Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 07 Machi 2016 10:51

Ulimwengu wa Michezo, Machi 7

Ulimwengu wa Michezo, Machi 7

Iran bingwa wa karate Asia

Timu ya taifa ya karate ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya mchezo huo barani Asia mwaka huu 2016 yaliyofanyika mjini Kermanshah nchini hapa. Nabi Fathi, afisa wa Shirikisho la Karate nchini amesema timu ya wanakarate wa kiume ya Iran imeibuka ya kwanza katika mashindano hayo yajulikanayo kama Asian Fudokan International Championship, yaliyofanyika magharibi mwa nchi. Afghanistan imeibuka ya pili huku orodha ya tatu bora kwa upande wa wanaume ikifungwa na Iraq.

Kadhalika timu ya karate mtindo wa fudokan ya Iran kwa upande wa wanawake imetwaa ubingwa katika mashindano hayo ya kieneo yaliyopigwa katika uwanja wa Shahid Beheshti, huku Iraq na Afghanistan zikitwaa nafasi za pili na tatu kwa usanjari huo.

Mashindano hayo yaliwaleta pamoja wanakarate 900 kutoka Iran, Iraq, Afghanistan, Azerbaijan na Tajikistan. Mashindano hayo ya Asian Fudokan International Championship yalianza Machi 3 na kufunga pazia lake Machi 4. Fudokan ni aina ya karate ya kale, iliyoasisiwa mwaka 1980 na ndugu wawili Ilija Jorga na Vladimir Jorga wa Russia, kama njia moja ya mazoezi ya mwili na akili, aghalabu ya walioucheza wakati huo walikuwa watu wenye visomo.

Mieleka: Iran yatwaa taji la Yadegar Imam

Timu ya taifa ya mieleka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa Kombe la Yadegar Imam katika mashindano ya kimataifa ya mieleka mwaka huu 2016 yaliyofanyika nchini hapa. Katika siku ya mwisho ya mashindano hayo Ijumaa usiku katika uwanja wa Azadi magharibi mwa Tehran, timu ya mieleka mtindo wa freestyle ya Iran iliibuka mshindi baada ya kunyakua medali 7 za dhahabu katika vitengo vya wanamieleka wenye kilo 46, 50, 54, 63, 69, 76 na 100. Katika kitengo hicho cha freestyle, Armenia ilimaliza ya pili huku timu ya Iran B ikimaliza katika nafasi ya 3. Ugiriki, Azerbaijan, Georgia na Ukraine zilimaliza katika nafasi za 4,5,6 na 7 kwa utaratibu huo.

Katika safu ya mieleka mtindo wa Greco-Roman, Iran iling’ara tena kwa kujishindia medali 7 za dhahabu huku nafasi ya pili na tatu zilichukuliwa na Azerbaijan na Iran B. Armenia, Kyrgyzstan, Iran C na Ukraine zimemaliza katika nafasi ya 4,5,6 na 7 kwa usanjari huo. Duru ya 6 ya mashindano hayo yajulikanayo kama Yadegare Imam Cup International yalifanyika kati ya Machi 3 na 4 hapa jijini Tehran.

Soka: Tanzania

Timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ililazwa na Zimbabwe kwenye mechi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake 2016 mwishoni mwa wiki. Twiga Stars walichapwa mabao 2-1 na Zimbabwe katika mechi iliyochezewa uwanja wa Azam complex jijini Dar es Salaam. Magoli ya Zimbabwe yalifungwa na mchezaji Elina Jeke.

Bao la kufutia machozi la Twiga Stars lilitiwa kimyani na Mwanahamisi Omar. Kocha wa timu ya Taifa ya soka ya wanawake, ‘Twiga Stars’, Nasra Juma amesema kukosekana kwa ligi ya wanawake Tanzania ni moja ya sababu zinazofanya timu hiyo kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa.

Kutokana na kipigo cha mabao 2-1, Twiga Stars sasa inahitajika kushinda mabao 2-0 katika mchuano wa marudiano nchini Zimbabwe Machi 18. Mshindi wa mchuano huo atamenyana na mshindi wa mchuano kati ya Zambia na Namibia.

Ligi Kuu Tanzania

Klabu ya Simba Sport ya Tanzania imekwea kileleni mwa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara baada ya kuichabanga Mbeya City mabao 2-0. Mabao ya Wekundu hao wa Msimbazi yalifungwa na Daniel Lyanga na Ibrahim Ajib. Kwa sasa Simba wananguruma kileleni mwa jedwali la ligi kwa alama 48 wakiwa wamecheza mechi 21, wakifuatiwa na mahasimu wao wa jadi Yanga wenye alama 47, walizozizoa kwenye michuano 20, alama ilizonazo Azam ingawa wanatofautiana na Yanga kwa idadi ya magoli. Ligi hiyo itaendelea tena Jumanne hii kwa mchezo mmoja wa kisisimua, ambapo Yanga wanatazamiwa kushuka dimbani kumenyana na African Sports ya Tanga.

Ligi Kuu Kenya

Watani wa jadi wa mpira wa miguu nchini Kenya klabu ya Gor Mahia na AFC Leopards walivaana siku ya Jumapili katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi, kumenyana katika mchuano wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya soka nchini humo mwaka huu 2016. Bao la Ingwe lilipachikwa kimyani na mtoka benchiLaminne Diallo kunako dakika ya 83, baada ya kuunganisha krosi safi iliyochongwa na Yussfu Juma.

Na ngoma ya kiutamaduni ya jamii ya Waluhya ya isukuti ikapigwa baada ya ushindi huo.

Mara ya kwanza timu hizi kukutana ilikuwa mwaka 1968, mchuano ambao Gor Mahia walishinda kwa mabao 2 kwa 1. AFC Leopards wanapokutana na Gor Mahia huwa ni mchuano unaozua hisia nyingi sana nchini humo, na katika miaka ya hivi karibuni, kitimutimu hicho kimepewa jina la Debi la Mashemeji.

 

Ligi Kuu ya Uingereza

Ligi Kuu ya Uingereza iliendelea kurindima mwishoni mwa wiki huku mchuano kati ya Arsenal na Tottenham na ule wa Manchester United dhidi ya West Brom zikiteka fikra na nyoyo za mashabiki wengi wa soka. Bao la pekee la Solomon Rondon wa Westbrom la dakika ya 66 katika mchuano wa Jumapili ugani Hawthorns uliokuwa na mashabiki karibia 25 elfu, lilitosha kuwashusha Mashetani Wekundu wa Man U kutoka nafasi ya 5 na kuwasukuma hadi katika nafasi ya 6.

Huenda wageni Man U walishinda kufurukuta mbele ya mwenyeji wake kutoka na mshtuko walioupata baada ya kiungo wake Juan Mata kulishwa kadi nyekundu. Majogoo wa Anfield ama ukipenda Liverpool nao wamepata pointi 3 muhimu baada ya kuizaba Crystal Palace mabao 2-1 wakicheza ugenini kwenye dimba la Selhurst Park. Kwengineko Alexis Sanchez wa Arsenal alisawazisha mambo na kuifanya timu yake iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani kupata pointi moja huku timu ya Tottenham Hotspurs ikikosa fursa muhimu ya kupanda katika uongozi wa jedwali la ligi.Bao la Aaron Ramsey liliiweka mbele Arsenal kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.Kiungo wa kati wa Arsenal Francis Coquelin alipewa kadi nyekundu baada ya dakika 55 alipomchezea visivyo Harry kane na kutoa fursa kwa Spurs kujibu mapigo kwa kufunga mabao mawili ya haraka.Toby Alderweireld alifunga bao la kwanza la Tottenham kabla ya Harry Kane kufanya mambo kuwa 2-1.Lakini Arsenal ilikataa kukubali kushindwa na kusawazisha dakika 14 kabla mchezo kukamilika kupitia kiungo Sanchez.

Leicester ambayo iliilaza Watford bao 1-0 inasalia kileleni mwa ligi ikiwa na pointi 60 huku Tottenham licha ya kulazimishwa sare inasalia katika nafasi ya pili ikiwa na alama 55 ikifuatwa na Gunners wenye pointi 52. Man City ambayo iliinyoa Aston Villa kwa chupa kwa kuisasambua mabao 4-0 wapo katika nafasi ya 4 wakiwa na pointi 50, alama 1 mbele ya West Ham United ambao wanafunga nafasi ya 5 bora ya msimamo wa Ligi ya Premier.

…………………………TAMATI…………………………..

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …