni unakaribia kuangamia.
Ayatullah Khatami amesema maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu nchini Iran yamekuwa makubwa na ya hamasa zaidi ya miaka iliyotangua na kuongeza kuwa: "Taifa la Iran leo limetangaza kujibari na mushirikina na huu ni ujumbe kwa dunia kuwa nchi hii itaendelea katika mkondo wake wa kutetea haki na malengo yake matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu ikiwa ni pomoja na kuikomboa Quds Tukufu na kuhakikisha taifa la Palestina linapata ushindi mbele ya utawala wa Kizayuni.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa pia amesisitiza udharura wa kuwepo umoja kati ya nchi za Kiislamu ili kuangamiza utawala haramu wa Israel ambao ameutaja kuwa ni donda la saratani. Amesema pendekezo la Iran la kuitisha kura ya maoni huko Palestina ni pendekezo mwafaka na kuongeza kuwa, Wapalestina wanapaswa kupewa haki ya kuainisha hatima yao.
Kuhusu mazungumzo ya nyuklia, Ayatullah Khatami amesema mapatano mazuri yanapaswa kuwa kwa msingi wa maslahi ya taifa la Iran. Akiashiria hatua ya Marekani kubadilisha msimamo wake katika mazungumzo ya nyuklia, Ayatullah Khatami amesema: Wamarekani wamevunja ahadi zao na hili linathibtisha kwa mara nyingine kuwa, Marekani haiwezi kuaminika hata kidogo. Kuhusu kadhia ya Yemen, Imamu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema utawala wa kikoo Saudi Arabia unahudumia utawala wa Kizayuni wa Israel na kwamba hatimaye watu wa Yemen watapata ushindi.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)