Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 04 Aprili 2016 11:43

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 4

Ulimwengu wa Michezo, Aprili 4

Soka: Iran yatinga hatua ya mwisho kuelekea Kombe la Dunia

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetinga hatua ya mwisho ya mbio za kusaka nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018. Hii ni baada ya kuisasambua Oman mabao 2-0 katika mchuano wa Kundi D katika uwanja wa taifa wa Azadi jijini Tehran. Nyota wa mchezo huo uliopigwa Jumanne alikuwa kiungo Sardar Azmoun ambaye alifunga mabao yote mawili katika dakika ya 16 na 23. Kwa ushindi huo, Iran inasalia kileleni mwa Kundi D ikiwa na pointi 20 na hivyo kujikatia tiketi ya kushiriki hatua ya mwisho ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018. Itakumbukwa kuwa, timu ya taifa ya Iran iliichabanga India mabao 4-0 katika mchuano mwingine wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018. Mabao manne katika mchezo dhidi ya India yalifungwa na nahodha Ehsan Hajsafi na Sardar Azmoun, kila mmoja mawili.

Wanataekwondo wa Iran waelekea Ujerumani

Wanaspoti watatu wa mchezo wa taekwondo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu hii waliondoka nchini kuelekea Ujerumani kwa ajili ya kushiriki mashindano mawili ya kimataifa ya mchezo huo. Farzan Ashurzadeh, Sajjad Mardani na Mehdi Khodabakhshi wanatazamiwa kushiriki mashindano ya kuwania Kombe la Rais wa Shirikisho la Taekwondo Duniani WTF, kuanzia Aprili 7 hadi 9. Mabingwa hao wa Iran ambao tayari wamejikatia tiketi ya kushiriki mashindano ya Olimpiki ya Rio nchini Brazil baadaye mwaka huu, pia watashiriki Mashindano ya Wazi ya Uhispania ya Taekwondo mwaka huu 2016, yatakayofanyika kuanzia Aprili 15 hadi 17 nchini Ujerumani.

Mbio za kuelekea AFCON

Nchi kadhaa za Afrika zimebisha hodi katika michuano ya kandanda ya kuwania Kombe la Mataifa Bingwa Barani Afrika AFCON, huku miamba ya soka barani humo kama vile Nigeria ikiwa na nafasi finyu ya kusonga mbele. Morocco imekuwa nchi ya kwanza kufuzu katika michuano ya AFCON, itakayofanyika mwaka ujao 2017 nchini Gabon. Hii ni baada ya kuisasambua Cape Verde mabao 2 kwa 0 katika mchuano wa aina yake uliopigwa Jumanne usiku mjini Marrakech. Mshambuliaji wa Morocco Yussuf al-Arabi aliifungia timu yake mabao yote mawili katika kipindi cha kwanza cha mchuano huo. Vijana wa kocha Herve Renard raia wa Ufaransa ambaye aliwahi kuisaidia Kodivaa na Zambia kunyakua taji la AFCON, wanaongoza Kundi F kwa alama 12 baada ya kushinda mechi 4 walizocheza hadi kufikia sasa. Misri na Senegal nazo zinakaribia kufuzu baada ya kushinda mechi zao muhimu. Bao la pekee la Ramadhan Subhy limeiweka Misri katika mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kuilaza Nigeria mjini Alexandria katika mchuano wa kundi G. Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Nigeria hawana uwezekano wa kufuzu kwa sababu kundi lao limesalia na timu tatu ikiwemo Tanzania baada ya Chad kujiondoa. Misri ambayo imeshinda taji la Afrika mara saba, ina alama 7 na inahitaji tu alama 1 kujikatia tiketi ya kucheza fainali hizo mwakani. Senegal nayo ilijiweka katika nafasi nzuri baada ya kuifunga Niger mabao 2 kwa 1 yaliyofungwa na Moussa Konate na Papa Souare. Senegal sasa inaongoza Kundi K kwa alama 12 mbele ya Burundi ambayo ina alama 6 baada ya kupata ushindi wa mabao 3 kwa 1 dhidi ya Namibia ugenini. Uganda Cranes ikichezea nyumbani katika uwanja wa Naambole jijini Kampala, ilitoka sare ya kutofungana na kuacha kila mmoja na alama 7 katika Kundi D. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nayo imehuisha matumaini yake ya kufuzu baada ya kuifunga Angola mabao 2 kwa 0 ugenini. Rwanda nayo iliishinda Mauritius mabao 5 kwa 0 huku Burundi ikiilemea Namibia mabao 3 kwa 1 jijini Windhoek. DRC imerejea kileleni mwa Kundi B baada ya kupata ushindi mjini Luanda dhidi ya Angola wa mabao 2-0. Ikiwa na alama 9, Kongo DR sasa iko mbele ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambayo ni ya pili ikiwa na alama 7.

Ligi ya Soka ya Premier

Ligi Kuu ya Soka Uingereza iliendelea kuroroma kwa michezo kadhaa, huku mchuano kati ya Manchester United dhidi ya Everton, mgaragazano kati ya Arsenal na Watford na kitimutimu cha vinara wa EPL Leicerster dhidi ya Southamptom zikiteka fikra za mashabiki wengi wanaofuatilia ligi hiyo. Bao la dakika ya 54 la kiungo Anthony Martial lilitosheleza kuipa Man U ushindi muhimu waliouhitaji walipochuana na Everton siku ya Jumapili nyumbani Old Traford mbele ya mashabiki zaidi ya 75 elfu. Baada ya kukosa bao katika kipindi cha kwanza, vijana wa Van Gaal walirejea kutoka mapumzikoni kwa kishindo. Martial alitumia vyema pasi safi ya Tim Fosu-Mensah na kuiacha Everton ikikuna kichwa baada ya kupoteza mechi yao ya tatu mfululizo katika ligi kuu ya Uingereza. Arsenal imeendelea kuyapa nguvu matumaini yao ya kuwania taji hilo mwaka huu baada ya ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Watford. Vijana wa Gunners walitangulia kuwa kifua mbele mapema. Hii ni baada ya Alexi Sanchez kufunga bao la kwanza kupitia pasi safi ya Iwobi dakika nne baada ya kuanza mchezo. Iwobi baadaye alifunga bao la pili, Bellerin la tatu kabla ya Theo Walcot kufanya mambo kuwa 4-0 baada ya kuingia kama mchezaji wa akiba. Leicester wameendelea kuimarisha nafasi yao ya kutwaa kombe lao la kwanza la ligi ya EPL walipoibana Southampton kwa bao 1-0.Nahodha wa The Foxes Wes Morgan alitumia vyema pasi safi ya Christian Fuchs na kuiweka Leicester alama 7 kileleni mwa jedwali la ligi kuu huku wakiwa wamesalia na mechi 6 kukamilisha msimu huu kwa kishindo. Matokeo mengine ya mechi zilizopigwa wiki iliyomalizika katika Ligi ya Premier ni kama yafuatayo: Bournemouth 0 Man City 4; Norwich 3 Newcastle 2; Stoke 2 Swansea 2; na Sunderland 0 West Brom 0.

5 bora kwenye msimamo wa EPL: (Leicerster-69, Tottenham-62, Arsenal-58, Man City-54, Man U-53).

El-Classico: Real Madrid 2-1 Barcelona

Klabu ya Real Madrid iliondoka na pointi 3 muhimu katika debi maarufu la El-Classico baada ya kuichabanga Barcelona mabao 2-1 katika mchuano wa Ligi ya Uhispania maarufu La Liga. Uwanja wa Camp Nou uliokuwa umebeba mashabiki zaidi ya 99 elfu ulishudia kitimutimu hicho cha aina yake siku ya Jumamosi ambapo Madrid walikuwa wanakipiga wachezaji 10 baada ya kiungo wake Sergio Ramos kupigwa kadi nyekundu. Barca ndio waliotangulia kuona nyavu kupitia bao la kichwa la dakika ya 56 lililotiwa kimyani na Gerard Pique. Dakika 6 baadaye, Karim Benzema alisawazisha mambo kwa bao lake la dakika ya 62 kabla ya kiungo mahiri wa Madrid Cristiano Ronaldo kufanya mambo kuwa 2-1, kupitia bao lake la dakika ya 85. Licha ya kichapo hicho, Barcelona wanaongoza msimamo wa La Liga kwa pointi 76 wakifuatwa na Atletico Madrid wenye alama 70. Ingawa ushindi huo umeifanya Madrid ikaongeza alama 3 muhimu, lakini imelazimika kutia nanga kwa sasa katika nafasi ya 3 ya Ligi ya Uhispania ikiwa pointi 69.

Dondoo: Wabahrain waandamana dhidi ya Mashindano ya Formula 1

Wimbi la maandamano limeshuhudiwa wiki iliyomalizika katika miji mbali mbali ya Bahrain kupinga kufayika mashindano ya magari ya langa langa ya Formula One Grand Prix nchini humo. Siku ya Jumamosi, waandamanaji walimiminika katika barabara za kijiji cha Karzakan mjini A’ali, yapata kilomita 3 kusini mashariki  mwa mji mkuu Manama, kupinga kufanyika mashindano hayo nchini humo, kutokana na kile walichokitaja kuwa, njama za utawala wa Aal-Khalifa za kupotosha fikra za walio wengi kuhusiana na ukandamizaji na dhulma unazozifanya. Waandamanaji hao ambao walikuwa wamebeba mabango na maberamu yaliyokuwa na picha za magari ya langa langa yaliyofunikwa na damu, wamesema kuruhusu kufanyika mashindano hayo ni sawa na kutoa kibali cha ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na watawala wa Manama. Maandamano mengine kama hayo yalifanyika katika vijiji vya Diraz na al-Dair. Siku ya Ijumaa, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilikashifu hatua ya Bahrain kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kimataifa wakati ambapo imekataa kata kata kuheshimu sheria za kimataifa. Tangu mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa malalamiko ya wananchi dhidi ya siasa za utawala wa kidikteta wa Aal Khalifa. Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International, Human Rights Watch na mengineyo yameukosoa mara kadhaa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na utawala wa Aal Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain.

………………………TAMATI……………………..

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …