Tovuti Hii Imefungwa. Tumehamia Kwenye Parstoday Kiswahili
Jumatatu, 22 Februari 2016 10:43

Ulimwengu wa Michezo, Feb 22

Ulimwengu wa Michezo, Feb 22

Futsal: Iran yatwaa kombe la AFC Championship

Timu ya taifa ya Iran ya mchezo wa futsal imetwaa kombe la mabingwa wa mchezo huo barani Asia nchini Uzbekistan, hii ikiwa ni mara ya 11 kwa Iran kutwaa taji hilo. Katika kindumbwendubwe cha fainali siku ya Jumapili katika Uwanja wa Taifa wa Uzbekistan jijini Tashkent, vijana wa Iran waliwachabanga wenyeji Wauzbeki mabao 2-1 na hivyo kutwaa ubingwa wa mashindano hayo yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Asia AFC. Dilshod Irsaliev aliiweka kifua mbele Uzbekistan dakika tano baada ya kuanza mchezo na kwa kuwa ngoma ya vijana haikeshi na daima kutangulia sio kufika, Ghodrat Bahadori alisawazisha mambo dakika nne baadaye. Nahodha wa timu ya taifa ya Iran Mohammad Keshavarz alipachika kimyani bao la ustadi dakika 6 kabla ya kwenda mapumzikoni.

Kipindi cha pili kilishuhudia piga nikupige na majaribio ya mabao bila mafanikio hadi kipenga cha kumaliza mchezo kinapigwa. Awali timu hiyo ya Iran iliicharaza Vietnam mabao 13-1 katika kipute cha nusu fainali siku ya Ijumaa. Farhad Tavakoli alifunga mabao 4, Mehdi Javid (3), Hossein Tayebi(2), Mohammad Keshavarz (2) huku Alireza Vafaei na Hamid Ahmadi wakicheka na nyavu za Wavietnam mara moja kila mmoja. Mapema siku hiyo, mwenyeji Uzbekistan iliitandikaThailand katika mikwaju ya penalty na hivyo kujikatia tiketi ya fainali. Vijana wa mkufunzi Mohammad Nazemosharia sasa watatoana jasho na mwenyeji Uzbekistan Jumapili katika uwanja wa taifa wa Tashkent huku Vietnam na Thailand wakipambana kumtafuta mshindi wa tatu. Vijana wa timu Melli ya Iran ambao kwa sasa wananolewa na Mohammad Nazemosharia, wametwaa taji hilo mara 11 kati ya mara 14 katika historia ya mashindano hayo ya kimataifa. Timu tano bora kwenye mashindano hayo ya AFC Futsal Championship zimejikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la Futsal baadaye mwaka huu nchini Colombia. Mbali na Iran na Uzbekistan, timu zingine ni Australia, Thailand na Vietnam.

Taekwondo: Iran yatwaa ubingwa wa Asia

Timu za Iran za mchezo wa taekwondo kwa upande wa wanaume na wanawake zimetwaa mataji ya Klabu Bingwa ya Taekwondo Barani Asia huko Sharjah, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Klabu ya Iran ya Shahrdari Varamin ya wanaume ilitwaa ubingwa baada ya kupata jumla ya pointi 50 na kujishindia medali 5 za dhahabu na 3 za fedha. Kazakhstan ilimaliza ya pili kwa pointi 37 na kushinda medali 1 ya dhahabu, 1 ya fedha na shaba 1. Nafasi ya 3 ilitwaliwa na al-Nasr ya UAE ambayo ilipata alama 13 pekee.

Kwa upande wa wanawake, vilabu vya Kan na Kourosh vya Iran vilimaliza katika nafasi ya kwanza na pili mtawalia huku nafasi ya 3 ikichukuliwa na klabu ya Kazakhstan. Kan ilipata jumla ya pointi 48 huku Kourosh ikipata alama 22. Kan ilitia kibindoni medali 6 za dhahabu, 1 ya fedha na 1 ya shaba huku Kourosh ikitwaa medali moja ya dhahabu, mbili za fedha na 5 za shaba. Mwanataekwondo mashuhuri wa Iran, Abolfazl Yaghoubi aliteuliwa kuwa kiungo mwenye thamani zaidi katika duru ya 6 ya mashindano hayo, yanayojulikana kama Asian Club Taekwondo Championship. Kadhalika mkufunzi wa Varamin, Payam Khanlarkhani alitangazwa kuwa kocha bora wa mashindano hayo kwa upande wa wanaume huku Azadeh Yasaei anayeichezesha Kan akitawazwa kuwa kocha bora wa mashindano hayo kwa upande wa wanawake.

Riadha: Medali 3 zawaendea Wairani Qatar

Wanamichezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametwaa medali 3 ikiwemo 1 ya dhahabu katika duru ya 7 ya Mashindano ya Ubingwa wa Riadha barani Asia huko Qatar. Siku ya Ijumaa, Hassan Taftian mwenye umri wa miaka 22 na Reza Ghasemi mwenye umri wa miaka 28, walimaliza katika nafasi ya kwanza na ya pili katika mbio za mita 100 na kutwaa medali za dhahabu na fedha. Katika mashindano hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Asia Dome katika mji mkuu wa Qatar, Doha; Wairani hao walimaliza kwa kutumia sekunde 6.56 na 6.66 kwa utaratibu huo.  Mfilipino Eric Shauwn alimaliza katika nafasi ya tatu kwa kutumia sekunde 6.7 na kushinda medali ya shaba.

