Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 28 Machi 2016 11:33

Ulimwengu wa Michezo, Machi 28

Ulimwengu wa Michezo, Machi 28

Iran yaizaba India 4-0 Tehran

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeichabanga India mabao 4-0 katika mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia mwaka 2018.

Katika kipute hicho kilichopigwa katika uwanja wa Azadi jijini Tehran, vijana wa Iran walionyesha mchezo mzuri katika kipindi chote, na kuupa maana msemo usemao ‘mcheza kwao hutuzwa.’ Nahodha wa Iran Ehsan Hajsafi alifungua mlango wa mabao kupitia mkwaju wa penalti kunako dakika ya 33, baada ya kiungo Alireza Jahanbakhsh kuchezewa visivyo katika eneo la hatari.

Sardar Azmoun alifunga bao la pili kabla ya Hajsafi kuongeza la tatu, ambalo lililikuwa lake la pili katika mchuano huo katika dakika 66 ya mchezo. Jahanbakhsh naye hakuachwa nyuma, alifunga lake la pili kunako dakika ya 78 na kupiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Wahindi waliokuwa wakiupiga ugenini.

Licha ya mvua ya mabao, lakini mkufunzi wa Iran Carlos Queiroz alisisitiza kuwa vijana wake walipoteza fursa nyingi za kuongeza mabao.

Kwa ushindi huo, Iran inasalia kileleni mwa Kundi D ikiwa na pointi 17 huku ikitazamiwa kutoana jasho na Oman mnamo Machi 29. India ambayo iko katika nafasi ya 5 ikiwa na pointi 3, itakutana na Turkmenistan siku hiyo.

Voliboli: Iran yang’ara China

Timu ya taifa ya wanaume ya voliboli ya kuketi chini ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Dunia la Voliboli ya Walemavu mwaka huu 2016 nchini China. Katika kipute cha fainali kilichopigwa katika uwanja wa Inji mjini Hangzhou, timu ya Iran iliipeleka mchakamchaka Brazil na kuizaba seti tatu za mpigo za 25-20, 25-13 na 25-14 na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo yajulikanayo kama World Paravolley Intercontinental Cup. 

Kiungo wa Iran, Davoud Alipourian aliteuliwa kuwa mchezaji bora mwenye thamani katika mashindao hayo ya dunia. Brazil ambayo iliibuka katika nafasi ya pili ililazimika kuridhika na medali ya fedha huku mabingwa wa Iran wakirudi nyumbani na dhahabu. Timu ya taifa ya wanawake ya Iran katika mchezo huo iliibuka katika nafasi ya 5 siku ya Jumanne. Timu ya Marekani ndiyo iliyotwaa ubingwa wa mchezo huo kwa upande wa wanawake baada ya kuichabanga mwenyeji China seti 3-1, za 25-22, 12-25, 25-20 na 28-26. Mashindano hayo ya kimataifa ya voliboli ya walemavu yalianza Machi 17 na kufunga pazia lake Machi 23.

Michuano ya AFCON

Michuano ya kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON iliendelea kurindima wiki iliyomalizika; baadhi ya nchi ziking’ara huku zingine zikibanduliwa na kukosa tiketi ya kusonga mbele. Timu ya taifa ya Congo-Brazzaville ilifanya vizuri kwa kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na timu ya taifa ya Zambia siku ya Jumatano, Machi 23, 2016. Matokeo hayo yameiweka Brazzaville katika nafasi nzuri kwenye kundi E. Kenya ambayo ikiwa ugenini iliangukia pua kwa kufungwa na Guinea-Bissau bao 1-0, wameshindwa kung’ara nyumbani katika mchuano wa marudiano na kuzabwa bao 1-0, mchuano uliojaa mihemko na patashika katika Uwanja wa Taifa wa Nyayo.

Vijana wa The Cranes ya Uganda ambao walishindwa kung’ara nyumbani, wamechachawizwa ugegeni pia kwa kulazwa bao 1-0 na Burkina Faso, katika kipute kilichopigwa Jumamosi mjini Ougadougou.

Wakati huo huo timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars wamejiandikishia alama 3 muhimu baada ya kuimenya timu ya taifa ya Chad bao 1-0. Huku hayo yakijiri, Chad imechukua uamuzi wa kujiondoa katika kinyang'anyiro cha kufuzu kwa fainali ya AFCON inayotarajiwa kupigwa mwakani nchini Gabon. Shirikisho la Soka la Chad limechukua uamuzi huo kutokanana kile kilichotajwa kuwa, ukosefu wa fedha. Moctar Mahamadou, Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Chad amelituma barua Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), akiliambia kuwa wanakabiliwa na ukosefu wa fedha za kufadhili safari ya kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mechi ya marudiano dhidi ya Taifa Stars Jumatatu hii ya Machi 28, 2016. Kufuatia uamuzi huo wa Chad, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limefuta matokeo ya mechi zote ya Chad, na hivyo kuiacha katika njia panda timu ya taifa ya Tanzania. Wakati huo huo CAF imeipiga marufuku Chad kushiriki mashindano ya mwaka wa 2019 pamoja na kuitoza faini ya dola 20 elfu za Marekani. Hayo yakijiri Benin wameshindwa kufanya vizuri na kukubali kichap cha mabao 2-0 kutoka Sudan Kusini. Nigeria pia ilishindwa kutamba ilipokutana na Misri licha ya kuwa walikuwa wanaupiga nyumbani, na mchuano huo kuishia kwa sare ya goli 1-1. 

Matokeo mengine ya michuano ya AFCON iliyopigwa Machi 26:

Mauritius 1-0 Rwanda, Ushelisheli 2-0 Lesotho,

Burundi 1-3 Namibia, Cameroon 2-2 Afrika Kusini, Kongo DR 2-1 Angola.

………………MUZIKI………………

Dondoo: Bingwa soka Johan Cruyff aaga dunia

Johan Cryuff, mmoja wa wachezaji soka wakongwe na stadi duniani ameaga dunia, baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu. Raia huyo wa Uholanzi aliyekuwa na umri wa miaka 68 alifariki dunia nyumbani kwake mjini Barcelona Alkhamisi iliyopita ya Machi 24. Cryuff ambaye aliwahi kuchezea klabu maarufu ya Barcelona; atakumbukwa kwa umbuji wake na namna alivyokuwa amekubuhu katika mpira wa mguu; haswa alivyoisaidia timu yake ya Uholanzi kutinga fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1974. Hata hivyo timu hiyo ilikubali kichapo katika mchuano huo kutoka kwa Ujerumani. Cruyff pia atakumbukwa kwa kuiongoza klabu ya Ajax kutwaa Kombe la Uropa mara tatu mfululizo, kati ya mwaka 1971 na 1973. Nyota yake katika uga wa soka haikufifia, mwaka 1992, mchezaji huyo mashuhuri alianza kuwanoa vijana wa klabu ya The Catalan na kuifanya iibuke mshindi kwa mara ya kwanza katika mashindao ya Kombe la Uropa. Kadhalika katika kipindi cha miaka 8 ya kuisimamia Barca, Cryuff aliiwezesha klabu hiyo kutwaa taji la La Liga mara nne mfululizo. Mchezaji huyo aligonga vichwa vya habari duniani mwaka 1991, kwa kufichua kuwa alifanyiwa upasuaji wa moyo kutokana na uraibu wake wa kuvuta sigara. Oktoba mwaka jana mchezaji huyo ambaye amewahi kutwaa taji la mchezaji bora duniani mara 3, alifichua kuwa anaugua saratani. Kocha wa timu ya taifa ya Iran Carlos Queiroz ni mmoja wa shakhsia watajika duniani waliyotuma salamu za rambi rambi kwa familia, jamaa na marafiki wa Johan Cryuff kutokana na kifo cha mwanasoka huyo aliyekuwa amebobea katika uga wa mpira wa miguu.

………………TAMATI………………….

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …