Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumapili, 15 Novemba 2015 19:13

Familia za waliotoweka Mina kupelekwa Saudia

Familia za waliotoweka Mina kupelekwa Saudia

Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara, ambaye pia ni kiongozi wa msafara wa mahujaji wa Kiirani amesema watu wa familia za Wairani waliotoweka katika maafa ya Mina watapelekwa Saudi Arabia ili kufanyiwa tena vipimo vya vinasaba (DNA). Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Ghazi-Askar amesema jamaa wa mahujaji wa Kiirani waliotoweka katika maafa ya Mina wakiwemo watoto au ndugu zao wa kiume watapelekwa huko Saudia na kufanyiwa vipimo vya vinasaba (DNA) ili kumaliza visingizio vinavyotolewa na serikali ya nchi hiyo. Akizungumza na vyombo vya habari leo pembeni ya kikao cha kitaalamu cha kujadili maafa ya Mina, kiongozi wa msafara wa mahujaji wa Kiirani amesema kuhusiana na hali ya mahujaji waliotoweka katika maafa ya Mina kuwa kungali na mahujaji kadhaa ambao hawajapatikana hadi sasa na kwamba Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran inafanya kila jitihada za kuandaa ushahidi kuhusu jinsi maafa ya Mina yalivyotokea sambamba na kufuatilia hatima ya mahujaji waliotoweka. Hujjatul Islam Walmuslimin Ghazi-Askar amefafanua kuwa Iran inaendelea kukusanya maelezo ya baadhi ya mashuhuda wa ndani na nje ya nchi kuhusu maafa ya Mina ili kuweza kupata ushahidi unaoweza kuwasilishwa katika taasisi za kimataifa. Alipoulizwa kuhusu hatima ya balozi wa zamani wa Iran nchini Lebanon Ghazanfar Roknabadi, Mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika masuala ya Hija na Ziara amesema vinasaba vya mwanadiplomasia huyo vimeshachukuliwa na Idara ya Uchunguzi wa Vifo ya Iran na kupelekwa Saudia. Kwa mara nyengine tena Hujjatul Islam Walmuslimin Sayyid Ali Ghazi-Askar amesisitiza kuwa lazima Saudia ifuatiliwe kwa makosa iliyofanya katika maafa ya Mina kwa sababu roho za watu zaidi ya elfu saba wasio na hatia zimepotea; na kwa hivyo inapasa adhabu zitolewe kulingana na makosa yaliyofanywa. Tarehe 24 Sepetmba mwaka huu, mahujaji 464 wa Kiirani walipoteza maisha katika siku ya Idul-Adh’ha wakati wakitekeleza amali za Hija katika eneo la Mina huko Makka. Hatima ya mahujaji wengine 19 waliopteza maisha katika maafa hayo hadi sasa haijajulikana…/

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)