Kwa upande wa wanawake, Sepideh Tavakoli aliipa Iran medali ya fedha katika mchezo wa pentathlon, baada ya kukusanya jumla ya pointi 3,828. Medali ya dhahabu katika mchezo huo ilienda Uzbekistan huku Mjapani akiondoka na medali ya shaba. Pentathlon ni riadha ya kisasa ambapo mchezaji anapaswa kushiriki katika michezo aina tano; haswa ulengaji shabaha, kuogelea, mbio za nyika, mchezo wa vitara (fencing) na mashindano ya farasi ama ukipenda horseback riding. Duru ya 7 ya mashindano hayo ya kieneo yalianza Februari 19 na kufunga pazia lake Jumapili ya Februari 21. Mashindano hayo ya mabingwa wa riadha barani Asia yalivutia wachezaji 300 kutoka nchi 36, ikiwemo India, Japan, Iran, Sri Lanka, Syria na Uzbekistan.

Mieleka: Wanamieleka wa Iran washinda dhahabu Ukraine

Mwanamieleka mashuhuri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mehran Nasiri ameshinda medali ya dhahabu katika siku ya mwisho ya Mashindano ya Kimataifa ya Mieleka nchini Ukraine. Katika mpambano wa fainali siku ya Jumapili, Nasiri alimlemea Ivan Bileichuk wa Ukraine katika kitengo cha mieleka mtindo wa freestyle, kwa wanamieleka wenye kilo zisizopungua 61. Medali ya fedha ilimuendea raia wa Armenia Voldoya Frangulyyan huku Ludvik Sholinyan wa Ukraine akitwaa medali ya shaba. Muirani mwingine Saeed Dadashpour aliipa nchi hii medali ya fedha katika kategoria ya wanamieleka wenye uzani wa kilo 70 baada ya kugaragazwa na Andrey Kviatkovski wa Ukraine katika kitimutimu cha fainali. Peyman Yarahmadi aliipa Iran ya Kiislamu dhahabu nyingine katika siku ya kwanza ya mashindano hayo katika kitengo cha kilogramu 74. Mashindano hayo ya kimataifa ya Outstanding Ukrainian Memorial International, yalifunga pazia lake Jumapili nchini Ukraine

Afrika: Mazembe yatwaa Super Cup

Klabu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeshinda Kombe la Super kwa mara ya tatu baada ya kuisasambua Etoile du Sahel ya Tunisia. Mazembe walipata ushindi wa mabao 2-1 kwenye mechi hiyo iliyochezewa mjini Lubumbashi siku ya Jumamosi. Mazembe waliibuka kidedea kupitia mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji raia wa Ghana Daniel Nii Adjei mwenye umri wa miaka 27. Adjei alifunga bao la kwanza kunako dakika ya 20 na la pili dakika chache kabla ya kwenda mapumzikoni.

Hata hivyo Watunisia wa Sahel walipata bao la kufutia machozi katika dakika za mwisho kupitia kiungo Mohamed Msekni. Mazembe ambayo ni katika miamba ya soka Afrika imeshinda kombe hilo linalokutanisha mshindi wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Afrika na mshindi wa Kombe la Mashirikisho mara 3 sasa. Vijana wa Kiarabu wa Etoile ya Tunisia walioshinda Kombe la Mashirikisho (Confederation Cup) mwaka jana 2015, pia wamo katika madaftari ya kumbukumbu kwa kushinda Super Cup mara 2.

Tenisi

Nyota wa mchezo wa Tenisi Rafael Nadal wikendi hii alishindwa kutinga hatua ya nusu fainali ya kuwania ubingwa wa taji la ATP, baada ya kuzamishwa seti 3 na raia wa Uruguay Pablo Cuevas katika mashindano ya Wazi ya Rio. Mshindi huyo mara 14 wa Grand Slam alianza kwa kuongoza kwa pointi mbili kwa seti mbili lakini baadaye alianza kupoteza dira na hatimaye kufungwa seti 3 za 6-7, 7-6 na 6-4.

Na kwa kuwa asiyekubali kushindwa sio mshindani, Nadal amekubali kupoteza mchezo huo huku akisisitiza kuwa, atafanya juu chini kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza ili kufanya vyema katika michuano ijayo. Cuevas ambaye anashikilia nafasi ya 45 duniani anatazamiwa kutoana jasho na Guido Pella katika kitimutimu cha fainali.

…………………..TAMATI……………………..

Andika maoni


Msimbo salama (Security code)
Upyesha (Refresh)

Hadithi ya Uongofu (39)

Ni matarajio yangu kuwa, hamjambo wapenzi wasikilizaji na tunakutana tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu. …

Ufeministi, Itikadi na Misingi yake (26)

Assalaamu Alaykum wafuatiliaji wa kipindi hiki na karibuni kuwa nasi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki kinachokosoa itikadi ya ufeministi …

Ulaji wa Lishe Bora katika Kipindi Chote cha Maisha

Wataalamu wa Afya wanasema kuwa, awamu mbalimbali za maisha zinahitajia ulaji wa chakula wa aina tofauti. Iwapo wewe ni mtoto, …

Maua mawili ya Mtume wa Allah (31) Sauti

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh Karibuni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili Radio Tehran na wasomaji wa mtandao …