Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 18 Aprili 2016 10:44

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 18

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 18

Debi la Tehran: Persepolis yaizamisha Esteghlal 4-2

Klabu ya soka ya Persepolis ya Iran imefanikiwa kusajili ushindi muhimu wa mabao 4-2 dhidi ya watani wao wa jadi Esteghlal, katika mchuano wa kusisimua unaojilikana kama Debi la Tehran siku ya Ijumaa mjini hapa. Wekundu wa Iran wanaonolewa na Branko Ivankovic waling'ara katika kipute hicho cha 82 cha mahasimu wa jadi na kuwalemea vijana wa The Blues katika mchuano huo wa wiki ya 26 ya Ligi Kuu ya Ghuba ya Uajemi katika uwanja wa Azadi uliokuwa umefurika maelfu ya mashabiki. Persepolis 'Vijana wa Mjini' walitandaza ngozi katika kipindi chote cha mchezo licha ya manyunyu na upepo mkali, huku Mehdi Taremi akiifungia timu hiyo mabao mawili katika dakika ya 5 na 35. Nusra afunge bao la tatu (hat-trick) lakini kipa wa Esteghlal Mehdi Rahmati akaokoa mkwaju wa penalty uliopigwa na kiungo huyo mahiri. Ramin Rezaeian alicheka na nyavu za Esteghlal na kuipa Persepolis la tatu, baada ya mlinda lango kuutema mpira, kutokana na shuti kali la Ahmadzadeh. Jaber Ansari aliipa Esteghlal bao la kwanza baada ya kipa wa Persepolis kutema mpira kwenye sanduku la hatari.

Kiungo Mosalman aliipa Persepolis bao la 4 na kufanya mambo kuwa 4-1 na kulizamisha kabisa dau la Esteghlal.

Omid Ibrahimi aliipa Esteghlal bao la pili kupitia mkwaju wa penalty katika dakika za lala salama, na mchuano huo kuishia kwa mabao 4-2.

Kwa ushindi huo, Persepolis wamekwea kileleni mwa Ligi ya Watalaamu ya Iran IPL, ikiwa na pointi 48 mbele ya Esteghlal ya Khuzestan yenye pointi 46, huku Esteghlal ya Tehran ikiridhika na nafasi ya 3 ikiwa na pointi 45.

Iraq: Mchuano kati yetu na Iraq upigwe Iran

Rais wa Shirikisho la Soka la Iraq amesema timu ya taifa ya kandanda ya nchi hiyo haitachuana na Saudia nchini Saudi Arabiakatika kipute cha kutafuta tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 na badala yake amesisitiza kuwa mchezo kati ya timu mbili hizo uchezewe Iran. Abul Khaliq Masood, amesema timu ya taifa ya Iraq inafadhilisha kuchezea michuano yake ya kufuzu Kombe la Dunia nchini Iran na kwamba wapo tayari mchuano huo upigwe katika nchi ya tatu na wala sio Saudia. Mashirikisho ya soka ya Iran na Saudia yamekuwa katika mkwaruzano tangu Riyadh itangaze kukata uhusiano wake na Tehran mapema mwaka huu. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, utawala wa Aal-Saud Januari 3 ulitangaza kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran, baada ya kufanyika maandamano nje ya ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi mdogo mjini Mashhad, kulalamikia hatua ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo kumuua shahidi mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini humo, Sheikh Nimr Baqir al-Nimr.Riyadh ilitumia kisibabu hicho kuliandikia barua Shirikisho la Soka Asia AFC, ikiliambia kuwa timu ya taifa ya soka ya Saudia haitatia guu nchini Iran kutokana na kile walichokitaja kuwa sababu za kiusalama. Iraq ipo katika Kundi B kwenye duru ya tatu ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2018; pamoja na Japan, Australia, Saudia, Thailand na Umoja wa Falme za Kiarabu. Iran nayo imeorodheshwa katika Kundi A pamoja na Korea Kusini, Uzbekistan, Qatar, China na Syria. Timu mbili zitakazofuzu katika kila kundi zitajikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2018.

Raga: Kenya 7's Yang'ara Singapore

Timu ya taifa ya Kenya ya mchezo wa raga ya wachezaji 7 kila upande imeingia katika madaftari ya kumbukumbu baada ya kutwaa Taji la Ligi ya Raga nchini Singapore. Vijana wa kocha Benjamin Ayimba waliandikisha historia hiyo kwa kuisasambua Fiji alama 30 kwa 7 katika fainali ya kukata na shoka siku ya Jumapili.

