Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 25 Aprili 2016 10:32

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 25

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 25

Wanataekwondo wa Iran wang'ara Ufilipino

 

Timu ya taifa ya mchezo wa taekwondo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa taji la mashindano ya kieneo ya mchezo huo nchini Ufilipino baada ya kuzoa jumla ya pointi 56. Siku ya Jumatano, mabarobaro hao wa Iran walitangazwa washindi wa duru ya 22 ya mashindano hayo yajulikanayo kama Asian Taekwondo Championships, baada ya kushinda medali 5, zikiwemo 3 za dhahabu na 2 za fedha.

Korea Kusini iliibuka ya pili kwa pointi 48, baada ya kutwaa jumla ya medali 4; 3 za dhahabu na shaba moja. Uzbekistan ambayo ilishinda dhahabu moja, fedha moja na shaba moja iliambulia nafasi ya tatu baada ya kutia kibindoni alama 32. China haikua na budi kuridhika na nafasi ya nne kwa kuzoa pointi 28 huku wakirejea nyumbani na medali moja ya dhahabu na 3 za shaba. Wanataekwondo 239 kutoka nchi 31 za bara Asia wameshiriki mashindano hayo yaliyofanyiwa katika ukumbi wa Pasay mjini Manala, kati ya Aprili 18 hadi 20.

Teraktor Sazi ya Iran yaiadhibu al-Hilal ya Saudia ACL

Klabu ya Teraktor Sazi ya Iran imeichabanga al-Hilal ya Saudi Arabia mabao 2-0 katika mchuano wa Kundi C ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Asia.

Katika kipute hicho cha Jumanne kwenye uwanja wa Suheim Bin Hamad katika mji mkuu wa Qatar, Doha, kiungo Aloys Nong wa watengeneza trakta wa Iran alipachika kimyani bao moja na kufanya juhudi za kupatikana la pili. Nong ambaye ni raia wa Cameroon aliipa Teraktor bao la kwanza kunako dakika ya 66 na kuiweka kifua mbele klabu hiyo ya Iran.

Dakika 9 baadaye, Farzad Hatami alipachika kimyani bao la pili na hivyo kuiwezesha klabu hiyo ya Iran kutinga hatua ya muondoano.

Vijana wa Teraktor  wa Iran tayari walikua wameikung'uta al-Jazira ya Umoja wa Falme za Kiarabu mara mbili huku ikiichapa Pakhtakor ya Uzbekistan mara moja na kukubali kichapo kutoka klabu hiyo katika mechi ya marudiano.

 

Kenya yatamba London Marathon huku Rais Kenyatta akisaini sheria mpya ya kudhibiti pufya

 

Wanariadha wa Kenya wameng'ara katika mashindano ya kimataifa ya mbio za London Marathon Jumapili na kuendeleza ubabe wa nchi hiyo ya kufanya vyema katika mbio za masafa marefu. Eliud Kipchoge nusura avunje rekodi ya dunia ya mbio hizo alipoandikisha muda wa kasi zaidi katika mbio za London Marathon. Mkenya huyo alihifadhi taji aliloshindwa mwaka jana, alipoandikisha muda wa kasi zaidi wa saa mbili dakika tatu na sekunde 5, sekunde 8 tu nje ya rekodi ya dunia ya mbio hizo. Rekodi hiyo ya dunia iliwekwa na Mkenya mwingine Dennis Kimetto katika mashindano ya Berlin Marathon mwezi Septemba mwaka wa 2014. Kipchoge alikimbizana unyo kwa unyo na Mkenya mwenza Stanley Biwott hadi iliposalia takriban kilomita tatu kufikia kwenye utepe, ndipo alipotifua kivumbi na kuidhihirishia dunia ubingwa wake katika mbio hizo za masafa marefu.

Biwott alijifurukuta na kumaliza katika nafasi ya pili huku hasimu wake katika mbio za mita 5000 Kenenisa Bekele kutoka Ethiopia akifunga orodha ya tatu bora. Katika safu ya wanawake kwenye mbio hizo, Mkenya mwengine Jemima Sumgong, licha ya kutegwa na mwanariadha mpinzani kutoka Ethiopia Aselefech Mergia na kudondoka chini mwanzoni mwa mbio hizo, aliupa maana msemo unaosema 'kuteleza sio kuanguka' na kuibuka mshindi, kwa kutumia saa mbili dakika 22 na sekunde 58. Tigist Tufa wa Ethiopia, aliyeshinda mwaka jana, mara hii ameonyesha kiumbi na kulazimika kumaliza wa pili. Mkenya mwengine Florence Kiplagat alimaliza katika nafasi ya tatu akitumia muda wa saa mbili dakika 23 na sekunde 39

Huku hayo yakijiri, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kati kati ya wiki iliyomalizika aliidhinisha sheria ya kuitambua pufya au matumizi ya dawa za kututumua misuli kuwa kosa la jinai.

Baada ya kukosa kutimiza makataa ya kupitisha sheria hiyo Februari 11, 2016 na kisha Aprili 5, 2016 kutoka kwa Shirikisho la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya Duniani (WADA), Kenya sasa imeidhinisha sheria hiyo kabla ya makataa ya tatu ya shirikisho hilo, iliyotazamiwa kukamilika Mei 2, 2016. Iwapo Kenya isingepitisha sheria hiyo, ingekuwa katika hatari ya kupigwa marufuku kushiriki katika Mashindano ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwaka huu na mashindano mengine ya riadha. Baadhi ya adhabu katika sheria hii mpya ni kuwa, wanariadha wanaokataa kupimwa, wanaopatikana na uhalifu wa dawa hizo haramu, wanadanganya shirika la kukabiliana na uovu huu ama kusumbua kazi yake kufungwa jela mwaka mmoja ama faini ya Sh100, 000 au adhabu zote mbili. Watu watakaopatikana wakisafirisha, kuweka ama kuwapa wanaspoti dawa zilizopigwa marufuku na WADA watatozwa faini ya Sh 3 milioni ama kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani ama yote mawili. Zaidi ya Wakenya 40 wamepatikana na hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli kati ya mwaka 2012 na 2015.

 

Mwafrika wa kwanza kutuzwa Taji la PFA

 

Kiungo nyota wa Algeria ameipa fahari bara la Afrika kwa kuwa mchezaji soka wa kwanza kutoka bara hilo kutangazwa mshindi wa Tuzo ya Shirikisho la Wachezaji Nguli wa Soka PFA mwaka 2015/2016.

Riyadh Mahrez, winga mshambuliaji wa kimataifa raia wa Algeriaanayeichezea pia klabu ya Leicester City ya Uingereza alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya PFA 2015/2016 (Professional Footballers Association) Jumapili usiku.

Mahrez ametangazwa kushinda tuzo hiyo na kuwapiku mabingwa wengine wa soka duniani waliouwa wameteuliwa; kama vile Mesut Ozil wa Arsenal, Jamie Vardy wa Leicester City, Harry Kane wa Spurs, N’golo Kante waLeicester City na Dimitri Payet wa West Ham United.

Twabaan, PFA ni tuzo za wachezaji bora wa kimataifa wa kulipwa.

 

Droo ya CAF mwezi ujao

 

Shirikisho la Soka barani Afrika CAF linatazamiwa kutangaza droo ya hatua ya makundi ya kutafuta ushindi wa taji la Klabu Bingwa barani Afrika tarehe 24 mwezi ujao wa Mei. Vilabu vinane ambavyo vimefuzu katika hatua hii tayari vimefahamika na vitawekwa katika hatua ya makundi mawili, kila kundi na timu nne. Kwa mujibu wa kanuni za shirikisho la CAF, mechi hizo zitachezwa nyumbani na ugenini na mshindi atafuzu katika hatua ya nusu fainali.

Vlabu vilivyofuzu ni pamoja na:-

ES Setif ya Algeria, AS Vita Club ya DRC, Al-Ahly ya Misri, Zamalek ya Misri, ASEC Mimosas ya Kodivaa, Wydad Casablanca ya Morocco, Enyimba ya Nigeria na ZESCO United ya Zambia

Mabingwa watetezi wa taji hili msimu uliopita TP Mazembe ya DRC waliondolewa baada ya kufungwa ugenini mabao 2 kwa 0 na kutoka sare ya bao 1 kwa 1 mjini Lubumbashi siku ya Jumatano.

 

Tenisi

 

Mchezaji tenisi nambari tano duniani kwa upande wa wanaume Rafael Nadal ameshinda mchezo wake uliokuwa ukifwatiliwa na wengi dhidi ya Albert Montanes katika mashindano ya BarcelonaOpens. Katika kitimutimu hicho cha Aprili 22, Nadal alimshinda mpinzani wake kwa seti mbili za 6-2 , 6-2.

Kwa ushindi huo bingwa huyo wa tenisi sasa atatoana jasho na Muitaliano Fabio Fognini ambae nae alimshinda Viktor Troicki katika mchuano wake. Fognini alimshinda Nadal katika raundi ya tatu ya michuano ya msimu uliopita na hivyo kumpa Nadal kibarua cha ziada za kujibu mapigo na wakati huo huo kusaka ushindi.

 

..................................................TAMATI................................

Zaidi katika kategoria hii: « Ulimwengu wa Michezo, Aprili 18

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …