Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 14 Machi 2016 12:56

Ulimwengu wa Michezo, Machi 14

Ulimwengu wa Michezo, Machi 14

Iran yatwaa ubingwa wa Riadha ya Asian-Oceanic UAE

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Mashindano ya Riadha ya Walemavu ya Asian-Oceanic, yaliyofanyika mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Wanaspoti wa Iran wameibuka kidedea baada ya kusanya jumla ya medali 40 zikiwemo 23 za dhahabu, 10 za fedha na 7 za shaba katika michezo tofauti. China imeibuka ya pili katika mashindano hayo ya ubingwa ya walemavu yajulikanayo kama IPC Athletics Championship kwa kuzoa medali 30, zikiwemo 16 za dhahabu, 9 za fedha na 5 za shaba; ikifuatwa na India ambayo inafunga orodha ya tatu bora kwa kuondoka na medali 12 za dhahabu, 10 za fedha na 9 za shaba. Mashindano hayo yaliyowaleta pamoja wanamichezo takriban 300 kutoka nchi 30 duniani yalianza Machi 6 na kufunga pazia lake Jumamosi ya Machi 12. Wanaspoti 29 wa kike na kiume wa Iran waliiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu katika michezo ya kurusha kisahani, kitufe na mbio za aina kadhaa katika mashindano hayo ambayo huandaliwa na Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Walemavu IPC.

Mwanamasumbwi wa Iran akataa kuzipiga na Mzayuni

Mchezaji wa timu ya taifa ya ndondi ya Iran amekataa kupigana na mchezaji mwenziwe wa utawala haramu wa Israel katika mashindano ya kimataifa ya ndondi ya Njia ya Hariri yanayofanyika Baku nchini Azerbaijan, akionyesha uungaji mkono wake kwa taifa linalodhulumiwa la Palestina. Katika mashindano hayo ya kimataifa ya ndondi yaliyoanza Alkhamisi katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan, mwanamasumbwi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mas'ud Abdullahi anayezipiga katika uzani wa kilo 69 aligoma kupigana na mwanamasumbwi kutoka Israel, akipinga jinai zinazofanywa na utawala huo dhidi ya raia wa Palestina na uungaji mkono wake kwa taifa hilo linalodhulumiwa. Wanamichezo wa Iran na baadhi ya nchi za Kiislamu daima wamekuwa wakilitetea taifa la Palestina dhidi ya utawala haramu wa Israel katika medani mbalimbali za kimataifa, kwa kususa kucheza na wawakilishi wa utawala huo katili unaoendelea kuua raia wasio na hatia wa Palestina na kukalia kwa mabavu ardhi na nchi yao.

Afrika: Ndondi

Wanamasumbiwi wa Kenya na Ethiopia wametinga robo fainali ya mashindano ya ndondi ya bara Afrika yanayoendelea nchini Cameroon. Nick Okoth wa Kenya na Mesfin Keralah wa Ethiopia Jumapili usiku walishinda mapigano yao ya uzani mwepesi katika mashindano hayo ya kibara, ya kufuzu kwa michezo ya Olympiki, yanayoendelea huko Yaounde, mji mkuu wa Cameroon. Hata hivyo mambo yalimtumbukia nyongo bondia wa Uganda Sulaiman Segawa aliyeshindwa na Reda Benbaziz wa Algeria katika kitengo cha uzani wa mwepesi licha ya kushinda mchuano wake wa ufunguzi. Okoth naye alitolewa jasho na Mohlerepe Qhobosheane wa Lesotho kabla ya kuibuka mshindi wa pointi 2-1, huku Kerale wa Ethiopia akimshinda Paulo Britos wa Msumbiji. Kibarua kinachomsubiri Okoth wa Kenya sasa kuzipiga na Reda Benabaziz wa Algeria katika hatua ya robo-fainali Jumatano wiki hii wakati ambapo Kerale wa Uhabeshi atakuwa anazipiga na Andrik Allisop wa Ushelisheli. Bondia mwingine wa Kenya ambaye ametinga robo-fainali ni Rayton Okwiri ambaye alifuzu moja kwa moja baada ya droo kufanyika. Okwiri atakutana ima Christian Abua wa Nigeria au Adamou Kohautto kwenye robo fainali. Katika uzani mzito matumaini ya Kenya na Uganda kusonga mbele yalizimwa na mabondia kutoka Misri na Nigeria. Fredrick Ramogi wa Kenya alishindwa kwa wingi wa pointi na Mostafa Hafez wa Misri naye Michael Dekabembe akaondolewa kwa pointi na Efe Ajagba wa Nigeria. Uganda walishinda mapigano ya ufunguzi siku ya Ijumaa katika mashindano ya bara Afrika ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki.Sulaiman Segawa uzani wa light alimtandika vilivyo Stephen Kabelo wa Botswana na kutia kibindoni pointi 3-0, huku Kennedy Katende akimpondaponda Yoada Aboubacar wa Ivory Coast kwa pointi 3-0. Tanzania ilitangaza kujiondoa katika mashindano hayo ya kibara kutokana na kile kilichotajwa kuwa ‘uhaba wa fedha.’

Kenya: Kudhibiti matumizi ya dawa za kusisimua misuli

Nchini Kenya sheria ya kudhibiti utumizi wa dawa za kututumua misuli huenda ikiwa tayari kufikia mwezi ujao wa Aprili. Hii ni baada ya Kamati ya Leba ya Bunge la Kitaifa nchini humo kupasisha mapendekezo ya mbunge wa Cherengany Wesley Koriri.

Kombe la Klabu Bingwa Afrika

Kindumbwendumbwe cha michuano ya Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika kiliendelea Jumapili kwa mechi kadhaa kushuhudiwa. Miongoni mwa matokeo ya mechi hizo: Enyimba ya Nigeria iliizamisha Vitaloo ya Burundi kwa kuichapa mabao 5-1. St George ya Ethiopia iliilazimisha sare ya mabao 2-2 TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati ambapo Union Douala ya Cameroon ilikuwa inapokea kichapo cha bao 1-0 kutoka Zamalek ya Misri. Katika Michuano ya Kombe la Shirikisho (Confederation Cup), klabu ya St Eloi Lupopo ya DRC imeifunga Ahli Shendi ya Sudan mabao 2-1, Al Ittihad ya Libya imeichabanga Medeama ya Ghana bao 1-0 sawa na ilivyotandikwa Constantine ya Algreria walipocheza  na Nasarawa ya Nigeria. Michuano hiyo inatazamiwa kuendelea Machi 18.

Kombe la FA

Michuano ya Kombe la FA iliendelea kurindima tena Jumapili huku klabu ya Arsenal ikivuliwa ubingwa wa taji hilo baada ya kuchachawizwa na Watford kwa kuzabwa mabao 2-1. Mabao ya Watford yalifungwa na Odion Ighalo na Adlene Guedioura huku bao la kufutia machozi la Wabeba Bunduki likifungwa na Danny Welbeck.

Kichapo hicho kimezidi kuamsha ghadhabu za mashabiki wa Gunners ambao wamekuwa wakishikiniza kuwa wakati umefika kwa mkufunzi Arsene Wenger aachie ngazi. Miongoni mwa makocha wanaopigiwa upatu kurithi mikoba ya Wenger ni pamoja na Manuel Pelegrini, Brendan Rodgers, Steve Bould, Diege Simeone na Pank de Boer. Katika mchuano mwingine Manchester United wakiwa nyumbani walibanwa na West Ham na kulazimishwa sare ya bao 1-1. Goli la West Ham lilifungwa na Dimitri Payet katika kipindi cha pili kunako dakika ya 68, huku bao la kusawazisha la Man U likipachikwa kimyani na Anthon Martial, zikiwa zimesalia dakika 7 kabla ya kupigwa kipenga cha kufunga mchezo.

Dondoo: Mambo yazidi kuwa mazito kwa Sharapova

Kitumbua cha Maria Sharapova, nyota wa mchezo wa tenisi, mfanyabiashara na mmoja wa wanaspoti tajiri zaidi duniani, kimeingia mchanga na tayari baadhi ya wadhamini wake wameanza kujitenga naye; siku chache baada ya kukiri kuwa amekuwa akitumia dawa za kusisimia misuli.

Kampuni ambazo tayari zimetangaza kuvunja uhusiano na Sharapova ni Nike, Tag Heuer na Porsche. Siku chache zilizopita, Sharapova alikiri kutumia dawa hizo kwa takriban mwaka mmoja.

Mwaka 2010, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, aliingia kwenye mkataba wa miaka minane na kampuni ya jezi za michezo ya Nike, uliokuwa na thamani ya dola milioni 70 za Marekani, pamoja na malipo ya nguo zake za kibinafsi. Kwa mujibu wa jariba la Forbes la Marekani,  Sharapova ndiye mchezaji wa kike anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani. Mwaka jana pekee, nyota huyo wa tenisi alipokea dola milion 30 za Marekani kutokana na ushindi wa michuano mbali mbali pamoja na vitita vikubwa vya fedha kutka kampuni zinazomfadhili.

.............................TAMATI..................................

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …