Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Ijumaa, 29 Mei 2015 09:12

Hatua hatari za utawala wa Kizayuni za kuihodhi kikamilifu Quds tukufu

Hatua hatari za utawala wa Kizayuni za kuihodhi kikamilifu Quds tukufu

Habari kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu zinaeleza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha harakati mpya za kuidhibiti na kuihodhi kikamilifu Quds Tukufu. Harakati hizo ambazo zinadhihirisha hatua hatari zinazochukuliwa na Wazayuni zimewatia jakamoyo na wasiwasi mkubwa wananchi wa Palestina. Kushadidi mashambulio ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya Quds na hatua za serikali ya utawala haramu wa Israel za kutaka kuudhibiti na kuuhodhi kikamilifu mji huo mtakatifu zinaonyesha jinsi mji huo ulivyofanywa kitovu cha duru mpya ya harakati za Israel za kughusubu maeneo mbalimbali ya Palestina. Kushadidi uchokozi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Quds tukufu na vitendo vya Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu mpaka vya kuuvunjia heshima msikiti mtukufu wa al Aqsa vimechukua muelekeo mpana na hatari zaidi katika wiki za karibuni. Harakati za karibuni za Baraza la Mawaziri la Israel zimezidi kuweka wazi nia chafu na ovu ya utawala haramu wa Kizayuni ya kutumia nyenzo na suhula zake zote ili kuihodhi na kuidhibiti kikamilifu Quds tukufu. Miongoni mwa harakati hizo ni uamuzi wa Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Kizayuni Benjamin Netanyahu wa kuasisi Wizara ya Masuala ya Quds na kumkabidhi wadhifa wa kushughulikia masuala hayo mzayuni mwenye misimamo ya chuki na ya kufurutu mpaka kutoka chama cha Likud aitwaye Ze'ev Elkin, uamuzi ambao unazidi kudhihirisha ukubwa wa njama inayoandaliwa na utawala huo dhidi ya msikiti mtukufu wa al Aqsa. Sambamba na hayo Miri Regev, Waziri mpya wa Utamaduni na Michezo wa utawala wa Kizayuni amesisitiza kuwa katika hatua atakazochukua ni pamoja na kuhamishia ofisi za wizara yake huko Quds inayokaliwa kwa mabavu. Hii ni katika hali ambayo maazimio nambari 250 hadi 253 yaliyopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 1968 na vilevile maazimio kadhaa ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiwemo azimio nambari 2253 na 2254 yaliyopitishwa mwaka 1967, yameipiga marufuku Israel kujipa mamlaka ya kufanya chochote itakacho katika maeneo ya Palestina inayoyakalia kwa mabavu ikiwemo Baitul Muqaddas hususan kuhamishia wizara zake katika mji huo mtakatifu. Lisilo na shaka yoyote ni kuwa Quds ina nafasi maalumu katika siasa za kujitanua za utawala wa Kizayuni wa Israel na kwa msingi huo baada ya kuuvamia na kuukalia kwa mabavu mji huo katika awamu mbili, yaani eneo lake la magharibi mwaka 1948 na eneo lake la mashariki mwaka 1967, lengo la utawala huo ghasibu ni kujizatiti katika kuidhibiti zaidi Baitul Muqaddas. Na katika mikakati ya kufanikisha njama yake hiyo, mnamo mwaka 1980 utawala wa Kizayuni uliitangaza Quds kuwa mji mkuu wake na kuanzisha mpango wa kuhamishia mjini humo taasisi muhimu za serikali pamoja na balozi za kigeni zilizokuwa Tel Aviv.

Alaa kulli hal, ushahidi uliopo unaonyesha kuwa katika wiki za hivi karibuni hatua za kifedhuli na kichokozi za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Palestina ukiwemo mji wa Baitul Muqaddas na hasa msikiti mtukufu wa al Aqsa zimechukua sura hatari zaidi na tata mno. Sisitizo la viongozi wa utawala wa Kizayuni la kudai kwamba Baitul Muqaddas ni eneo lisilotenganishika na ardhi nyengine zilizoporwa na Wazayuni na kuunda nchi bandia ya Israel ni utangulizi wa hatua kubwa zaidi za njama za kisiasa za utawala huo dhidi ya msikiti mtukufu wa al Aqsa…/  

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)