Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumanne, 27 Oktoba 2015 14:06

Ripoti kuhusu Matukio ya Kiusalama Yemen

Ripoti kuhusu Matukio ya Kiusalama Yemen

Saudi Arabia inaendeleza hujuma zake za kinyama dhidi ya raia wa nchi masikini ya Yemen. Katika kipindi cha siku mbili zilizopita ndege za kivita za Saudia zimedondosha mabomu katika maeneo ya raia katika mji mkuu wa Yemen Sana’a na maeneo mengine ya nchi hiyo.  Imedokezwa kuwa ndege za Saudia zilishambulia shule katika eneo la Al Siniyat mjini humo. Aidha ndege za Saudia zimedondosha mabomu katika mkoa wa Ma’arib kati mwa Yemen. Habari zingine zinasema kuwa Saudi Arabia sasa inatumia  askari mamluki wa shirika la kijeshi la Marekani la Blackwater, ambalo sasa linajulikana kama  Academi, katika kuendeleza hujuma zake dhidi ya Wayemen. Abdullah bin Ammar, mwandishi habari wa Yemen katika tovuti ya Yemen Press amefichua kuwa shirika la Blackwater ambalo lilitenda jinai za kinyama huko Iraq sasa linahudumu Yemen  chini ya bendera ya Jeshi la Colombia. Imedokezwa kuwa shirika la hilo la mamluki la Blackwater lina ofisi Colombia na aghalabu ya mamluki hao ni raia wa nchi za Amerika Kusini waliolipwa na Saudia kuua raia wa Yemen.

Kwingineko magaidi wa al Qaeda hivi karibuni walihujumu gereza kuu la mji wa Aden kusini mwa Yemen. Magaidi hao ambao wamekuwa wakiunga mkono hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen waliwaachilia huru wahalifu na magaidi kadhaa katika gereza hilo.

Katika kulipiza kisasa jinai zisizo na kikomo za Saudia,  jeshi la Yemen na makundi ya wapiganaji wa kujitolea wametekeleza hujuma na kuzamisha meli moja ya kivita ya Saudia katika Bahari ya Sham ambapo pia wanajeshi kadhaa vamizi wa Saudia na Imarati waliuawa. Meli hiyo ya Saudia ilikuwa ikivurumisha makombora katika vijiji vya Yemen kabla ya kuzamishwa. Aidha vikosi vya wananchi vimeshambulia ikulu ya rais na idara ya mkuu wa shirika la kijasusi katika mji wa Tai’zz ambapo mamluki 38 wa Saudi Arabia wameangamizwa a wengine wengi kujeruhiwa karibu na  bandani ya Mocha. Mapigano hayo yalijiri wakati vikosi vitiifu kwa rais mtoro wa Yemen, Abdurabuh Mansour Hadi vilipojaribu kuchukia udhibiti wa eneo hilo bila mafanikio.

Kwingineko katika uga wa kisiasa, Mohammad Al Houthi mkuu wa kamati ya kisiasa ya Harakati ya Ansarullah ya Yemen siku ya Jumatati alifanya mazungumzo na wanachama wa Muungano wa Kiraia, Amani na Maelewano ya Kitaifa Yemen na kusema, utawala wa Aal Saud kwa hujuma yake Yemen umepuuza misingi yote ya kisiasa ya kuutatua mgogoro nchini humo.

Aidha amesema amepokea mpango wa amani na maelewano ambapo pande zote za kisiasa ndani ya nje ya nchi zimeshirikishwa. Mpango huo wa amani unajumuisha kurejea mchakato wa kisiasa  wenye kuzingatia misingi ya kitaifa na kuundwa serikali mpya ya kiraia kwa mujibu wa maelewano na mazungumzo. Saudi Arabia imekuwa kizingiti kikubwa katika kupatikana muafaka wa amani Yemen. Saudi Arabia na waitifaki wake tarehe 26 mwezi Machi mwaka huu walianzisha mashambulizi dhidi ya waanchi wa Yemen wasio na hatia  kwa kisingizio cha kuirejesha serikali ya Yemen iliyojiuzulu. Mashambulizi hayo mbali na kuharibu miundo mbinu, hospitali, misikiti, shule na nyumba za raia, yameuwa na kujeruhi pia maelfu ya watu. Karibu Wayemen 7,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa katika hujuma hizo za kinyama za Saudia nchini Yemen.

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)