Soka: Harambee Starlet kuwania Kombe la Afrika

Timu ya Taifa ya Soka ya Kenya ya Wanawake imetinga fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya kandanda barani humo. Michuano hiyo ya kikanda itapigwa nchini Cameroon kati mwezi Novemba na Disemba mwaka huu 2016. Mabanati wa Harambee Starlets wamefuzu katika michuano hiyo ya kibara licha ya sare 1-1 na Algeria katika mchuano wa Jumanne jijini Nairobi, ikizingatiwa kuwa tayari walikuwa wamefanya vyema ugenini katika mchuano wa mzunguko jijini Algiers. Kenya sasa inajiunga na mwenyeji Cameroon ambayo mwaka 2014 walimaliza wa pili. Misri nayo imefuzu kwa mara ya pili baada ya kushiriiki mara ya kwanza mwaka 1998 na kuondolewa katika hatua ya makundi. Mabingwa wa mwaka 2008 na 2015, Equitorial Guinea nao wamejikatia tiketi ya kucheza katika fainali hizo ambazo wameshiriki mara tano. Nigeria ambao ni mabingwa watetezi na ambao wameshinda taji hili mwaka 1991, 1995, 1998, 2000, 2004, 2006, 2010 na 2014 wanashiriki kwa mara ya 12. Afrika Kusini nayo imefuzu kwa mara ya 11 huku Zimbabwe iliyomaliza katika nafasi ya 4 mwaka 2000 ikitazamiwa kucheza kwa mara ya 4. Mataifa haya manane yatajumuishwa katika makundi mawili, kila kundi likiwa na timu nne. Timu mbili za kwanza katika kila kundi zitafuzu katika hatua ya nusu fainali.

Ulimwengu atakata TP Mazembe

Mchezaji nyota wa kimataifa wa soka raia wa Tanzania, Thomas Ulimwengu anaendelea kung’ara katika klabu yake ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kongo. Hii ni baada ya kiungo huyo kufunga bao moja kati ya mawili yaliyofungwa usiku wa Alkhamisi katika mchuano dhidi ya Shark XI FC. Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliochezwa kwenye uwanja wa Martys mjini Kinshasa, Ulimwengu alifunga bao hilo kunako dakika ya 68 baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Rogger Asale dakika 57. Ulimwengu alifunga bao hilo akimalizia pasi ya Rainfrod Kalaba, wakati bao la kwanza la mabingwa hao wa Afrika lilifungwa na Luyindama dakika ya 65 kwa pasi ya Joseph Bolingi. Mazembe inarejea Lubumbashi kujiandaa na mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora kwenye Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco Aprili 20. Mazembe inahitaji ushindi wa 3-0 ili kusonga mbele baada ya kufungwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza hivi karibuni mjini Casablanca.

Wanariadha wa Afrika Mashariki wajikatia tiketi ya Olimpiki ya Rio

Moses Kipsiro, mwanariadha bingwa wa Uganda amejikatia tiketi ya kushiriki Mashindano ya Olimpiki ya Rionchini Brazil Agosti mwaka huu, licha ya kumaliza wa 14 katika mashindano ya mbio za Hamburd Marathon siku ya Jumapili nchini Ujerumani. Kipsiro mwenye umri wa miaka 29, alimaliza mbio hizo za nyika za kilomita 42 kwa kutumia 2:17:00. Raia wa Ethiopia Tesfaye Abera ndiye aliyeibuka kidedea katika mashindano hayo ya Hamburg Marathon kwa kutumia 2:06:58, huu ukiwa ni ushindi mnono wa pili mwaka huu kwa mwanariadha huyo, ikitiliwa maanani kuwa alishinda mbio za Dubai Marathon. Phelemon Rono wa Kenya alimaliza wa pili huku mwenzake Josphat Kiprono akimaliza katika nafasi tatu.

Ligi ya UEFA

Bayern Munich imefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya maarufu kama UEFA Champions League, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Benfica, katika mechi ya marudiano iliyopigwa Jumatano usiku. Katika mchezo mwingine Barcelona ilivuliwa taji la Ligi ya Champions baada ya kulambishwa mabao 2-0 na Atletico Madrid. Kwa mantiki hiyo hiyo Benfica na Barcelona zimebaduliwa katika michuano ya ligi hiyo, huku klabu za Bayern Munich na Atletico Madrid zikitinga nusu fainali. Katika mechi ya awali iliyopigwa katika uwanja wa Camp Nou, Atletico Madrid walifungwa mabao 2-1, lakini katika mchuano wa marudiano klabu hiyo ilifanya vizuri kwa kupata ushindi wa mabao 2-0, na hivyo kutinga nusu fainali. Bayern Munich na Atletico Madrid wanaungana na Manchester City pamoja na Real Madrid katika nusu fainali. Hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Soka Ulaya ilipigwa Alkhamisi kwa michezo minne. Sevilla imeiondoa Athletic Bilbao kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya mechi ya awali na ya maurudiano ya timu hizo mbili kuishia sare ya kufungana jumla ya mabao 3-3 baada ya kila timu kushinda 2-1 mechi ya nyumbani. Villarreal iliinyeshea mvua ya mabao Sparta Praga kwa kuichapa 4-2, huku Liverpool ikiipepeta Borrussia Dortmund mabao 4-3. Sevilla, Villarreal, Liverpool na Shakhtar Donetsk wamefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

…………………..TAMATI…………………

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …