Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 29 Februari 2016 10:26

Ulimwengu wa Michezo, Feb 29

Ulimwengu wa Michezo, Feb 29

Taekwondo: Iran yashinda dhahabu 2 UAE

Timu ya taifa ya taekwondo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshinda medali kochokocho ikiwemo dhahabu 2 katika duru ya 4 ya Mashindano ya Taekwondo ya Fujairah Open mwaka huu 2016 katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Siku ya Alkhamisi, Omid Amidi aliipa Iran dhahabu ya pili katika mechi ya fainali ya wanataekwondo wenye kilo zisizozidi 87, alipomlemea raia wa Norway Muhammed Elhatri na kumshinda kwa pointi 10-2. Muirani huyo alitinga fainali baada ya kuwazidi raia wa Hong Kong na Kazakhstan katika michezo ya ufunguzi. Awali Armin Hadipour aliipa Iran dhahabu ya kwanza katika kitengo cha wacheza-taekwondo wenye kilo zisizodidi 54 siku ya Jumatano. Ahmad Khosrowfar aliipa Iran ya Kiislamu medali ya fedha katika kitengo cha kilo zisizozidi 74 katika mashindano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Khalifa. Mashindano hayo taekwondo ya Fujaira Open yaling’oa nanga Februari 23 na kumalizika Februari 25 huko Imarati. Makumi ya wanataekwondo walishiriki mashindano hayo kutoka nchi mbali mbali duniani, ikiwemo Misri, Cyprus, Hong Kong, Iran, Kazakhstan, Norway, Qatar, Imarati na Uzbekistan.

Iran yaanza vizuri mashindano ya tenisi Malaysia

Timu ya taifa ya mchezo ya tenisi ya Iran imeanza vyema katika mashindano ya kimataifa ya mchezo huo nchini Malaysia, baada ya kuizaba Thailand seti 3-2. Katika mchezo wa kwanza, hatua ya makundi siku ya Jumapili katika uwanja wa Malawati eneo la Sham Alam, timu ya wanaume ya Iran ya mchezo wa tenisi ambayo inanolewa na Jami Lotfollah iliichapa Thailand seti 3-2 katika mchezo uliopigwa jijini Kuala Lumpur.

Nchi zaidi ya 90 zinashiriki katika mashindano hayo ya dunia yaliyoandaliwa na Shirikisho la Tenisi Duniani ITTF. Timu ya Iran ya wanaume inawajumuisha Mohammad Reza Akhlaghpasand, Afshin Norouzi, mandugu Noshad na Nima Alamian pamoja na Pouria Omrani. Kwa upande wa wanawake, Iran inawakilishiwa na Neda Shahsavari, Mahjoubeh Omrani, Maryam Samet na Ghazaleh Mollatalab. Mashindano hayo ya dunia mchezo wa tenisi yanayojulikana kama Perfect World Team Championship yalianza Jumapili ya Februari 28 na yanatazamiwa kumalizika Mei 6.

Muirani anunua 50% ya hisa za Everton

Mfanyabiashara raia wa Iran, Farhad Moshiri amenunua asilimia 49.9 ya hisa za klabu ya Everton, ambayo inacheza katika Ligi Kuu ya Uingereza. Imearifiwa kuwa Moshiri ambaye aliwahi kuwa mdau mkubwa katika klabu ya Arsenali ametoa yuro milioni 200 sawa na dola milioni 277 za Marekani ili kununua hisa hizo katika klabu hiyo ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya 12 ya msimamo wa Ligi ya Premier. Moshiri ambaye kwa mujibu wa jarida la kibiashara la Forbes la Marekani, ana utajiri wa dola bilioni 1.3 za Marekani, amesema: “Ninafurahi kuwa na hisa katika klabu ya Everton yenye utajiri wa turathi na ambayo inafanya vyema kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.” Bill Kenwright, Mwenyekiti wa Everton amesema kuwa amefurahi mno kwa Moshiri kuwa mwanahisa na mdau wa klabu hiyo. Siku ya Ijumaa, Moshiri mwenye umri wa miaka 60 aliuza hisa zake za klabu ya Gunners kwa mjasiriamali mwenzake, Alisher Usmanov.

SOKA AFRIKA MASHARIKI

Michuano ya klabu bingwa bingwa barani Afrika imeendelea kurindima; baadhi ya timu zikijikatia tiketi ya kusonga mbele na zingine zikibanduliwa kwenye mashindano hayo ya kibara. Siku ya Jumamosi, klabu ya Yanga ya Tanzania ilipata ushindi wa mabao 2-0 iliposhuka dimbani kumenyana na klabu ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika mchezo wa marudiano. Yanga ilianza kupata bao la mapema dakika ya tatu mfugaji akiwa Amiss Tambwe kutokana na krosi iliyochongwa na Simon Msuva.

Wageni walijitahidi kupanga mashambulizi dakika za mwanzo kipindi cha pili, lakini walijikuta wakipachikwa bao la pili dakika ya 56 kupitia kiungo Thabani Kamusoko kwa shuti lilitokana na mpira wa adhabu wa Juma Abdul. Yanga walikuwa katika nafasi nzuri ya kuendelea na hatua inayofuata, baada ya mchezo wa kwanza waliocheza Mauritius kuibuka na ushindi wa goli 1-0, hivyo Cercle de Joachim walikuwa kwa nia ya kupata ushindi ili waendelea hatua inayofuata. Yanga sasa wanatazamiwa kusafiri Kigali mwanzoni mwa mwezi Machi, kucheza na APR ya Rwanda katika hatua inayofuata.

Kwengineko, matumaini ya klabu ya Kenya Gor Mahia kusonga mbele katika kombe la Klabu Bingwa barani Afrika CAF yalizimwa siku ya Jumamosi baada ya kupoteza mechi ya marudiano ya mchuano huo ugenini. Gor Mahia walilazwa bao 1-0 na klabu ya CnaPs ya Madagascar.

Tukiachana na hayo, mkutano wa dharura wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), umeiondoa Kamati ya Muda ya chama hicho, huku pia ukimuondoa madarakani Makamu wa Rais wa ZFA Unguja, Haji Ameir Haji. Uamuzi huo ulifikiwa katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki visiwani humo chini ya Mwenyekiti wa chama hicho Ravia Idarous. Akisoma maazimio ya mkutano huo, Makamu wa Rais wa ZFA, Pemba, Ali Mohammed alisema uamuzi wa kumuondoa Haji Ameir ulifikiwa kwa kura za ndiyo za wajumbe 43 kati ya 47 waliohudhuria mkutano huo. Licha ya kuondolewa katika wadhifa huo, pia Makamu huyo wa Rais amefungiwa asijihusishe na soka kwa miaka minne akidaiwa kukiuka katiba ya ZFA kwa kupeleka masuala ya soka mahakamani. Alisema pia mkutano huo umeiondosha Kamati ya Muda ya ZFA Taifa iliyokuwa ikisimamia masuala ya mpira kwa kukiuka katiba ya chama hicho kwani masuala ya mpira yanasimamiwa na Kamati ya Utendaji.

Ligi ya EPL

Mabao 2 ya tineja wa miaka 18 Marcus Rashford yaliisaidia Mau U kupata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Arsenali katika mchuano wa kusisimua wa Ligi Kuu ya Uingereza uliopigwa ugani Old Trafford siku ya Jumapili. Katika mchuano huo uliosakatwa mbele ya mashabiki zaidi ya 75 elfu, Rashford ndiye aliyekuwa wa kwanza kucheka na nyavu, kupitia goli lake la dakika ya 29. Hata kabla ya mate kukauka, chipukizi huyo alipachika kimyani bao la pili dakika 3 baadaye, huo ukiwa mchuano wake wa kwanza ligi ya EPL.

Danny Welbeck alihuisha matumaini ya vijana wa Arsene Wenger kupitia bao lake la dakika 40. Baada ya mapumziko, Anders Herrera wa mashetani wekundu alipachika kimyani bao la 3 kunakako dakika ya 65 na kufifisha tena matumaini ya wabeba bunduki. Dakika 4 baada ya goli hilo, Arsenali walijizoazoa na kufunga bao la pili kupitia kiungo Messut Ozil.

Licha ya ushindi huo, Mau U wanasalia katika nafasi ya 5 wakiwa na pointi 44 huku Arsenali wakizidi kutuama katika nafasi ya 3 wakiwa na pointi 51. Huku hayo yakijiri, watu 24 waliuawa mjini Baidoa Kusini mwa Somalia wakitizama mechi hiyo ya mahasimu wa jadi wa Ligi Kuu ya Uingereza. Habari zinasema kuwa, milipuko miwili mikubwa ilitokea katika mkahawa uliokuwa umejaa mashabiki wa timu hizo mbili usiku wa Jumapili. Shambulizi hilo lilitokea masaa machache baada ya kumalizika mkutano wa viongozi wa nchi zinazochangia wanajeshi wake kwenye vikosi vya muungano wa Afrika AMISOM uliofanyika nchini Djibouti.

Leicerster City wanasalia kileleni mwa jedwali la Ligi ya Premier wakiwa na pointi 56, baada ya kuendeleza wimbi lake la ushindi kwa kuitandika Norwich bao 1-0. Tottenham ambayo iko katika nafasi ya pili, ilipata alama 3 muhimu baada ya kuichabanga Swansea mabao 2-1 na hivyo kuongeza alama zake hadi 54. Man City ambayo haina budi kuridhika na nafasi ya 4 ikiwa na pointi 47.

Dondoo: Gianni Infantino arithi mikoba ya Blatter Fifa

Gianni Infantino raia wa Uswisi amechaguliwa kuwa Rais mpya wa Shirikisho la Kandanda Duniani FIFA na kurithi mikoba ya Sepp Blatter aliyeongoza shirikisho hilo kwa miaka mingi. Katibu huyo mkuu wa Fifa alipata kura 115 katika raundi ya pili ikiwa ni kura 27 zaidi ya mpinzani wake wa karibu Sheikh Salman bin Ibrahim al-Khalifa wa Bahrain ambaye kwa sasa ni rais wa Shirika la Soka barani Asia. Mwanamfalme Ali bin al-Hussein wa Jordan alikuwa wa tatu akiwa na kura nne. Jerome Champagne mwanadiplomasia wa Ufaransa aliambulia patupu baada ya kushindwa kupata hata kura moja. Tokyo Sexwale kutoka Afrika Kusini alijiondoa kabla ya kura kuanza kupigwa mjini Zurich.  Raundi ya kwanza ya upigaji kura ilishindwa kumpata mshindi wa moja kwa moja. Wingi wowote wa kura[zaidi ya aslimia 50] katika raundi ya pili ya uchaguzi huo ulikuwa unaweza kumwezesha mgombea kutangazwa mshindi katika raundi ya pili. Infantino ni wakili mwenye umri wa miaka 45 kutoka eneo la Brig jimbo la Valais nchini Switzerland ,ikiwa ni eneo lililopo chini ya maili sita kutoka nyumbani kwa Blatter. Blatter ambaye aliliongoza shirikisho hilo tangu mwaka 1998 alijiondoa mwaka uliopita kabla ya kupigwa marufuku katika shughuli zozote za kandanda kwa kipindi cha miaka sita. Baada ya kutangazwa mshindi, Infantino aliwaambia wajumbe waliopiga kura kwamba hakuweza kujielezea kutokana na hisia alizokuwa nazo. Lakini aliwaambia wajumbe kwamba ”kwa pamoja wataweza kuirudisha sura halisi ya Fifa na heshima yake”.

……………………TAMATI…………………….

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …